DC Timbuka: Tunapanga namna nzuri ya kuwanusuru wananchi na mafuriko

Baadhi ya wananchi wakifuatilia matukio katika sherehe za Muungano.

Muktasari:

 Serikali imewata wananchi waendelee kuchukua tahadhari hasa wale wanaoishi katika maeneo hatarishi.

Siha. Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuathiri maeneo mengi nchini, Mkuu wa Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, Dk Christopher Timbuka amesema wanapanga namna nzuri ya kuwanusuru wananchi na hatari ya mafuriko.

Hata hivyo, amesema wakati Serikali ikiendelea na mipango na mikakati yake, amewomba wananchi nao waendelee kuchukua tahadhari hasa wale wanaoishi katika maeneo hatarishi waanze kuondoka.

Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Dk Christopher Timbuka akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano yalifanyika Kituo cha Mabasi Sanya juu.

Dk Timbuka amesema hayo leo Ijumaa Aprili 26, 2024 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika katika Kituo cha Mabasi Sanya Juu.

Amesema kutokana na hali ya hewa kuendelea kuwa tete, ameitisha kikao cha kupanga mkakati wa namna ya kunusuru waathirika wa mvua katika maeneo yaliyoathirika wilayani humo.

“Tumepata taarifa kuna  maeneo wilayani kwetu yameathirika na mvua, baada ya maadhimisho haya tutakuwa na kikao cha dharura tuone namna ya kwenda kuwanusuru wenzetu,” amesema Dk Timbuka.

Amesema Wilaya ya Siha ni miongoni mwa zilizoathirika na mvua hizo zinazoendelea kunyesha.

 “Naomba  nichukua nafasi hii kuwapa pole wale wote waliopata majanga ya mvua, tumeshapita maeneo mbalimbali kuona athari zilivyo, tumeshaanza kuchukua hatua ya kuwasaidia waathirika na hivi leo tuna kikao kingine muda si mrefu tuone tunafanya nini zaidi,”amesema Dk Timbuka.

Ametaja maeneo yaliyoathirika na mvua hizo mpaka sasa ni pamoja na vijiji vya Wiri, Magadini, Mlangoni, Makiwaru, Karansi na Naibili.

Amesema maeneo mengine ni ya Munge na Embukoi ambako miundombinu mbalimbali imeathiriwa na mvua hizo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema dhamira ya Serikali ni kuhahakisha inapunguza makali ya maumivu ya mvua hizo kwa wananchi kwa kuwasaidia mahitaji muhimu.

Akizungumzia madhira ya ukatili wa kijinsia mkuu huyo wa wilaya ameitaka jamii kuendelea kupinga ukatili huo kwa kutoa taarifa za wabakaji, walawiti na wale wanaowasafirisha watoto kwa lengo la kwenda kutumikishwa kwa kazi mbalimbali hususan za ndani.

“Leo natumia hadhara hii kuendelea kukemea kwa nguvu zote wale wote wanaoshiriki vitendo hivyo viovu, nawasihi mbadilike, la sivyo mkono wa sheria utawafikia, tunataka jamii inayostawi ikiwa na utu na inayoishi kwa amani na utulivu kama Muungano wetu unavyotusisitiza,” amesema Dk Timbuka.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mark Masue akizungumza kwa niaba ya Mkurungenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo, Hajj Mnasi amesema Muungano umeleta manufaa makubwa ikiwamo amani ndani ya nchi hali inayochangia maendeleo kuonekana kwa kiwango kikubwa.

“Nchi isiyo na amani, kamwe huwezi kuona ikiendelea, sana sana itaishia kwenye vita na vurugu kila mahali,” amesema Masue.

Diwani wa Livishi, Luku Nkini amesema Watanzania hawana budi kuuenzi Muungano kwa sababu hata vitabu vitakatifu vya Kiislamu na Kikirsto vinahimiza mshikamano, ushirikiano na kupendana.

“Viongozi wetu waliouasisi huu Muungano waliyaona haya yote kuwa yana afya kwa Taifa, na kweli hata sisi tunaona, kwa hiyo tuulinde, hata ukiangalia mataifa makubwa duniani nayo yanapenda Muungano na yanaendeleza Muungano,” amesema diwani huyo.