Chadema waanza kujipanga uchaguzi Serikali za mitaa Moshi

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kimewaomba wananchi wa Moshi kujiandaa kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu 2024

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kimesema kimejipanga kuhakikisha kinashinda mitaa yote katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, ili kuweza kuwa sauti ya wananchi na kushughulikia changamoto ambazo zinaikabili Manispaa hiyo.

Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi, Januari 4, 2024 na Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Moshi.

Amesema tayari chama hicho kimeandaa wagombea makini na wenye uchungu na maendeleo ya Moshi.

Mboya amesema wenyeviti wa mitaa ndiyo msingi wa maendeleo katika manispaa hiyo, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha wanachagua viongozi watakaoweka mbele masilahi ya maendeleo ya wananchi na manispaa hiyo.

"Mwaka huu ni uchaguzi wa Serikali za mitaa na sisi tumesema hatuwezi kuwa kama wenzetu kwa maana ya kwenda kutafuta wagombea, sisi tayari tumewaandaa viongozi, tunasubiri muda na wakati ufike ili waje wagombee," amesema Mboya.

"Kipindi hiki tumeweka watu ambao watakuwa na nia ya kweli. Niwaombe wananchi wote wa Moshi kila mmoja haijalishi umeumizwa kiasi gani na uchaguzi uliopita wa 2019 na Uchaguzi mkuu 2020 na ukasema hapana sitashiriki tena uchaguzi, utakuwa umefanya kosa kubwa sana," amesema.

Mwekahazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kilimanjaro, Sharifa Mallya amesema wamejipanga kikamilifu na endapo uchaguzi utakuwa huru na haki, watashinda mitaa yote ya Manispaa ya Moshi.

"Kama uchaguzi utakuwa huru na haki, Chadema tutabeba mitaa yote Manispaa ya Moshi, tunachohitaji atakayeshinda atangazwe na kusiwepo na mtu kupita bila kupungwa.

“Niombe wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa kwani ndiyo watu wao wa karibu," amesema Sharifa.

Manispaa ya Moshi yenye mitaa 60, yote inashikiliwa na Chama cha Mapinduzi(CCM).