Mvua yasababisha barabara nne kufungwa Dar

Muktasari:

  • Mvua imesababisha mazingira magumu ya usafiri na usafirishaji katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara mkoani Dar es Salaam.

Maeneo ambayo barabara zimefungwa ni Jangwani, Mkwajuni, Africana, na ya kutokea Kibada kuelekea Kisarawe 2, ambako daraja limevunjika na kukata mawasiliano.

Kwa mujibu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, kufungwa kwa barabara hizo kumesababishwa na wingi wa maji yanayopita juu yake.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 23, 2024 na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, William Mkonda alipozungumza na Mwananchi Digital.

Amesema eneo la Jangwani, walilazimika kulifunga tangu jana Aprili 22 hadi leo, baada ya ujazo wa maji kuongezeka hivyo kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo.

Mwonekano wa Barabara ya Morogoro, eneo la Jangwani likiwa limefurika maji. Picha na Michael Matemanga

“Kwa sababu barabara hii ina watumiaji wengi, wanafunzi na waendesha vyombo vya moto tumelazimika kuifunga  kwa ajili ya usalama wao, maana ujazo wa maji ni mkubwa,” ameeleza.

Katika eneo la Mkwajuni, amesema sababu za kufungwa ni wingi wa maji yanayopita juu ya barabara katika bonde hilo, hivyo kutishia usalama wa watumiaji.

Eneo lingine lililofungwa kwa mujibu wa Mkonda ni Africana karibu na Nyaishozi ambako maji mengi yanapita juu ya barabara hiyo.

Kigamboni nako si kwema, baada ya mawasiliano ya barabara kutoka Kibada kwenda Kisarawe 2 kukatika, kutokana na kuvunjika kwa daraja.

“Hapa daraja limekatika kwa hiyo hakuna mawasiliano ya kutoka eneo moja kwenda lingine. Wananchi wanalazimika kupita njia ya kuzungukia Mjimwema ndiyo wafike Kigamboni au Kisarawe 2,” ameeleza.

Kamanda ameeleza njia ya Vetenari kupitia Mwembeyanga nayo si salama sana kwa kuwa ina mashimo mengi, hivyo kutokana na mvua ni vigumu kujua kina cha shimo kutokana na maji kujaa.

“Tunaendelea kuwasihi watumiaji hasa wa vyombo vya moto waongeze umakini, lakini wasipime maji kwa kuyaangalia ni vema kama hawana shughuli ya lazima kwenda maeneo ya mbali wasalie nyumbani au watafute huduma katika maeneo ya jirani,” amesema.