‘Housigeli’ afanyiwa ukatili, mwajiri wake mbaroni

Baadhi ya majeraha ya Melesiana Nestory (16) anayedai kufanyiwa ukatili na mwajiri wake wa kazi za ndani

Muktasari:

  • Kulingana na kifungu 4(1) cha sheria ya mtoto sura ya 13 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2019, mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18 anahesabiwa kama ni mtoto na anastahili kulindwa dhidi ya ukatli wa aina yoyote.

Moshi. Ni simulizi inayoweza kukutoa machozi ya mtoto Melesiana Nestory (16) anayedai kufanyiwa ukatili na mtu anayedai ni mwajiri, akidai amekuwa akimpiga na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kulingana na kifungu 4(1) cha sheria ya mtoto sura ya 13 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2019, mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18 anahesabiwa kama ni mtoto na anastahili kulindwa dhidi ya ukatli wa aina yoyote.

Lakini si kwa Melesiana , mzaliwa wa Nyakanazi wilayani Biharamulo anayedai kupitia mateso makubwa kutoka kwa mwajiri wake anayeishi eneo la Njiapanda ya Himo Wilaya ya Moshi.

Mwananchi Digital baada ya kupata taarifa, imefika hadi kwenye nyumba anakofanyia kazi binti huyo na kujionea mazingira anayoishi huku mwenyewe akisimulia jinsi anavyoteswa na vipigo kutoka kwa mwajiri huyo ambaye ni mwanamke.

 Waandishi wa habari hizo wameshuhudia majeraha mbalimbali mwilini.

Mwonekano wa mwili wa binti huyo ni dhoofu na una majeraha makubwa maeneo ya mgongoni, makalio, mapaja na maeneo ya usoni. Sikio moja analodai alipigwa kofi na mwajiri wake huyo, limevimba na kufunga.

“Nateseka, natamani nirudi nyumbani lakini naogopa kuwaambia hata majirani wasije kumwambia akanipiga tena,” amesimulia binti huyo huku akibubujikwa machozi.

Hata hivyo, baada ya simulizi hiyo, gazeti hili lilimtafuta mwanamke anayetuhumiwa kufanya vitendo hivyo kwa kumpigia simu, lakini iliita bila majibu.

Baadaye siku hiyo hiyo juzi Machi 5, 2024, Jeshi la Polisi nalo lilipata taarifa za tukio hilo na askari wake wakafika nyumbani kwa mtuhumiwa kufanya mahojiano na binti huyo na baadaye lilimpeleka hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kumhoji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alikiri kulifahamu na alisema, "tunaendelea kulifuatilia, tutawapa ripoti baada ya kupata uhalisia wa jambo lilivyo.

Hata hivyo, baadaye jana, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Kituo cha Polisi Himo, Sajent Consesa Ndolingo, aliiambia Mwananchi Digital kuwa tayari wanamshikilia mshukiwa huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.

"Huyu mwajiri (mtuhumiwa) tuko naye hapa Kituo cha Polisi Himo, tunamhoji tutatoa taarifa baadaye,” alisema Ndolinga.


Kagera hadi Himo

Melesiana anasema baada ya kuhitimu darasa la saba mwaka 2022 katika Shule ya Msingi Kasato, wilayani Biharamulo mkoani Kagera, alifaulu lakini hakuweza kuendelea na masomo kwa kuwa familia yake haikuwa na uwezo kumsomesha.

Akisimulia jinsi alivyofika kwa mwajiri huyo, Melesiana alisema baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari aliamua kutafuta kazi.

Matokeo ya mtihani wake katika shule ya msingi Kasato, Wilaya ya Biharamulo, yanaonyesha alifaulu kwa alama B katika somo la Kiswahili, Kiingereza D, maarifa C, hisabati C, sayansi C, uraia C akiwa na wastani wa alama C zilizowapeleka wenzake wengi sekondari.

"Baba na mama wote ni wakulima hawana uwezo, nilipomaliza darasa la saba na kufaulu, nikashindwa kwenda shule nilikopangiwa,” alisema binti huyo.

Kwa mujibu wa Melesiana, baada ya kuona maisha ya kijijini yanazidi kuwa magumu, akaamua kutafuta kazi za ndani, ndipo bosi wa dada yake, ambaye naye anafanya kazi za ndani, alimtafutia kazi kwa mwajiri huyo.

"Nilikuja kwa huyu mama Agosti 13m 2023 baada ya kutafutiwa kazi na bosi wa dada yangu anayekaa Mwanga, Kilimanjaro. Nimekuja lakini kabla ya mwezi kuisha, tukaenda Morogoro na huyu mama na mwezi wa 12 tukarudi,” anasema Melesiana.

Katika siku 204 ambazo ameshafanya kazi kwa tajiri yake huyo, anadai amekuwa akiishi maisha ya shida na anatamani kurudi kwa wazazi wake Nyakanazi, lakini anashindwa kwa sababu hajui ataondokaje.

“Ananilipa Sh40,000 kwa masimango, nisaidieni nirudi nyumbani kwa wazazi wangu Nyakanazi,” alisema binti huyo kwa akibubujikwa machozi.

“Mimi napigwa sana makofi, hata kama kosa limefanywa na watoto wake napigwa mimi, ananifanyia hivyo bila huruma,” alisema.

Anadai kuna siku alimpiga akamuuza, alipoona hali inazidi kuwa mbaya, alimpeleka hospitali na akadanganya kwa daktari kuwa ameshambuliwa na mama wa kambo.


Majirani wanasemaje

Akizungumzia tukio hilo, mjumbe wa eneo hilo, Elly Mosha alisema hawakuwa na taarifa za tukio hilo, jana ndiyo walipatiwa taarifa baada ya yeye kupigiwa simu na Polisi akitakiwa kufika katika nyumba anayoishi mtoto huyo.

“Mimi ni jirani yangu, lakini sikuwahi kujua, nimepigiwa simu na Polisi nikitakiwa kwenda kwenye hiyo familia kuona ukatili aliofanyiwa mtoto huyo, nilipofika nikashuhudia mtoto ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake,” alidai.

“Nimekuta kaumizwa kwenye makalio, mgongoni, mapajani na sehemu za usoni. Kuna siku hapo nyuma alikuja huyu binti karibu na hapa kwangu anapojenga bosi wake, alikuwa na afya yake nzuri tu,” alisema Mosha.

“Ila leo nimeshangaa kumwona alivyoisha, afya yake imedhoofika, inaumiza sana, sheria ichukue mkondo wake. Mimi ni mwanamke nimezaa lakini sio kwa huu unyama ambao mtoto huyu anafanyiwa," alisema mjumbe huyo.

Mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alidai tangu binti huyo afike kwenye familia hiyo, amekuwa akinyanyaswa na kadiri siku zinavyokwenda amekuwa akidhoofika kiafya kutokana na ukatili huo.

"Huyu binti tulianza kutilia mashaka kama kuna changamoto anayoipata, mara leo utamuona kavimba uso hana furaha, tukimuuliza ana shida gani anadai anapigwa na bosi wake,” amesimulia jirani huyo akisisitiza kutotajwa jina lake.

Jirani huyo alidai juzi alizungumza nab inti huyo na akasema usiku halali kutokana na maumivu anayoyapata ya vidondo na sikio.

Jirani mwingine, alidai mtoto huyo hutengwa hata wakati wa chakula.

"Huyu binti anaweza kula makande wiki nzima lakini watoto wa huyu mama wanakula nyama na vyakula vizuri," alisema na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kuingilia kati suala hilo ili haki iweze kutendeka kwa mtoto huyo mdogo.