Kuna unyanyasaji wa kimyakimya kwa wanawake mahala pa kazi

Meneja Uhusiano kutoka Kampuni ya Barrick Gold, Georgia Mutagahywa

Dar es Salaam. Meneja Uhusiano kutoka Kampuni ya Barrick Gold, Georgia Mutagahywa amesema ili kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake kuna ya elimu kutolewa  kwa kizazi kinachokuja cha vijana wa kiume kuhakikisha wanatambua jinsi ya kike ni binadamu kama walivyo wao.

Mutagahywa ameyasema hayo leo Machi 8, 2023 katika hafla maalumu iliyoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) ijulikanayo kama The Citizen Rising Woman katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Amesema baadhi ya wanawake katika maeneo ya kazi wamekuwa wakikumbana na unyanyasaji wa kijinsia wa chinichini ambao ni ngumu kuuonyoshea kidole kwa kuwa hauonekani bayana  ila ni changamoto ambayo imekuwa ikiwasumbua kizazi cha sasa.

Amesema ili kuondokana na changamoto hiyo mbali na kutoa elimu kwa vijana wa kiume pia mwanamke mwenyewe anatakiwa kusimamia utu wake, huku akiamua nini cha kufanya kwa wakati gani.

Mkurugenzi wa CRDB, Abdulmajid Nsekela  ametoa wito kwa taasisi na kampuni mbalimbali nchini kutoishia katika kuwawezesha wanawake pekee bali pia iwape nafasi ili waweze kuonyesha uwezo wao.

Amesema katika kampuni na taasisi mbalimbali nchini zimekuwa zikifanya jitihada kubwa katika kuwawezesha wanawake na changamoto inakuja katika kuwapatia nafasi kuweza kuonyesha uwezo wao.

Amesema wanawake wakipewa nafasi kupitia elimu na vipaji walivyonavyo wanaweza kufanya mambo makubwa.
Alitolea mfano wa benki ya CRDB kuwa asilimia 44 ya wafanyakazi wake ni wanawake na wanafanya kazi nzuri.

"Hilo linawezekana kwa kuwa kuna mazingira mazuri yanayowezesha wao kuwepo na kufanya kazi. Tumekuwa pia mipango inayowawezesha kujitambua"anasema.

Pia amesema pamoja na kuwapa nafasi wanawake pia wamekuwa na programu maalum kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wenye uwezo wa kushika nafasi ya uongozi.

"Tuna programu za kuwasaidia wanawake wenye uwezo wa kuwa viongozi lakini wenyewe hawajui kama wanaweza kufanya hivyo, "
"Hata mpango wa miaka mitano wa CRDB kwa sasa unaongozwa na mwanamke ambaye pia amekuwa Mkurugenzi wa CRDB Congo nchi ambayo ni ngumu kuongoza,"anasema