Wahitimu Udom wageuka bodaboda

Dodoma. Vijana 40 waliomaliza masomo yao katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameshindwa kurejea makwao baaada ya kujiajiri kwenye udereva wa bodaboda chuoni hapo.

Miongoni mwao, saba bado ni wanafunzi wanaoendelea na masomo katika kozi mbalimbali na wametaja sababu kuu ya kufanya biashara hiyo ni kukabiliana na tatizo la ajira na ugumu wa maisha.

Wakizungumza na Mwananchi chuoni hapo, madereva hao walitaja sababu kubwa ya kuanzisha biashara hiyo ni ukosefu wa ajira na maisha magumu mtaani lakini chuoni hapo wamebaini kuna fursa ya kupata fedha.

Alberto Chrisent ambaye ni miongoni mwao, alisema maisha ya udereva pikipiki chuoni hapo alianza hata kabla ya kumaliza masomo yake hadi sasa alipomaliza kwani kazi hiyo ni nzuri na inamuingizia kipato tofauti na kukaa bure.

Chrisent ambaye alimaliza Shahada katika mambo ya utalii, alisema kuwa alianza kuendesha bodaboda tangu akiwa mwaka wa pili mwaka 2021 japo hakuwa rasmi kutokana na kutojisajili kwenye chama cha madereva wa bodaboda chuoni hapo.

Kwa mujibu w Chrisent, kwenye masomo yake alipata mkopo wa asilimia 100 hivyo alikuwa anajitafutia fedha za ziada siku ambazo hakuwa na vipindi au siku za mwishoni mwa juma walipokuwa wanapumzika.

“Pikipiki hii ni ya kwangu niliinunua kwa ajili ya kutembelea ingawa nilikuwa naifanya bodaboda pale nilipokuwa sina hela ya matumizi japo kwa kuibia kwa kuwa nilikuwa sijasajiliwa,” alisema Chrisent.

Kwa mujibu wa dereva huyo, hakuwa peke yake wakati anajiunga bali alikuwa na wenzake wawili ambao kwa sasa wamepata ajira na kuachana na kazi hiyo hivyo na yeye akifanikiwa kupata kazi ataachana na udereva bodaboda.

Alitaja kipato anachoweza kupata kwa siku ni Sh100,000 kama biashara ni nzuri kutokana na chuo hicho kuwa na shughuli nyingi zinazowakutanisha watu wengi kwa wakati mmoja.

Kwa upande wake, Adrick Zawayo ambaye anasoma chuoni hapo mwaka wa tatu, alisema kazi ya bodaboda inamsaidia kutatua mahitaji ya kila siku kutokana na kupanda kwa gharama za maisha hivyo anashindwa kuomba fedha nyumbani.

Awayo alisema amekuwa akitumia muda wa ziada baada ya kutoka kwenye vipindi au siku za mwisho wa wiki ambapo mara nyingi huwa hawaingii madarasani.

“Kuna wakati natoka kwenye kipindi saa 2:00 asubuhi na kipindi kinachofuata huwa ni saa 9:00 alasiri, huo muda wa kusubiri kipindi huwa nautumia kufanya kazi ya bodaboda na muda wa kipindi ukifika naingia darasani.” alisema Zawayo.

Alisema kazi hiyo haiathiri masomo yake kwa kuwa anajua kilichompeleka chuoni na hajawahi kukosa hata kipindi kimoja.

Mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda Udom Daniel Mujuni alisema chama hicho kina wanachama 260 ambapo kati yao wapo 40 walisoma hapo ama wanaendelea na masomo yao kwenye fani mbalimbali lakini wamejiunga ili kutafuta riziki.

Mujuni alisema Udom ni chuo kikubwa ambacho chenye watu wengi ambao wanahitaji huduma ya usafiri kutoka wanakoishi na kwenye madarasa yao na pengine wanapohitaji kwenda mjini kutafuta mahitaji yao.

Alisema wanachama wake wamerahisisha huduma ya usafiri chuoni ikiwemo wageni wanaokwenda kupata huduma kwani wanajua maeneo mengi ambayo bodaboda wengine hawayajui.

Mwenyekiti huyo alisema wanafunzi waliosoma chuo hicho wamekuwa msaada hata kuzuia waharifu kwa kuwa wanazifahamu njia nyingi ukilinganisha na madereva waliotoka nje ya hapo.