Serikali kuwashughulikia waliomzushia kifo Dk Mpango

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza kabla ya kufungua kongamano la saba la taifa la Tehama jijini Dar es Salaam jana Desemba 10, 2023. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa wale waliohusika kutangaza uvumi wa kifo cha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango katika mitandao ya kijamii.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa wale waliohusika kutangaza uvumi wa kifo cha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango katika mitandao ya kijamii.

Waziri Nape amesema hayo leo Jumapili Desemba 10, 2023 kupitia akaunti yake ya X (zamani Twitter) muda saa chache baada ya Dk Mpango kuwataka Watanzania kutumia vizuri mitandao ya kijamii na kuachana na kuzusha habari za uongo.

Dk Mpango hakuonekana hadharani kwa takribani mwezi mmoja jambo lililoibua minong’ono kuwa anaumwa huku wengine wakidai kuwa amefariki.

Nnauye amesema ameelekeza vyombo vyote vinavyohusika kuchukua hatua ili iwe mfano na kujenga jamii inayoheshimu uhuru wa kila mtu.

“Pole sana Mhe Makamu wa Rais. Tumekusikia. Kwakuwa tuna sheria zinazoelekeza mitandao itumike vizuri na kwakuwa tuna taasisi na watu wa kusimamia sheria hizi, bila kuathiri uhuru wa watu, TUTACHUKUA HATUA kutokomeza matumizi haya mabaya ya mtandao! Naamini wote watatuelewa!

“Uhuru wowote unapoingilia uhuru wa mwingine ni uvunjaji wa sheria, hatuwezi kujenga jamii inayoona hilo jambo ni la kawaida,”ameandika Nape.

Dk Mpango wakati wa kumkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kuhutubia katika hafla ya kupokea hundi ya mchango wa waathirika wa maafa ya Hanang leo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma alisema kuzushiwa kifo kuna athari kubwa kwa familia.

“Unajua ukisema huyu mzee,walisema amekata moto na wengine wanaweka picha yangu iliyochongwa na mshumaa unawaka, Rais sisi viongozi ni binadamu tuna watoto, wajukuu, famiia na marafiki na wafanyakazi wenzetu hivyo kufanya hivyo inaweka taharuki kubwa,”alisema.