Bakwata kulinda rasilimali zake kidijitali

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh  Abubakar Zubeir 

Muktasari:

  • Ubadhirifu wa mali ndiyo uliolisababisha Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), kubadili mifumo ya uendeshaji wake kutoka analojia kwenda dijitali.

Dar es Salaam. Ili kudhibiti upotevu wa mali na mapato yake, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeanzisha mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kuratibu shughuli zake.

Kabla ya matumizi ya mifumo hiyo, Baraza hilo lilikabiliwa na changamoto lukuki katika urasimishaji wa rasilimali zake na wakati mwingine kushindwa kudhibiti ubadhilifu.

Hayo yalielezwa jana Ijumaa, Aprili 26, 2204 na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusu mabadiliko ya mifumo hiyo.

Amesema kupitia mifumo hiyo kwa sasa Bakwata itasajili kwenye programu yake tamizi inayoitwa Bakwata App rasilimali zake, fedha, misikiti, viongozi, miradi, walimu wa madrasa, madrasa na wachinjaji wote. "Bakwata kwa sasa tumeamua kuiwekea mifumo ya kidijitali na muda sio mrefu itaanza kutumia namba maalumu ya kukusanya mapato kwa kutumia mifumo yake ya kisasa," ameeleza.

Pamoja na mambo mengine, ameeleza msingi wa mabadiliko hayo ni kuhakikisha baraza hilo linatimiza madhumuni ya kuanzishwa kwake.

Amesisitiza linafanyika hilo, kwa kuwa baraza hilo lina mipango ya maendeleo na huduma kwa jamii kupitia miradi ya vituo vya afya, zahanati na mingine ya kiuchumi.

"Jambo linaloendelea ni kuwajengea uwezo viongozi wote wa Bakwata kuanzia misikiti hadi mikoa kwa kuwapa mafunzo ya uongozi, Tehama, ujasiriamali na maarifa mengine muhimu ya kuandaa mipango na ufuatiliaji," amesema.

Mufti huyo amesema hata mafunzo hayo, yatatolewa kwa njia ya kidijitali kupitia Bakwata online Academy.

Akizungumzia hayo, Imamu wa Msikiti wa Tunungua mkoani Morogoro, Said Ng’atsegwa amesema ndiyo mambo yaliyosababisha Mufti huyo atunukiwe shahada ya udaktari wa heshima, kutoka Chuo Kikuu Huria cha Gambia.

"Amekuwa na maono makubwa yanayofanya Bakwata tuende kuwa na udhibiti thabiti wa mali zetu. Shahada aliyotunukiwa ni halali yake mwenye macho na akili haambiwi tazama," amesema.

Pamoja na hayo, amesema Mufti huyo ameanzisha tuzo za kitaaluma zinazotolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo mbalimbali, hasa hesabu na sayansi bila kubagua dini.

"Mwaka jana alitoa tuzo kwa kijana wa kidato cha sita wa Marian boys kwa jina John Wilbald aliyeongoza kitaifa katika masomo ya fizikia, kemia na hisabati, kwa Kiswahili sahihi tahsusi ya PCM," amesema.