Dk Biteko: Viongozi tatueni kero za wananchi, msiishie kuzisikiliza

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiwasha taa baada ya kuzindua umeme katika Kijiji cha Magodi wilayani Mkinga mkoani Tanga

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Biteko amewataka viongozi wa umma kutatua kero za wananchi na badala yake kukaa kuwasubiri viongozi wa kitaifa wanapofanya ziara katika maeneo yao.

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameeleza Serikali inakusudia kuona viongozi wote wanatatua kero za wananchi, huku akieleza kusikitishwa na baadhi wanaoshindwa kutekeleza wajibu huo.

Dk Biteko amesema hayo leo, Januari 25, 2024 alipozungumza na wananchi katika Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga, baada ya kuwasha umeme katika vijiji hivyo uliosambazwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Katika ziara yake kwenye vijiji hivyo, aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

“Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika kila sekta na mabilioni ya fedha yamekuwa yakipelekwa kila mkoa kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi.

“Nikitoa mfano hapa Tanga, Serikali imeshaleta Sh2 trilioni na Sh600 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwenye umeme miradi inaongezeka, kwani mmepata Sh133.6 bilioni.

“Wilaya ya Mkinga imepata Sh8 bilioni kwa ajili ya usambazaji umeme, Dk Samia anapambana ili kuwaletea maisha bora Watanzania. Viongozi wengine tusiishie kusikiliza kero tu, tuzitatue na kama kuna mahali tunahitaji watupe muda, tuwaambie kwa uwazi,” amesema Dk Biteko.

Kuhusu usambazaji umeme vijijini, amepongeza REA kwa kuendelea kusambaza umeme vijijini akitolea mfano usambazaji umeme vijijini mkoani  Tanga umefanyika kwa asilimia 91 na Wilaya ya Mkinga yenye vijiji 85 tayari vijiji 82 vimesambaziwa umeme huku vijiji vilivyobaki kazi iikiendelea.

Kuhusu hali ya umeme nchini, amesema Serikali inaendelea kufanya kila jitihada kuboresha hali hiyo kwa kuhakikisha kuwa mitambo ya umeme inafanyiwa maboresho na miradi mipya inaanzishwa na kutekelezwa kikiwemo kituo cha umeme cha New Pangani (MW 68) alichosema kinatarajiwa kuzalisha umeme baada ya siku mbili.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula ameishukuru Serikali kwa kutekeleza kwa ubora miradi ya umeme vijijini wilayani humo na kuwafanya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi.

Pia ameiomba Serikali kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo mengine yaliyosalia kama vile kwenye vitongoji, ili wananchi katika maeneo hayo pia wapate huduma ya umeme.

Katika hatua nyigine, Dk Biteko amewataka wazazi na walezi nchini kupeleka shule watoto wote wanaopaswa kuwa huleni katika kipindi hiki ambacho shule zimefunguliwa.