Mitandao ya kijamii yatajwa kuleta ukakasi

Muktasari:

  • Mitandao ya kijamii wakati mwingine imetajwa kuleta ukakasi na kutoa taarifa za watu binafsi kwa kuingilia faragha zao, huku baadhi ya taarifa zikishughulikiwa na sheria ya mitandao.

Dar es Salaam. Mhariri wa Gazeti la Mwananchi Kanda ya Ziwa, Peter Saramba amesema maendeleo ya teknoljia na matumizi ya mitandao wakati mwingine inaleta ukakasi katika maisha ya kawaida.

“Wakati mwingine kuna matumizi ya kutoa taarifa za watu binafsi katika mitandao ya kijamii na inaingilia faragha za watu kwa kutoa picha zinazotweza utu wa watu, taarifa za uzushi na kuibua taharuki,” amesema.

Kauli hiyo ameitoa leo Desemba 13, 2023 wakati akichokoza mada kwenye Mwananchi Space iliyoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) ikibebwa na mada isemayo, Nini mchango wa mitandao ya kijamii katika kufichua taarifa kwa umma.

Amesema licha ya kutoa taarifa hasi lakini kuna taarifa zinashughulikiwa na sheria ya makosa ya mitandao.

"Nafasi ya mitandao na maendeleo ya teknolojia imeleta unafuu mkubwa katika mawasiliano kufichua mambo ambayo wakati mwingine wahusika wasingependa wafichuliwe," amesema Salamba.

Amesema kuna wakati inafika wanadhani kuwa ile nafasi ambayo ilikuwa ikitumika na vyombo vya habari vya kipindi kilichopita, waandishi walikuwa wakifanya uchunguzi na kuripoti kwa kina sasa mitandao ya kijamii imekuwa ni sehemu muhimu ya kujua habari hizo.

Pia amesema mchango wa mitandao ya kijamii ni mkubwa katika kuhabarisha, kusaidia umma ambayo huenda wahusika wasingependa yafichuliwe.

Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko amesema mchango wa mitandao ya kijamii katika kufichua taarifa kwa umma umekuwa mkubwa sana, ukijaribu kupima hasi na chanya basi chanya inaweza kufika asilimia 75.

Amesema bahati mbaya watu huwa wanalalamikia mitandao hii bila kutazama faida zake, faida kubwa ni kutazama jamii inayoshinda mitandaoni ni kubwa zaidi na inaweza kuzidi wale wanaotumia vyombo vya habari vya zamani.

"Tunajivunia kuwa wafuatiliaji wetu wako mitandaoni sana hivyo ni wazi kuwa uwepo wa mitandao hii inatumika kama njia ambayo watu wanaweza kujadiliana, kupata habari, kupata hisia na hii inaonyesha kuwa ujumbe unafika kwa haraka," amesema Soko.

Amesema hivi karibuni kumekuwa na matukio ambayo yaliibuliwa na kuleta mchango mkubwa ikiwemo lile la ukatili lililofanywa na aliyekuwa Naibu waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul, chanzo ilikuwa mitandao, inaonyesha jinsi gani watu walivyolipokea na hadi mamlaka ilivyolishughulikia.

Ameongeza kuwa Desemba 3, mwaka huu kulikuwa na tukio la Hanang amesema mitandao ilivyokuwa ikitumika kutoa taarifa hata mamlaka zilivyokuwa zikitumia mitandao kuhabarisha kinachoendelea.

Pia amekumbushia tukio la Panyaroad la Mei 2022 nalo lilisomwa mtandaoni hadi IGP kusimama na kulikemea.