Nabii Suguye aeleza mbinu kukabili mmomonyoko wa maadili

Nabii Nicolaus Suguye akizungumza na vyombo vya habari kuelekea sherehe za maadhimisho ya Kanisa lake kutimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake itakayofanyika Aprili Mosi mwaka huu. Picha na Tuzo Mapunda

Muktasari:

  •  Kanisa lake kuadhimisha miaka 17 tangu lilipoanzishwa Februari 2007.

Dar es Salaam. Nabii wa Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule, Nicolaus Suguye amesema suala la maadili ni changamoto kubwa, na ili kupata suluhisho ni lazima viongozi, wasio na nafasi kuungana kupambana kuanzia ngazi ya familia.

Amesema changamoto hiyo si ya kuisha leo, na imekuwa ikiongezeka kwa vijana hadi watu wazima wenye nafasi zao, akitoa mfano wa mavazi na hata kuzungumza.

Amesema hayo Dar es Salaam leo Machi 27, 2024 kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kilele cha miaka 17 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo Februari 2007. Yatafanyika Aprili Mosi, 2024.

“Tatizo hili si tu limekuwa kero katika makanisa bali hata kwenye taasisi nyingi ikiwemo, serikalini. Kinachotakiwa ni viongozi na hata wasio viongozi kuungana kupambana nalo kuanzia ngazi ya familia,” amesema. 

Amesema wazazi na walezi hawana budi kuwa vinara wa maadili; tabia zao ziende kwa watoto pamoja na wafanyakazi wa shughuli za ndani.

“Tukianzia ngazi ya familia tutaanza kuwa na maadili mema, tutafanikiwa kwa sababu wanaokuja makanisani, misikitini au kazini ni walewale wanaotoka ndani ya familia,” amesema.

Amesema kwa kutambua hilo, amekuwa akitoa mafundisho ya mara kwa mara kuhusu mahusiano ya ndoa yanayopaswa kutekelezwa ndani ya jamii na hata wazazi kutowachokoza watoto wao.

Amesema miaka kadhaa ya nyuma Bunge lilipokuwa na mchanganyiko wa wabunge wa upinzani wengi na wale wa chama tawala (CCM) ilishuhudiwa changamoto zao za kimalezi, akisema wapo waliomjibu Spika kwa kauli zisizofaa au mbunge mwenzake.

Suguye amesema viongozi wa dini na asasi nyingine wanatakiwa kushikamana kupambana na changamoto ya maadili hasa katika mavazi na kauli.

“Lugha ya staha inapaswa kwenda kulingana na rika, huwezi kuongea na baba yako kama unaongea na mtu mtaani. Kuna misingi ya kuzungumza na baba au mama, huwezi kutumia lugha ya mtaani,” amesema.


Kuhusu maadhimisho

Suguye ambaye kanisa lake limejengwa eneo la Matembele Mwisho, Ukonga amesema shughuli hiyo itafanyika kanisani hapo na  mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa.

Amesema kanisa hilo limetoa misaada kwa watoto yatima na wajane kwa kuwapatia mavazi na chakula.

Amesema wamesaidia upatikanaji wa umeme katika Shule ya Sekondari ya Kivule na ujenzi wa ukuta. Pia wameisaidia Shule ya Msingi ya Kivule kujenga madarasa.

Pia wamesaidia kuboresha barabara na kutoa msaada wa vifaatiba katika hospitali ya Kivule.

Suguye amesema hakuna huduma isiyokuwa na changamoto akieleza ndani ya miaka 17 ya kanisa hilo amepitia nyingi, lakini kubwa kwake ni kubezwa na kudharauliwa alipoanza kutoa huduma.

Hata hivyo, amesema  kukubalika na kukataliwa kwake kwa upande fulani kulimjenga hadi kufikia alipo sasa.