Adaiwa kumuua mkewe baada ya kugoma kurudiana

Mshtakiwa Baraka Shija anayedaiwa kumuua mke wake kwa kumpiga na chuma kichwani baada ya mwanamke huyo kukataa wasirudiane, akiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Geita. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

  • Baraka Shija anashtakiwa kwa kosa la kumuua kwa maksudi Grace Daudi Kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, tukio analodaiwa kulitenda Juni 23, 2022.

Geita. Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomkabili Baraka Shija, ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alimuua mkewe, Grace Daudi kwa kumpiga na chuma kichwani, baada ya kukataa wasirudiane naye.

Kwa mujibu na shahidi huyo Sajini Pascal ambaye ni askari wa upelelezi wa Wilaya ya Geita, baada ya kufanya mauaji hayo, mshtakiwa alienda kwa mganga wa kienyeji na kujificha ndani ya nyumba yake kabla ya kukamatwa na wananchi.

Kachero huyo wa Polisi aliyerekodi maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ameeleza hayo leo Aprili 17, 2024 wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, mbele ya Jaji Mfawidhi, Kelvin Mhina anayeisikiliza kesi hiyo.

Baraka Shija anashtakiwa kwa kosa la kumuua kwa maksudi Grace Daudi Kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, tukio analodaiwa kulitenda Juni 23, 2022.

Pamoja na ushahidi huo, Sajini Pascal amewasilisha mahakamani hapo maelezo ya onyo ya mshtakiwa yaliyopokelewa mahakamani kama kielelezo namba moja cha ushahidi kwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo.

Akisoma maelezo hayo, shahidi huyo alisema mshtakiwa alioana na Grace mwaka 2022 na litakiwa kulipa mahari ya Sh1 milioni, lakini baba yake alilipa Sh100, 000.

Baada ya baba yake kulipa kiasi hicho cha fedha na kubakiza Sh900,000 za mahari, aliruhusiwa kuondoka na mkewe na kwenda kuishi naye hadi mgogoro baina yao ulipoibuka.

Wakiwa pamoja, walipanga nyumba eneo la Nyaseke na kuishi kwa miezi mitatu, kisha wakarudi nyumbani kwa baba yake (mtuhumiwa) huko Butobela Wilaya ya Geita.

Mwanzoni mwa Juni 2022 akiwa nyumbani, mke wake alitoka shambani akiwa na mzigo wa mihogo na kuuweka chini, kisha akambeba mtoto wake ambaye alimza kabla ya kuolewa, na kuondoka bila kuaga anakokwenda.

Baada ya muda kupita, mshtakiwa aliamua kwenda nyumbani kwa wazazi wa mkewe na kumkuta, alimuuliza mbona ameondoka bila kuaga, ndipo mkewe alidai amechoka kuishi naye na hawezi kurudi tena.

“Nilimmeleza mama mkwe, lakini Grace alikataa kumsikiliza nikaenda kwa baba mkwe, maana wanaishi tofauti ili atusuluhishe lakini sikupata majibu, nikarudi kwao kumbembeleza akakataa,” anaeleza katika maelezo hayo.

“Siku moja alirudi nyumbani na kuchukua nguo zake nikamuomba sana abaki lakini alikataa, nikaendelea kwenda kwao kuomba arudi bila mafanikio,” alisimulia mshtakiwa katika maelezo hayo ya onyo ambayo sasa ni kielelezo cha mahakama.

Baadaye Juni 23, 2022 alipanga kwenda kumuomba mkewe arudi nyumbani kwa mara ya mwisho na wakati anaenda alibeba chuma alichokificha na alipofika nyumbani kwao, alimuomba tena mkewe arudi nyumbani bila mafanikio.

Akiwa hapo nyumbani mwanamke huyo alimuaga mumewe anaenda shambani kuchuma mboga na mshtakiwa baada ya muda alimfuata.

Akiwa njiani, walikutana na mkewe na alipomuona mwanamke alikimbia na mshtakiwa alimkimbiza akampiga chuma kichwani na kudondoka. Kisha akampiga tena na akautelekeza mwili na kile chuma alichotumia kumpiga nacho kisha akaondoka.

“Nilienda Bugalama huko Shinyanga kwa mganga wa kienyeji nikajificha ndani ya nyumba yake, ndipo wananchi wa Nyang’omango walifika na kunikamata,” alinukuliwa mshtakiwa huyo kwenye maelezo yake.

Baada ya ushahidi huo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 18, 2024 kwa ajili ya upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi wake.

Mshtakiwa anatetewa na Wakili Batholomeo Musyangi huku upande wa Jamhuri ukiwa na mawakili wawili ambao ni Godgrey Odupay akisaidiana na Kabula Benjamin kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS).