Dk Biteko: Umeme wa joto ardhi kuongeza nguvu kwa vyanzo vilivyopo

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la uendeshaji wa Joto Ardhi (TGDC), Mathew Mwangomba (katikati) akiemuelekeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini Dk Biteko Biteko sehemu ya uzalishaji wa maji ya moto yanatoka ardhini na kuzalisha nishati ya umeme .

Kunradhi Dk Biteko

Jana tuliripoti habari kuhusu Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko baada ya kukagua vyanzo vya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani Mbeya. Katika habari hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti, gazetini na mitandao yetu ya kijamii ilikuwa na nukuu inayosema:

“Kwa sasa hatuwezi kuzungumza suala la umeme litakwisha lini, kama Serikali nikiwepo mimi na Rais Samia Suluhu Hassan hatupendi kabisa kuona kunakuwepo na tatizo la umeme nchini. Hivyo, tunafanya kila jitihada kuhakikisha linakwisha kwa kuiboresha miradi ya nishati ya joto ardhi nchini,” amesema.

Nukuu hii sio sahihi na imetumika kimakosa kwa sababu Dk Biteko kwenye mazungumzo yake hakugusia suala hilo. 

Tunaomba radhi kwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Wizara ya Nishati na kwa wasomaji wetu kutokana na upotoshaji huo na usumbufu uliojitokeza.

Mhariri

Hiki ndio alichozungumza Dk Biteko

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amesema Serikali imeamua kwa dhati kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi ili kuhakikisha nchi inazalisha nishati hiyo ya  kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Amesema chanzo hicho cha umeme kitaongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya maji na gesi asilia.

Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati aliyasema hayo jana Jumanne Februari 20, 2024, baada ya kukagua vyanzo vya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani Mbeya, ambako  alifuatana na viongozi mbalimbali akiwamo  Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera.

"Miradi hii ya Jotoardhi sasa lazima ianze, tutaanza na megawati 10 hapa Kiejo-Mbaka na Ngozi tutaanza na megawati 30 huku nyingine zikifuata, na hii inajumuisha miradi mingine kama wa Jua wa Kishapu (150 MW) ambao, umeanza kutekelezwa, miradi ya umeme wa upepo ukiwemo wa Makambako na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi,” amesema Dk Biteko.

Akizungumzia changamoto ya umeme, amesema inatokana na vyanzo vya vilivyopo nchini kwa muda mrefu sasa kujikita kwenye makundi matatu tu ambayo ni maji (570MW), mafuta na gesi asilia.

Amesema kwa sasa, vyanzo vya umeme vinatokana na gesi asilia na maji ambavyo bado havitoshelezi mahitaji kutokana na kuzidi kukua kwa maendeleo.

Dk Biteko amesema idadi ya watu inayozidi kuongezeka na ukuaji wa miji umeongeza mahitaji ya matumizi ya umeme na kuonekana kuwa  sasa ni hitaji muhimu na si anasa.

Amesema pamoja na kutegemea megawati 235 kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) na megawati 27 kutoka Rusumo, maboresho ya mitambo mingine ya umeme yanaendelea katika vituo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema Serikali imeshaamua kutekeleza vyanzo vingine vya umeme vikiwemo vya jotoardhi, jua na upepo kwa sababu vipo na kinachohitajika ni kuvipa nguvu. 

Hivyo, amesema tayari amewaelekeza watendaji wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), kufanya kazi zinazoleta matokeo badala ya maneno tu, kwa kuwa Serikali inatafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo na wajibu wa watendaji wa taasisi hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa.

Dk Biteko amesema Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona Watanzania wanapata huduma  bora katika sekta zote, wanatolewa kwenye umaskini, vitendo na siyo maneno, anataka kuona watu wanahudumiwa na kufuatwa walipo, wanasikilizwa shida zao na kutatuliwa.

Kwa maana nyingine, Naibu waziri mkuu huyo amesema Rais Samia anataka utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali iangalie miaka mingi mbele na si muda mfupi, hivyo ametoa uhakika kwa wananchi kuwa miradi hiyo ya Jotoardhi itatekelezwa.

“Tumemsikia Mtendaji Mkuu wa TGDC, Mathew Mwangomba amesema utazalisha megawati 60, huku awamu ya kwanza wataanza na megawati 10 sasa kinachohitajika ni fedha. Niwaahidi tu mimi na Rais Samia Suluhu Hassan tunaleta fedha, ili kuwekeza kwenye uzalishaji wa nishati katika mradi huu.

“Mimi na Rais, Dk Samia Suluhu Hassan haturidhishwi na hali ya kukatika kwa umeme, sasa tumeona ni vyema tukawa na vyanzo vingine vitakavyozalisha umeme na kuwezesha  upatikanaji wake kwa uhakika,” amesema Dk Biteko.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko aliwapongeza  viongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo pamoja na ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa Serikali na wabunge wa mkoa huo.

Awali, Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba amesema kampuni hiyo ina miradi mitano ya kipaumbele nchini ambayo ni Kiejo-Mbaka, Ngozi, Songwe, Ruhoi na Natron.

Amesema kwa Mkoa wa Mbeya, miradi ya kipaumbele ni Ngozi na Kiejo-Mbaka ambako mradi wa Ngozi unatarajiwa kuzalisha megawati 70 na Kiejo-Mbaka unatarajiwa kuzalisha megawati 60.

Katika mradi wa Ngozi, amesema utatekelezwa kwa awamu huku ya kwanza ikitarajiwa kuzalisha megawati 30 na fedha zimeshapatikana.

Amesema mradi huo wa awali utakaozalisha  megawati 30, utagharimu Dola za Marekani milioni 144 (Sh369 bilioni).

Kuhusu mradi wa Kiejo-Mbaka, amesema unatarajiwa kuzalisha megawati 60 na zitaanza kuzalishwa megawati 10, utekelezaji wake utagharimu Dola 75.64 milioni za Marekani (Sh175.88 bilioni).

Amesema katika kuhakikisha nishati ya Jotoardhi inapatikana Tanzania, TGDC imechonga visima vifupi vya mita 300 ambavyo viliwezesha kupatikana kwa joto la takribani 75 na hii ikithibitisha kwamba, kuendelea kuchimbwa kwa visima hivyo kuanzia mita 1500 hadi 1900 itapatikana joto la kutosha kuweza kuzalisha umeme.

“Nishati ya Jotoardhi ina umuhimu mkubwa nchini kwa sababu ni ya hakika, endelevu na salama hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mwangomba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Homera amemhakikishia Dk Biteko kuwa, Mbeya inamuunga mkono Rais, Samia katika kulinda vyanzo vyote vya umeme vinavyogundulika pamoja na utunzaji wa mazingira, ambayo yanasababisha  vyanzo hivyo kuzalisha umeme kwa ufanisi.