Wanaotumia vyandarua ndivyo sivyo kushughulikiwa

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya na Diwani Kata ya Isanga ,Dourmohamed Issa akizungumza na walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Azimio mchepuo wa kiingereza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua bure  vilivyokuwa vikitolewa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa niaba ya Serikali. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba, 20,2023; na Mstahiki Meya wa jiji hilo, Dourmohamed Issa mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua bure kwa wanafunzi wa shule za Msingi 105 za jiji hilo, kati ya hizo Shule 22 zikiwa za watu binafsi.

Mbeya. Serikali jijini Mbeya inaweza ikaanza kuwashughulikia watu ambao wanakaidi mipango ya matumizi bora ya vyandarua vinavyotolea na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa Malaria, huku wao wakivitumia kwa mambo mengine.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba, 20,2023 na Mstahiki Meya wa jiji hilo, Dourmohamed Issa mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua bure kwa wanafunzi wa shule za Msingi 105 za jiji hilo, kati ya hizo shule 22 zikiwa za watu binafsi.

Vyandarua hivyo ambavyo vimetolewa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ni kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa hatari wa malaria, hata hivyo, vimekuwa vikionekana kutumika tofauti na ilivyokusudiwa, huku wengine wakivizungushia kwenye  bustani za mboga mboga, au kwenye mabanda ya mifugo hususan bata na kuku.

“Serikali inatumia fedha nyingi kuagiza vyandarua kwa ajili ya kugawa kwa Watanzania kwa lengo la kuwakinga na maambukizi ya ugonjwa wa malaria unaotokana na kuumwana mbu, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia kuzungushia bustani za mboga mboga na mifugo kama bata na kuku,” amesema.

Issa amesema ufike wakati jamii kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa maralia na sio kuwa kikwazo cha kukwamisha juhudi hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya, Beno Malisa ambaye alikuwa mgeni rasmi amekazia kauli hiyo ya Mstahiki Meya, kwa kuwataka wanafunzi walionufaika na mpango huo kuwafichua wazazi ambao wanashindwa kuwalaza kwenye vyandarua vyenye dawa na badala yake kutumia ndivyo sivyo.

“Wanafunzi, Serikali imetoa vyandarua kwa lengo la kuendesha kampeni ya mapambano dhidi ya malaria, sasa ukiona mzazi anatumia kwa malengo ya kuhifadhia bustani za mboga mboga au mifugo, toeni taarifa kwa walimu ili hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema.

Malisa ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuona wanalinda afya za watoto kuanzia umri wa mwaka 0 hususan wale wa elimu ya awali mpaka wale wa darasa la sita, na kwamba inapotokea mzazi haoni umuhimu wa kuwakinga, hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa jiji hilo, Dk Yesaya Mwasubila amesema kuwa changamoto kubwa za ufinyu wa matumizi ya vyandarua ni baadhi ya wananchi kudai vinapunguza nguvu za kiume licha kutoa elimu ya mara kwa mara.

Ametaja changamoto nyingine na jamii kugeukia kutumia katika matumizi yasiyo sahihi ikiwepo kama uzio wa bustani za mboga mboga, na mifugo wakiwepo kuku na bata.

“Hii ni changamoto kubwa ambayo jamii licha ya kupatiwa elimu bado imekuwa ikiendeleza hivyo kuna kila sababu hatua kuanza kuchukuliwa ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya vita dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa maralia nchini,” amesema.

Mzazi, Joyce Mwakifwamba amesema kuwa Serikali inapaswa kutumia watendaji wa Serikali za mitaa kuanza ukaguzi na kuchukua hatua kwa jamii ambayo imegeuza vyandarua kwenye matumizi ambayo sio maelekezo ya Serikali ili iwe fundisho.

“Kwa Jiji la Mbeya hilo ni donda ndugu kuna maeneo wanafikia mahala vyandarua vinatumika kuvulia samaki kwenye mito na vipini vyake kutumika kama ndowano sasa Serikali itambue kuwa vinaletwa kama mitaji kwa baadhi ya jamii,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano na Mawasiliano, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) amesema mara  kampeni hiyo kwa Jiji la Mbeya inawafikia, wanafunzi 98,396 ambao watapata burevyandarua hivyo katika shule 105 na kwamba watatumia siku tatu kuzifikia shule zote.

Amewatahadharisha wananchi kutokubali kulaghaiwa kuwa vyandarua hivyo vinauzwa na badala yake watambue Serikali imetoa bure huku akihamasisha jamii hususan wazazi kutumia kuwafunika watoto kwa lengo la kuwakinga na malaria.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo imezindukiwa katika Wilaya ya Mbeya mjini na vijijini ambapo watatumia siku tatu, na kuendelea katika Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya ikiwa ni kutekeleza agizo la Serikali.