Maajabu ya mbuzi wanaokula vyakula vya binadamu Morogoro

Mbuzi wakiwa katikati ya mji katika duka Mtaa wa mtoni . Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu mjini Morogoro kumekuwa na makundi ya mbuzi wanaozurura katikati ya mji na kuonyesha maajabu yao kwa kula chipsi, maandazi, kupishana na magari na kuvuka kwenye alama za usalama barabara (zebra) huku wananchi wakiwahusisha na imani za kishirikina.

Morogoro. Kuwa uyaone, ni maneno ya wahenga unayoweza kuoanisha na . kile kinachofanywa na mbuzi wanaozurura mjini hapa, wakila vyakula ambavyo huwezi kutarajia mnyama kama huyo kuvila.

Inafahamika wazi kwamba vyakula vya mbuzi ni pamoja na majani, pumba na baadhi ya nafaka. Hata hivyo, mbuzi wanaoonekana na kuishi katikati ya mji wa Morogoro wamekuwa na tabia tofauti na mbuzi wengine waliozoeleka kwenye jamii hasa kutokana na vyakula wanavyokula na maisha yao kwa ujumla.

Hata hivyo, mbuzi hao wa Morogoro wanakula wali, chapati, maandazi, chipsi na vyakula vingine ambavyo kwa asili vinaliwa na binadamu na siyo wanyama wafugwao au wanyamapori wengine.

Ofisa Kilimo na Mifugo wa Manispaa ya Morogoro, Dk Tito Kazige ameeleza sababu za mbuzi hao kubadili tabia zao za asili na kuishi maisha mengine, jambo ambalo linastaajabisha watu ambao hawajazoea hali hiyo.

Mbuzi hao wakivuka barabara katika moja ya mitaa Morogoro. Picha na Hamida Sharrif

Wenyeji na wanaoishi maeneo ya Sultani, Sabasaba, Mtaa wa Uhuru na Mtaa wa Mtoni wameeleza namna wanavyokerwa na mbuzi hao, pamoja na maajabu waliyonayo licha ya kwamba hawajulikani ni mali ya nani.

Mkazi wa Mtaa wa Mtoni, Innocent Mtuli amesema mbuzi hao zaidi ya 30 wamekuwa wakizurura mtaani hapo hadi saa 2 usiku na kulala kwenye vibaraza vya nyumba za watu au nyumba za wageni, hivyo wamekuwa wakiacha kinyesi pamoja na mkojo inayotoa harufu kali isiyoisha.

“Mtaa huu nyumba nyingi zina maduka, magenge, mabanda ya biashara za vyakula (mama na baba lishe), mabanda ya chipsi na nyumba za kulala wageni. Hawa mbuzi kutwa nzima wanazunguka kwenye maeneo hayo, wakikuta chipsi kwenye sahani au kwenye beseni wanakula, ukiacha duka wazi wanakula biskuti, maandazi, karanga na kutia hasara watu,” amesema Mtuli.

Amesema miaka ya nyuma mbuzi hao walikuwa wachache lakini kwa sasa wanaonekana kuongeza kila siku na wanatembea kwa makundi, huku wakipita mtaa mmoja hadi mwingine.

Mkazi mwingine wa mtaa huo ambaye ni dereva wa bodaboda, Chaulembo Chaulembo amesema mbuzi hao wamekuwa wakionekana nyakati za mchana na jioni na wamekuwa wakipita pembeni mwa barabara.

“Hawa mbuzi wanajua kutembea barabarani kama binadamu, wanapishana na magari na hawavuki ovyo, wanatafuta sehemu zenye michoro ya zebra ama kwenye matuta ya barabarani,” amesema Chaulembo.

Kuhusu chakula wanachokula, Chaulembo amesema kuwa wamekuwa wakichukua mabaki ya ugali, viporo vya wali vinavyomwagwa kwenye ndoo za taka zinazowekwa mwenye nyumba za watu.

“Mbuzi hawa hatujawahi kuwaona wanakula majani, wao kutwa kwenye viroba vya kuhifadhia taka, wakikuta ugali umetupwa au kiporo cha wali kimetupwa,  wanakula, wakipita kwenye banda la chipsi, kabati ya kuwekea ikiwa chinichini wanapanda, wanakula,” amesema Chaulembo.

Said Ally, mkazi wa Barabara ya Sabasaba, ameeleza maajabu ya mbuzi hao ambao anasema wamekuwa wakizaliana siku hadi siku na hajawahi kusikia wameibwa wala kugongwa na chombo chochote cha usafiri.

“Kila siku lazima waje hapa kwenye kijiwe chetu cha bodaboda, wakifika hapa, wakimkuta mtu ameagiza chakula watamsumbua hadi kero, kuna siku mtu kaagiza chai, mbuzi wamekuja wakanywa ile chai na mchana wamerudi tena, wamekuta kaagiza wali na ndizi mbivu, alipojisahau kidogo walikula ndizi chana nzima,” amesema Ally.

Kuhusu imani za kishirikina zinazohusishwa na mbuzi hao, Ally amesema naye amewahi kusikia taarifa hizo, hata hivyo haamini kwa sababu hana uhakika nazo.

“Niliwahi kusikia kwamba watu wa manispaa waliwahi kuwakamata hawa mbuzi lakini walipokwenda kuwashusha kwenye ofisi za manispaa, waligoma kushuka kwenye gari, hali iliyowafanya watu wa manispaa kuwarudisha hawa mbuzi hapa mtaani. Tangu wakati huo, sijawahi kusikia kama manispaa walifanya tena hiyo kazi ya kuwaondoa,” amesema Ally.

Fundi viatu katika Mtaa wa Sabasaba ambalo mbuzi hao wamekuwa wakionekana, Juma Shabani amesema kila siku na mvua inaponyesha wamekuwa wakijibanza kwenye vibaraza vya nyumba, ikikata wanarudi tena barabarani.

Shabani amesema hajawahi kumuona mmiliki wa mbuzi hao lakini anaamini kuwa watakuwa na mwenyewe, ingawa  hajui kwa nini aliamua kuwaacha katikati ya mji wajichunge wenyewe.

Kutokana na changamoto hiyo ya mbuzi hayo, Ofisa Kilimo na Mifugo wa Manispaa ya Morogoro, Dk Tito Kazige amekiri kuwepo kwa mbuzi hao wanaozurura katikati ya mji bila kuwa na mchungaji.

Amesema mbuzi hao wanatembea katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza lipo Mtaa wa Sabasaba, kundi la pili lipo Mtaa wa Uhuru na Mlapakolo na kundi la tatu lipo maeneo ya mtawala.

Dk Kazige amesema kuwa makundi hayo yamekuwa yakitembea kwenye mitaa mingine na kwa kuwa katikati ya mji hakuna majani ya kutosha wamekuwa wakila vyakula ambavyo sio vile vilivyozoeleka kuliwa na mbuzi.

“Mbuzi ni mnyama wa kufugwa na chakula chake ni majani, pumba na nafaka mbalimbali, lakini kwa kuwa hawa wapo katikati ya mji, wanajikuta wanapoteza ile asili yao na maisha yao kwa ujumla, ndiyo maana wanakula vyakula kama chips, ugali, wali, maandazi na vingine anavyokula binadamu,” amesema Dk Kazige.

Amesema hata mfumo wa maisha ya mbuzi hao wanaozurura, umebadilika kutokana na mazingira na kuwa karibu na binadamu na ndiyo maana wanaweza kupishana na magari barabarani na kujua namna ya kuvuka barabara.

Akizungumzia mikakati ya kuwaondoa mbuzi hao, Dk Kazige amesema changamoto kubwa ni namna ya kuwapata wamiliki kwa kuwa kumekuwa na mawazo ya imani za kishirikina yaliyojengeka kwenye jamii inayoishi nao.

“Unaweza ukaamua kufanya operesheni ya kuwaondoa hao mbuzi, lakini ukifika mtaani unauliza nani mwenye hawa mbuzi, cha kusikitisha, hakuna hata mtu mmoja anayeweza kukutajia mmiliki wa hao mbuzi. Sasa, kwetu sisi kama maofisa mifugo tunashindwa kuendesha operesheni hiyo, kwa kuwa ile ni mali, hivyo mmiliki asaini fomu ambayo inamtaka kisheria asaini,” amesema Dk Kazige.

“Nikiendesha kampeni ya kuwaondoa mbuzi au mifugo yoyote bila ya mmiliki kusaini ile fomu, baadaye anaweza akajitokeza na kusema mbuzi wake wameibwa na ikataja idadi kubwa ya mifugo tofauti na ile mliyoichukua, na hapo ndipo changamoto itakapokuwa kubwa maana kama manispaa mtatakiwa kulipa hiyo mifugo,” ameongeza Dk Kazige.

Amesema ili shughuli hiyo ifanikiwe, lazima mifumo ya taasisi zinazosimamia sheria za mifugo isomane na operesheni hiyo ifanywe kwa ushirikiano baina ya halmashauri na wananchi kuwabaini wamiliki wa mbuzi hao.

Hata hivyo, Dk Kazige amesema kuwa mbali ya changamoto ya mbuzi kuzurura katikati ya mji, pia ipo mifugo mingine  wakiwemo mbwa, paka na ng'ombe, hata hivyo kwa kiasi kikubwa wamewapunguza.

Kwa upande wa mbwa, Dk Kazige amesema idara ya mifugo katika halmashauri hiyo imeongeza kasi ya uchanjaji wa kichaa cha mbwa, hasa kwa mbwa wanaofugwa na wanaozurura.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, idara hiyo ya mifugo imefanikiwa kuchanja zaidi ya mbwa 8,000 sawa na asilimia 80 ya mbwa wote waliopo Manispaa ya Morogoro.

Amesema idara hiyo imelazimika kuongeza kasi ya uchanjaji kupitia kampeni ya kuchanja bure baada ya kubaini kuwa changamoto ya kichaa cha mbwa bado ni kubwa, hasa katika wilaya ya Morogoro kutokana na kuwa na maeneo mengi ya mapori yenye wanyamapori kama mbweha, chui, duma na Simba.