Kanisa la Nabii Suguye lafunguliwa, atuma ujumbe serikalini

Muktasari:

  • Kanisa la huduma ya The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule- Matembele ya Pili limefunguliwa na kuendelea kutoa huduma baada ya kufungwa kwa miezi mwili.

Dar es Salaam. Nabii wa Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule- Matembele ya pili jijini Dar es Salaam, Nicolaus Suguye amesema baadhi ya watu hawapendi kazi anayofanya huku akitoa wito kwa watendaji wa umma kuwa makini nao na mbinu wanazotumia kutaka kumgombanisha na mamlaka.

Suguye ametoa kauli hiyo leo Februari 05, 2023 baada ya kanisa lake kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma za kiroho kufuatia kufungiwa kwa kipindi cha miezi miwili kwa madai kwamba taasisi hiyo haikuwa na usajili rasmi.

Kanisa hilo lenye waumini zaidi ya 4,000 lilifungiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa halijapata usajili rasmi, isipokuwa barua ya usajili wa awali inayoruhusu kufanya huduma sehemu moja bila kualika wageni kutoka nje.

Pia, ilieleza kuwa lilifungua matawi na kufanya makongamano, huku Serikali ikifanya uchunguzi wa mwenendo wake. Desemba 22, 2022 Mwananchi lilishuhudia askari wakililinda kanisa hilo, huku uzio wake ukiwa umezungushiwa utepe.

Akiwaeleza leo waumini wake waliojitokeza kwenye ibada ya kwanza tangu kupewa kibali cha kuendelea kufanya kazi hiyo amesema watumishi hao wawe makini na watumishi wanafiki waliovaa mavazi ya kitumishi wanaotaka kumgombanisha.

“kuna watu hawapendi ninachokifanya kuiombea Serikali na Taifa kwa ujumla naomba muelewe hivyo wanahisi kama mimi najipendekeza,

“Ujumbe wangu kwa watendaji mliopo Serikalini kuweni makini na watu wanaowaingiza kwenye vita ambavyo hamvijui sawasawa kwa sababu unapoanza kumshambulia Nabii wa kweli unapambana na mafuta ya Mungu,” amesema Suguye.

Amesema kupambana na mafuta ya Mungu hautasalimika hivyo vita ya kiroho itawaandama hadi kwenye familia zao.

“Tambueni nafasi mlizoshika ni dhamana kumbukeni kuna wenzenu walitangulia kabla yenu na wakaondoka na wako na familia zao, utakapokuja mtaani huku utatukuta akina Suguye bado tupo,”amesema


Taarifa za kufungwa kanisa hilo

Amesema taarifa za kufungiwa kanisa hilo alizipata kwa njia ya simu akiwa Marekani Desemba tisa mwaka uliopita akiambiwa na wasimamizi wake kwamba Jeshi la Polisi limefika kufunga kanisa hilo ndipo alipowataka waachwe watekeleze azma yao na kwamba akirejea atafuatilia kujua shida nini.

Amesema aliamua kukaa kimya huku akiwaasa waumini wake wasitume taarifa mbaya kwenye mitandao huku akieleza halikuwa jambo rahisi kuwanyamazisha waumini wake na kuwataka waabudie manyumbani kwao.


Kuhojiwa na Polisi

Amesema “baada ya kufika  nchini Januari 16 mwaka huu niliitwa Kituo cha Polisi Kanda maalumu kuhojiwa nilitoa taarifa zangu pale na nikaambiwa  kwamba usajili wa kanisa langu haukuwa sawa jambo nililoshangaa sana na miaka yangu yote hii,”

Suguye amesema kingine alichoelezwa na Polisi kwamba anahatarisha amani huku akieleza suala hilo lilimshangaza ndipo alipoandika maelezo yake na kuondoka kurudi nyumbani kwake.

“Kufika nyumbani taarifa za uongo zimeanza kusambaa kwenye mitandao Suguye kakamatwa na madawa ya kulevya na amekamatwa anahojiwa na Polisi niliendelea kukaa kimya nikijua ukweli utafahamika,”amesema

Amesema alishindwa kuwajibu kwakuwa yeye siyo mwanasiasa huku akijiuliza maswali kama kuna watumishi wanaodiriki kuacha madhabau zao na kuanza kusambaza taarifa za uongo na uchonganishi.