Waumini, Bakwata wavutana umiliki wa msikiti

Baadhi ya wananchi wakipita mbele ya Msikiti wa Masjid Noor uliopo mtaa wa Uhuru jijini Mwanza. Msikiti huo uko kwenye mvutano wa umiliki kati ya Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza na bodi ya udhamini ya Masjid Noor. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Waumini hao kupitia bodi ya udhamini ya msikiti huo (The Registered Trustee of Masjid Noor) walipinga uamuzi huo Septemba 2, 2023 baada ya Bakwata ikiongozwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke na wasaidizi wake kufika msikitini hapo kuswali na kutangaza kumuweka imamu, Mussa Rajabu kuusimamia.

Mwanza. Waumini wa Msikiti wa Masjid Noor maarufu msikiti wa Uhuru wamepinga uamuzi wa Baraza la Kiislam Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza kudai wenyewe ndio wamiliki na kuteua msimamizi wa msikti huo.

Waumini hao kupitia bodi ya udhamini ya msikiti huo (The Registered Trustee of Masjid Noor) walipinga uamuzi huo Septemba 2, 2023 baada ya Bakwata ikiongozwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke na wasaidizi wake kufika msikitini hapo kuswali na kutangaza kumuweka imamu, Mussa Rajabu kuusimamia.

Katibu wa msikiti huo uliopo kitalu Q namba 26 mtaa wa Uhuru Kata ya Mbugani wilayani Nyamagana, Mbaraka Mohammed amesema bodi ya msikiti huo imesikia fununu za Bakatwa kuuchukua msikiti huo kwa muda mrefu.

Kutokana na fununu hizo waliamua kuchukua tahadhari kwa kuvijulisha vyombo vya dola na Mahakama ya ardhi ambayo iliwapa oda ya zuio ili kuthibitisha mmiliki halali wa eneo hilo.

Mohammed amesema kwamba msikiti huo umekuwa chini ya uongozi wa Masijd Noor na kamati zake tangu mwaka 2010 umesajiliwa akidai Bakwata haitakiwi kujiingiza katika uendeshaji wa shughuli zinazofanyika hapo kwani wao ndiyo wanaumiliki.

Amesisitiza kuwa hawatouachia msikiti huo mpaka hapo vyombo vya sharia vitakapotoa haki baada ya kuskiliza ushahidi wa pande zote mbili.

“Leo (Jumamosi) kumetokea vurugu ambazo zimesababishwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ambaye amekuja hapa na kundi lake akitaka kuchukua msikiti huu wa Masijd Noor ambao upo chini ya usajili wa bodi ya wadhamini wa Masijd Noor amekuja akidai msikiti huu ni mali ya Bakwata.

“Tumewaambia kwamba jambo hili lipo mahakamani hatuwezi kugombana lakini wakawa wanaendelea kuleta fujo wakati tunaswali wakataka kuweka viongozi wao tukashindwa kukubaliana na jambo hilo,” amesema Mohammed

Akizungumzia madai hayo na mvutano huo leo Septemba 3, 2023, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema msikiti huo ni mali halali ya Bakwata kwa mujibu wa nyaraka walizonazo kwani wanaumiliki tangu mwaka 1970 baada ya kuachiawa na iliyokuwa jumuiya ya kiislamu ya Afrika Mashariki (East African Muslim Society).

Amesema msimamo wao uko pale pale wataendelea kuusimamia na utakuwa chini ya Imamu Mussa Rajabu.

Amefafanua kuwa viongozi wa Bakwata walifika kwenye msikiti huo jana Septemba 2, 2023 kuswali kwa nia njema na kuwajulisha kwamba msikiti ule ni mali yake kisha kumpendekeza Mussa Rajabu kuwa imamu wa msikiti huo.

Kabeke ametoa onyo kwamba kuanzia sasa hawatakaa kinyonge kulalamika kwenye mali ambazo wanazimiliki kihalali na hawako tayari kupoteza hata kipande cha ardhi wanayoimiliki na kuisimamia.

“Bakwata Mkoa wa Mwanza hatukukurupuka kwenda pale ifahamike wazi msikiti ule ni mali ya Bakwata tangu miaka ya 1970 na hakuna sababu ya kutumia nguvu kubwa jambo lililopo tunapishana tu kwamba nani aongoze pale.

“Wanaodai ni msikiti wao mwaka 2010 walijisajili kwa jina la The Registered Trustee of Masjid Noor wakajiita viongozi wa msikiti huo na kuuchukua, kwahiyo walikwenda kwenye msikiti wa Bakwata wakajisajili kwa kutumia mali yetu na kukubaliwa na mamlaka huu ni uonevu,”amesema

Nakuongeza,“Maamuzi na msimamo wetu unabakia hivyo kwamba msikiti ni wetu kwa nyaraka na umiliki na tumeamua utakuwa msikiti wa wilaya ya Nyamagana, wito wangu kwa mamlaka zinazofanya usajili ziwe makini wajiridhishe na hizi bodi wanazozisajili ili wasije kusababisha machafuko na kuvuruga amani,”

Muumini wa msikiti huo, Salma Rajabu amesema busara zitumike kusuluhisha mgogoro huo ili waumini waendelee kufanya ibada kwa amani kama ilivyokuwa awali kabla Bakwata hawajasema ni mali yao.