Mimba zinavyokatisha ndoto za wanafunzi

Muktasari:

Kila kukicha kumekuwa na kesi nyingi za watoto wa kike kuachishwa masomo kutokana na mimba au ndoa za utotoni, hali hii imekuwa changamoto kubwa kwa Taifa na jamii

Rorya. Walipojiunga na elimu ya sekondari mwaka 2012, wanafunzi 2,419 wa shule 31 za sekondari wilayani Rorya kila mmoja alikuwa na ndoto yake.

Miongoni mwao wapo waliokuwa na ndoto ya kuwa madaktari, walimu, marubani, wauguzi, waandishi wa habari, wanasheria, mahakimu na kila aina ya taaluma ambayo mtu anaweza kuifikiria.Lakini ndoto hizo kwa wanafunzi 369 zimeyeyuka wakati kundi hilo la mwaka 2012 lilipofanya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka jana.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Rorya, Ruge Sange, ni wanafunzi 2,050 kati ya 2,419 waliojiunga na elimu ya sekondari wilayani humo mwaka 2012 ndiyo walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.

Wavulana 228 na wasichana 141 hawakufanya mtihani wa mwisho kutokana na sababu mbalimbali.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na kupata ujauzito, utoro unaochagizwa na kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali kwenye sekta ya uvuvi, kilimo, ufugaji na biashara (kusafirisha abiria kwa kutumia bodaboda).

Zipo sababu kadhaa zinazoaminika kuchangia idadi hii ya wanafunzi kutohitimu elimu ya sekondari licha ya juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wengi wanapata elimu hiyo kwa kujenga shule za sekondari kila kata.

Kwa mujibu wa wadau wa elimu wilayani Rorya akiwamo Mkuu wa wilaya hiyo, Simon Chacha, umbali kutoka nyumba kwenda na kurudi shule, kukosekana kwa mabweni kwenye shule za sekondari za kata, mwamko mdogo wa elimu na umaskini wa kipato kwa wakazi wa wilaya hiyo ni miongoni mwa sababu kuu za wanafunzi wengi kukatisha masomo.

Zaidi ya wanafunzi 100 wapata ujauzito 2014/2015

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, katika shule zinazozunguka mji mdogo wa Shirati, zaidi ya wanafunzi wa kike 100 waliacha masomo baada ya kupata ujauzito katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Takwimu zilizopatikana kutoka kwa uongozi wa shule nne za sekondari wilayani humo zinaonyesha kuwa wastani wa wanafunzi wanne kutoka shule 31 za sekondari wilayani Rorya hupata ujauzito kila mwaka.

Shule zilizohusika katika utafiti huo ni ya Profesa Philemon Sarungi, Katuru, Tai na Raranya ambako kati ya Januari, mwaka jana hadi Julai mwaka huu, kila shule imepoteza watoto wa kike kati ya watano hadi saba kwa kupata ujauzito au kuwapa ujauzito wenzao.

Mwalimu wa taaluma katika Shule ya Sekondari Profesa Philemon Sarungi, Hoja Zubina anasema mwaka jana shule yake ilipoteza wanafunzi wanne waliokatisha masomo kutokana na ujauzito, wakati hadi kufikia Julai mwaka huu, wanafunzi watatu walifukuzwa shule baada ya kubainika kuwa ni wajawazito.

Mwalimu mlezi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Katuru, Gerald Ochola anasema wanafunzi saba; watatu mwaka jana na wanne mwaka huu, wamekatisha masomo baada ya kupata ujauzito.

Kati ya hao, wapo wanafunzi wawili wa kidato cha nne, mmoja msichana na mwingine mvulana ambao wamesimamishwa masomo kusubiri uamuzi wa bodi ya shule baada ya kubainika kuwa na uhusiano wa kimapenzi na hatimaye kupeana ujauzito.

Tofauti na wenzao waliokosa fursa ya kufanya mitihani, wanafunzi hao kwa mujibu wa Mwalimu Ochola, wataruhusiwa kufanya mitihani ya mwisho mwaka huu kwa sababu tayari wamesajiliwa kufanya mitihani.

Katika Shule ya Sekondari Tai, kwa mujibu wa mwalimu wa taaluma shuleni hapo, Mawala Hamisi, wanafunzi wanne wamegundulika kuwa wajawazito na kufukuzwa shule.

Hali ni mbaya zaidi katika Shule ya Sekondari Raranya ambako mwaka huu pekee, wanafunzi saba tayari wamegundilika kuwa ni wajawazito na suala lao kuachwa mikononi mwa vikao vya bodi kwa uamuzi.

“Mwaka jana tumepoteza wanafunzi watano kutokana na tatizo la ujauzito na hivyo kufanya shule yetu kupoteza wanafunzi 12 kwa sababu ya mimba kwa kipindi cha miaka miwili pekee,” anasema kwa masikitiko Mwalimu Alex Lucas.

Shule kukosa mabweni na wanafunzi kuishi ‘geto’

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Chacha, shule nne pekee za sekondari za Nyanduga, Tai, Bukama na Kisumwa, kati shule 31 zilizoko wilayani humo ndizo zenye mabweni, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanafunzi wa kike wanaotoka maeneo ya mbali.

Hali hiyo huwalazimu wanafunzi wanaotoka mbali na maeneo ya shule aidha kutembea umbali mrefu au kupanda baiskeli kwa wale wenye uwezo, kwenda na kutoka shuleni kila siku.

Baadhi ya wanafunzi hao wamepanga vyumba mitaani karibu na maeneo ya shule maarufu kama ‘geto’ ambako wanaishi bila usimamizi wa wazazi, walezi wala walimu.

Bahati Andolo, mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Raranya ni miongoni mwa waathirika wa kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka shuleni.

Anasema bila ya kuwa na mapenzi ya kupata elimu na juhudi za wazazi wake ambao wamemnunulia baiskeli, angekuwa ameacha masomo kutokana na kulazimika kutembea umbali wa kilomita 22 kila siku kwenda na kurudi shule.

Bahati anatoka Kijiji cha Buchire kilichopo mwambao wa Ziwa Victoria na hulazimika kuamka saa 10:30 alfajiri kila siku kujiandaa kabla ya kuondoka nyumbani saa 11:00 alfajiri kuwahi kushika namba inayohesabiwa saa 1:00 asubuhi ili kuepuka adhabu ya uchelewaji.

“Yupo rafiki yangu tuliyemaliza naye darasa la saba mwaka jana na wote tukachaguliwa kujiunga na Raranya sekondari, anaitwa Meshack Wambela tayari ameacha shule baada ya kushindwa kuvumilia adha ya kutembea kilomita 22 kila siku kwenda na kurudi nyumbani,” anasema Bahati.

Akizungumzia maisha ya ‘geto’, Mwanafunzi Mussa Ndiege anayesoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Katuru anasema baadhi ya wanafunzi huzigeuza ‘geto’ zao kuwa fursa ya kufanya ngono na wanafunzi wenzao au vijana wanaoishi jirani.

“Vishawishi, tamaa, umaskini wa kipato na shinikizo la rika ni kati ya sababu zinazosababisha wanaoishi ‘geto’ kujihusisha na ngono miongoni mwao au na vijana wanaoishi jirani na maeneo yao,” anasema Mussa na kuongeza:

“Kule ‘geto’ kila mtu yuko huru kufanya lolote. Hakuna uangalizi, siyo wa wazazi, walezi, walimu wala wamiliki wa nyumba.”

Itaendelea kesho