Kauli ya RC Dendego yaibua mjadala

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kitaraka iliyopo Halmashauri ya Itigi  baada ya kukagua ujenzi wa nyumba ya mwalimu. Picha ya mtandao

Muktasari:

 Jukwaa la Elimu kwa Mtoto wa Kike limekosoa kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego kuwa wasichana watakaopata mimba katika umri mdogo, watakuwa washitakiwa wa kwanza katika mashauri yatakayofunguliwa

Dar es Salaam. Kufuatia kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego kuwa wasichana watakaopata mimba katika umri mdogo, watakuwa washitakiwa wa kwanza katika mashauri yatakayofunguliwa, baadhi ya wanaharakati wamemkosoa wakisema kauli hiyo haileti suluhisho la tatizo hilo.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani humo na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitaraka Aprili 21, 2024, RC Dendego alisema ataanza kuwashughulikia wasichana wenye mimba kabla ya kuwatafuta wavulana waliohusika.

“Nikikuta msichana umepata mimba wewe utakuwa mshtakiwa namba moja na wewe ndio utakayeenda jela bila huruma na tumbo lako utajifungulia huko huko,” amenukuliwa akisema Dendego kupitia tovuti ya Mkoa wa Singida.

Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Elimu kwa Mtoto wa Kike jana Aprili 24, 2024 imesema kauli ya Dendego imewahukumu wasichana bila kutatua chanzo cha tatizo.

Wanaharakati hao wamesema kwa kutambua umuhimu wa elimu, wamekuwa wakishirikiana na Serikali kuboresha mifumo ya elimu, ili kurahisisha upatikanaji wa elimu sawa kwa wote kama ilivyoanishwa kwenye ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

“Sisi mashirika yanayounda Jukwaa la Elimu kwa Mtoto wa kike, tumesikitishwa na kauli iliyotolewa na Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Singida.

“Kauli ya Dendego, inasahau chanzo cha mimba za utotoni katika jamii yetu na kuwahukumu wasichana kama ndio chanzo na suluhu pekee ya kumaliza tatizo la mimba za utotoni. Inarudisha nyuma jitihada zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau wa elimu katika kuhakikisha tunaondoa vikwazo na kila mtoto anapata fursa ya kupata haki ya elimu,” wamesema wanaharakati hao.

Wametaja Sheria ya Elimu Kifungu cha 60 (3) (Sura ya 353 R.E 2019) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inayofafanua mazingira na adhabu atakayopewa mtu pale ambapo mwanafunzi amepata ujauzito.

Kifungu hicho kinasema: “Mtu yeyote ambaye amempa mimba mwanafunzi shule ya msingi au sekondari amefanya kosa atawajibika kwa kifungo cha kwenda jela muda wa miaka thelathini.”

Pia, wametaja Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 katika kifungu chake cha 130 (1) (e) inayosema kuwa, mwanamume atakuwa amebaka pale atakapofanya tendo la ngono na binti wa umri chini ya miaka 18.

“Sheria hizi zote zinatoa ulinzi kamili kwa msichana wa miaka chini ya 18 na pia kwa mwanafunzi yeyote wa kike bila kujali umri, dhidi ya vitendo vya kingono, ili kumfanya afurahie haki yake ya kielimu.

“Kumkamata binti aliyepata ujauzito ni kuendelea kumkandamiza yeye kama binti na pia yeye kama mhanga wa vitendo vya ubakaji alivyofanyiwa,” wamesema.

Wamerejea pia Waraka wa Elimu Na. 2 uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) Novemba, 2021 Serikali unaoruhusu wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito kurejea shuleni katika mfumo rasmi.

“Serikali pia ilitoa mwongozo mnamo Februari, 2022 unaotaka wanafunzi kurejea shule ndani ya miaka miwili baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi.”

 Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Elimumsingi (BEMIS) za miaka 2022 na 2023, wakisema wasichana 5,197 wamesharejea shuleni kama utekelezaji wa mwongozo huo.

“Hivyo, kwa uwepo wa mwongozo huu kuna maanisha Serikali iko tayari kusaidia upatikanaji wa haki na usawa kwa watoto wote, ikiwemo wasichana waliokatiza masomo kutokana na mimba za utotoni.”

Wametaja pia uamuzi wa Kamati ya Wataalamu ya Haki na Ustawi wa mtoto katika shauri namba (ACERWC) 0012/Com/001/2019, uliotolewa baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na CRR kufungua kesi kwa niaba ya wasichana.

“Kupitia shauri hilo kamati ilitoa mapendekezo kwa Serikali ya Tanzania ya kuhakikisha inafanyia uchunguzi kesi za watoto wa kike waliowekwa gerezani kwa sababu ya mimba na kuhakikisha wanaaachiwa haraka.

“Pia, Serikali ilitakiwa kuacha mara moja kuwaweka ndani na kuwakamata wasichana wanaopata ujauzito kwani ni uvunjifu mkubwa wa haki zao za msingi.”

Wameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) kwa kushirkiana na wizara za kisekta kutoa ufafanuzi na maelekezo kwa watendaji kuhusu utoaji wa taarifa sahihi kuhusu utekelezaji na msimamo wa Serikali kikanda na kimataifa kwenye suala la wasichana wenye ujauzito kurudi shule.