Bodaboda 750 kupigwa msasa Tanga

Muktasari:

  • Zaidi ya madereva 750 wa pikipiki (bodaboda) katika Mikoa ya Tanga na Dodoma wanatarajiwa kupatiwa elimu ya usalama barabarani na matumizi ya alama za barabarani ili kupunguza ajali zinazotokea kila kukicha.

Tanga. Zaidi ya madereva 750 wa pikipiki (bodaboda) katika Mikoa ya Tanga na Dodoma wanatarajiwa kupatiwa elimu ya usalama barabarani na matumizi ya alama za barabarani ili kupunguza ajali zinazotokea kila kukicha.

Mafunzo hayo yanatolewa na Taasisi wa Amend Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Uswisi ambapo imebainika baadhi ya madereva hufanya makosa kutokana na kutokuwa na uelewa wa sheria, kanuni na miongozo ya nchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya usalama wa barabara kwa madereva wa bodaboda wa Kata ya Magaoni jijini Tanga, Ofisa Miradi Mwandamizi Mratibu  wa Taasisi ya Amend, Ramadhani Nyaza amesema mpaka sasa wamewafikia madereva bodaboda 180.

"Mradi huu ambao unafadhiliwa na ubalozi wa Uswizi una lengo la kuwafikia vijana 750 wanaofanya shughuli za usafirishaji kwa kutumia bodaboda katika mikoa ya Tanga na Dodoma"amesema Nyanza.

Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mabawa jijini humo, Athumani Babu amesema mradi huo wa elimu utapunguza changamoto ya ajali za barabara kwenye maeneo mbalimbali Jiji la Tanga ambapo amesisitiza mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa.

Hata hivyo madereva wa bodaboda waliopatiwa mafunzo wamesema watakuwa mabalozi wazuri wa kuendeleleza elimu hiyo Kwa wenzao Ili kupunguza changamoto ya uwepo wa ajali za barabara.

"Tunakwenda kuacha kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia shughuli zetu za bodaboda lakini na kuwashawishi wenzetu wengine kuachana na tabia za kujichukulia sheria mkononi lakini na kufuata sheria za usalama barabara "amesem Nasib Issa ambaye ni dereva bodaboda.