Gekul aitwa Mahakama Kuu kujitetea

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Muktasari:

  • Rufaa ya kupinga uamuzi wa DPP kufutwa kesi ya Pauline Gekul imeiva

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara wilayani Babati, imepanga kusikiliza rufaa ya kesi ya jinai dhidi ya mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul, Machi 18, 2024.

 Rufaa hiyo imekatwa na aliyekuwa mfanyakazi wa mbunge huyo, Hashim Ally anayemtuhumu mwajiri wake huyo wa zamani kumfanyia ukatili akimtuhumu kuwaelekeza vijana wake kumvua nguo na kumwingizia chupa ya soda katika njia ya haja kubwa.

Akizungumza na Mwananchi, Jumamosi Januari 27, 2024, wakili wa Hashim, Peter Madeleka amethibitishia kuhusu wito huo.

Gekul ambaye kabla ya kuibuka kwa tuhuma hizo dhidi yake alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumamosi Januari 27, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital kwa simu kuhusu hilo, amesema hajaipata hati hiyo.

Pia, amehoji inakuwaje nyaraka za Mahakama zinawahi kupatikana kwenye mitandao wakati mhusika hajaipata.

“Mimi sijapata brother (kaka). Najua mambo ya Mahakama yana taratibu zake, inakuwaje nyaraka za Mahakama zinawahi kwenye mitandao kabla mhusika hajaipata? Kwa hiyo sifahamu chochote,” amesema Gekul.

Katika rufaa hiyo ya jinai namba 577, Hashim anapinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati kuifuta kesi yake aliyokuwa amemfungulia mbunge huyo, kufuatia taarifa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya wito wa  Mahakama hiyo kwa Gekul iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Januari 18, mwaka huu, ambayo Mwananchi imeiona nakala yake jana,  rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa na Jaji Stephen Magoiga.

“Fahamu kwamba siku ya Machi 18, 2024, saa 3:00 asubuhi imepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na mrufani katika kesi iliyotajwa hapo juu (Hashim Ally), mbele ya Jaji S.M Magoiga,” inasomeka hati hiyo kwa tafsiri isiyo rasmi.

Hatua hiyo ya kupangwa kusikilizwa kwa rufaa hiyo imekuja huku DPP Sylvester Mwakitalu, akiwa ameshaweka msimamo wake kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa hivyo, yeye ndiye mwenye dhamana na hajashindwa kufungua upya kesi hiyo.

Hata hivyo, msimamo na hoja ya DPP Mwakitalu zilipigwa na wakili Madeleka aliyedai kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kihalali kwa mujibu wa sheria iliyotumika na kusisitiza, DPP katika mazingira ya kesi hiyo hana mamlaka ya kuingilia na kutoa uamuzi wa kuiondoa wakati hakuwa mdaawa.

Hivyo, usikilizwaji na uamuzi wa rufaa hiyo ndio utakaomaliza ubishi baina ya DPP kwa upande mmoja na wakili Madeleka kwa upande mwingine iwapo kesi hiyo ilifunguliwa kihalali kwa mujibu wa sheria au haikuwa halali.


Awali, Hashimu alimfungulia Gekul kesi hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Babati chini ya kifungu cha 128(2) na (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),  kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022, kwa msaada wa wakili  Madeleka.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya malalamiko ya kesi hiyo, Gekul alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la shambulio na kusababisha madhara kwa mwili chini ya kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marekebisho ya mwaka 2022.

Hashimu aliyekuwa mfanyakazi wa Gekul katika hoteli yake ya Paleii Lake View Garden, alidai yeye Gekul na watu wengine ambao hawako katika malalamiko hayo, Novemba 11, 2023, mjini Babati Mkoa wa Manyara walimuita Hashim na kumuweka kizuizini.

Alidai baada ya kumuweka kizuizini walimtishia kwa silaha ya moto, walimvua nguo na kumshambulia kwa kumlazimisha kukalia chupa ya soda ili iingie katika njia yake ya haja kubwa.

Hata hivyo, Desemba 27, 2024, siku ya kwanza kutajwa, kesi hiyo ilifutwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Victor Kimario; baada ya DPP kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea nayo kwa mamlaka yake chini ya kifungu cha 91 (1) cha CPA.

Akizungumza baada ya uamuzi huo wa kuifuta kesi hiyo, wakili Madeleka ambaye alikuwa amefika mahakamani hapo kumwakilisha Hashim alieleza kutokuridhishwa na uamuzi huo.

Siku hiyohiyo alichukua hatua ya awali ya mchakato wa kukata rufaa kuupinga uamuzi huo.

Baadaye aliwasilisha sababu tano za rufaa kupinga uamuzi huo, ambazo ndizo Mahakama itakazozisikiliza na kuzingatia katika uamuzi wake iwapo ilikuwa ni halali kesi hiyo kufutwa au la.

Katika sababu ya kwanza anadai kuwa, hakimu alikosea kuifuta kesi hiyo kwa kushindwa kuzingatia maelekezo ya sheria chini ya ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Nchi inayotoa haki ya kusikilizwa.

Sababu ya pili Hashim anadai kuwa, hakimu alikosea kwa kuzingatia maelekezo ya sheria chini ya Ibara ya 58B (4) (a), (b). (c) na (5) ya Katiba ya nchi huku katika sababu ya tatu akidai kuwa, hakimu alikosea kwa kushindwa kuzingatia maelekezo ya sheria chini ya kifungu cha 228(1) cha CPA.

Katika sababu ya nne Hashim anadai kuwa, hakimu alikosea kwa kushindwa kuzingatia  kwamba,  wakati anatoa amri yake ( kuifuta kesi) mshtakiwa (Gekul) hakuwepo mahakamani.

Katika sababu ya tano anadai kuwa hakimu alikosea kwa amri yake kuzingatia nolle prosequi (taarifa ya DPP ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo) ambayo haikuwasilishwa mahakamani sawasawa (kwa mujibu wa taratibu za kisheria zilizowekwa).


Akizungumza na Mwananchi siku moja baada ya kesi hiyo kufutwa, DPP Mwakitalu alisema ameamua kuiondoa kesi hiyo mahakamani kwa kuwa, kwanza ofisi yake inaendelea na mchakato wa mashtaka dhidi mbunge huyo kwa kuwa ndiyo yenye dhamana.

“Kwa hiyo tumeiondoa hiyo kwa sababu hatuwezi kufanya huku sisi halafu na mtu mwingine tena naye anaendesha huko,”alisema DPP Mwakitalu.

Pia, alisema kuwa ili kumshtaki mbunge lazima kwanza yeye atoe ridhaa na hata kama angeiacha kesi hiyo aliyeifungua asingefanikiwa kwa sababu hapakuwa na ridhaa  ya DPP.

DPP Mwakitalu alifafanua kuwa mtu binafsi anaweza kufungua na kuendesha kesi baada ya kuomba kwanza ridhaa mahakamani, lakini akasema kesi hiyo hawakuomba ridhaa hiyo mahakamani.

Alisema kifungu kilichotumika kufungua kesi hiyo hakihusiani na mashtaka binafsi na kwamba kifungu kinachoruhusu mashtaka binafsi ni kifungu cha 98.

Kuhusu hatima ya kesi hiyo DPP Mwakitalu alisema kuwa, jalada la upelelezi wa tuhuma zinazomkabili mbunge huyo limeshafika ofisini kwake lakini bado hajapata muda wa kuliangalia kwa kuwa alikuwa na msiba (msiba wa aliyekuwa Naibu DPP, Joseph Pande).

“Nitakuwepo ofisini labda wiki ijayo. Kwa hiyo nitaliangalia halafu tutafanya uamuzi wa kumshtaki ama la. Kama kuna ushahidi wa kutosha tutashtaki. Hatujashindwa majukumu yetu mpaka mtu atusaidie,” alisema Mwakitalu kwa msisitizo.


Majibu ya wakili Madeleka

Hata hivyo, wakili Madeleka alipinga maelezo na msimamo huo wa DPP akisema malalamiko yaliyowasilishwa mahakamani dhidi ya mbunge huyo yalipelekwa kwa mujibu wa sheria na vifungu walivyovitumia havisemi hayo aliyoyasema DPP.

Alisema kifungu hicho kinaelezea mtu yeyote kuwasilisha malalamiko yake kwa hakimu hata kwa mdomo dhidi ya mtu yeyote bila kujali kama ni mbunge au waziri.

Alisema kwa maoni yake, kesi hiyo ilifunguliwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu uliotumika kuipeleka mahakamani upo kisheria, DPP hana mamlaka ya kuiondoa.

“Kwa sababu shauri hilo lilishaamuriwa kama lilivyoamuriwa jana, sisi tumeshachukua hatua za kukata rufaa ili Mahakama Kuu ione kama kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa ilikuwa halali,” alisema Madeleka.

“Mahakama Kuu pia, itaona kama DPP ambaye hakuwa sehemu ya kesi hiyo kuingilia na kuifuta ni sahihi au si sahihi na hakimu kuifuta ni sahihi au si sahihi.”