Ni mauaji ya kutisha

Muktasari:

  • Watu wanne wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia ndani ya nyumba yao katika Kitongoji cha Kibumbe wilayani Rungwe, huku miili ikiwa imeharibika.

Mume, mke, watoto wakutwa wameuawa

Mbeya. Watu wanne wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia ndani ya nyumba yao katika Kitongoji cha Kibumbe wilayani Rungwe, huku miili ikiwa imeharibika.

Watu hao ambao ni mume Simon Mtambo (41), mke wa Fortunata George (38) na watoto wawili, Oscar Mtambo (14) na Florence Mtambo (9) wanadaiwa wamepoteza uhai ndani ya wiki moja na kwamba chanzo cha kifo chao bado hakijafahamika.

Akizungumza baada ya kufika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk Vincent Anney, alisema tukio hilo ni moja kati ya mfululizo wa matukio ya mauaji na kujiua yanayotokea wilayani humo.

“Inasikitisha sana kifo cha baba, mama na watoto, tumeruhusu miili yao izikwe kwa sababu imeharibika. Nawaomba wananchi mnapokuwa na mgogoro hakikisheni mnatoa taarifa kwa mamlaka husika ili tuushughulikie,” alisema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, katika wiki moja kati ya watu wanne hadi watano wanaripotiwa kuuawa au kujiua katika wilaya hiyo.

Hali hiyo, alisema imeilazimu Serikali kuona haja ya kufanya utafiti wa kujua sababu za kutokea kwa matukio hayo.

Alionya tabia za baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi wakiwaua wengine kwa dhana kuwa ni washirikina na kuwa Serikali itachukua hatua dhidi yao.

Diwani wa Kata ya Kiwira, Michael Mwamwembe alisema taarifa ya tukio hilo aliipata baada ya kupigiwa simu na polisi na alipofika katika nyumba hiyo alikuta miili imeharibika.

“Kwa wiki hii hili ni tukio la pili. Kuna mwanamke alimuuwa mumewe katika Kitongoji cha Mpandapanda na kisha kumfukia nje ya nyuma yake, sababu ni migogoro ya wivu wa mapenzi,” alisema.

Mfululizo wa matukio ya mauaji ya mapenzi, alisema yanaonyesha haja ya kutungwa sheria ndogo itakayoruhusu wanandoa kutengana iwapo watakuwa na migogoro, ili kunusuru uhai wao.


Ilivyogundulika

Ukimya wa wiki moja ndio uliomfanya mmoja wa ndugu kufunga safari kutoka Mbeya hadi nyumbani hapo, alisema mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina litajwe.

Alisimulia kuwa nyumbani hapo alikuta milango imefungwa, huku kukiwa na harufu kali, hali ambayo ilisababisha kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi.

Baada ya milango ya nyumba hiyo kuvunjwa, ndipo walikuta miili hiyo ya watu wanne.

“Tulipoingia ndani tulikuta hali hiyo, chini kulikuwa na panga na nyundo pamoja na paketi ya kuhifadhia dawa ya kuulia wadudu wa mbogamboga,” alisema.

Mkazi wa Kiwira, Ally Mwakipesile aliwataka wazee wa kimila kuingilia kati matukio hayo, akisema wanapaswa kukemea ili kuinusuru nguvu kazi.

Mwanamume alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Mbuja na mke mwalimu wa Shule ya Msingi Ikuti wakati mtoto mmoja alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Busokelo na mwingine shule ya msingi Ikuti.

Ajinyonga kwa madai ya kuzidiwa na madeni

Iringa. Msiba wa Mkazi wa Kihesa, Kilolo, Enea Mkimbo (55) aliyefariki dunia baada ya kujinyonga kwa madai ya kuzongwa na madeni ya Vicoba, unafanyika katika maeneo mawili tofauti kutokana na mvutano ulioibuka.

Baada ya kikao kilichofanyika nyumbani kwa marehemu, ndugu wa upande wa kike wametenga msiba wao wakidai mtoto wao hakulipiwa mahali.

Hata hivyo, mume wa marehemu, Edward Sanga alisema licha ya kutuma posa mara mbili, wakwe zake waligoma kuipokea na hivyo akaendelea kuishi naye.

Sakata la Vicoba

Habari zinasema juzi wanakikundi wenzake walienda nyumbani kwake kudai madeni na ilipofika jioni akamuaga mumewe, Edward Sanga kuwa anaenda nyumbani kwa mama yake mzazi, badala yake aliingia jikoni na kujitundika hadi kufa.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Allan Bukumbi alithibitisha tukio hilo na kwamba, wanaendelea na upelelezi kuhusu madai ya Enea kujiua.

“Tukio limetokea na ni kweli marehemu alikuwa anadaiwa madeni ya Vicoba na wenzake, tunaendelea na upelelezi tutatoa taarifa kamili,” alisema Bukumbi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kihesa Kilolo B, Michael Mlalwe alisema alipigiwa simu kuhusu tukio la Enea kujinyonga saa 12 asubuhi na yeye akatoa taarifa polisi.

“Inasemekana ni madeni ya vicoba na jana wenzake walikuja kumdai lakini hatujui zaidi. Changamoto tunayohangaika nayo sasa ni eneo la msiba, wananchi wa Kihesa Kilolo na mume wanataka msiba uje nyumbani kwa marehemu na upande wa kike wametenga msiba huko,” alisema Mlalwe.

Mume wa marehemu, Sanga alisema “naomba mke wangu aletwe nyumbani, hiki kibanda tulijenga wote yeye anasomba maji mimi najenga, aje nimuage. Hapa ni nyumbani kwangu na ni mke wangu.”

“Nilituma washenga mara mbili walikataa kupokea posa, tuna watoto na wajukuu, nitalilia hapa,” aliongeza.

Kaka wa marehemu, Aldo Chonya alisema mama mzazi wa marehemu amegiza kuwa msiba uwekwe nyumbani kwake na yeye ataondoka kwenda kulia sehemu nyingine.

Kuhusu vikoba, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema jana walishuhudia Enea alipokuwa akidaiwa deni hilo.

Mmoja wa wananchi hao ambaye aliomba jina lake lisiandikwe, alisema kama wenzake wangemdai fedha hizo kwa ustaarabu asingepata msongo wa mawazo na kuamua kujiua kwa sababu ya madeni.

“Atakuwa hakuwa na pesa na akawaza namna wanavyokuja kumdai hizo pesa kwa maneno makali akaamua kujiua,” alisema Kilipo.

‘Panya Road’ waua mwanafunzi Dar

Dar es Salaam. Wiki moja baada ya vikundi vya uhalifu maarufu Panya Road kuibuka tena jijini Dar es Salaam na kuvamia nyumba 24 za wapangaji mtaa wa Kabaga Kinyerezi, kisha kuwajeruhi na kupora mali zao, juzi wamevamia tena na kusababisha kifo cha mwannafunzi.

Matukio ya watu kuvamiwa na kuporwa vitu mbalimbali, hasa nyakati za usiku katika jiji la Dar es Salaam, yamekuwa yakijirudia mara kwa mara licha ya Jeshi la Polisi kutangaza kuwasaka wanaojihusisha na uhalifu huo.

Septemba 6, mwaka huu, saa 8 usiku katika maeneo ya Kibaga Kinyerezi watu wanne walijeruhiwa na kulazwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana wakiuguza majeraha waliyoyapata.

Akizungumza na Mwananchi jana, shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni jirani Benitto Edward alisema usiku wa kuamkia jana, kundi la vijana zaidi ya 20 wakiwa na mapanga, visu, bisibisi na marungu walivamia nyumba hiyo iliyopo Kawe Maringo.

Alisema baada ya kuvamia nyumba hiyo mali ya Pascal Basso, walianza kuvunja mlango wa mmoja baada ya mwingine wakiamrisha kupatiwa vitu mbalimbali kama vile simu, fedha na kompyuta mpakato (laptop).

“Kwenye purukushani hizo watu wanne walijeruhiwa katika jitihada za kutaka kujiokoa, lakini kwa bahati mbaya mtoto wa mwenye nyumba Maria Basso (24) ambaye alikuwa wanafunzi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,alifariki akiwa anakimbizwa hospitali,”alisema

“Kama mnavyojua kwenye matukio kama haya sio rahisi mtu kutoa fedha au simu kirahisi, kwahiyo kila aliyebisha alipigwa au kuchomwa bisibisi ili mradi tu wapate vitu walivyokuwa wanavihitaji,” alisema Edward.

Kaimu Amid wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Kamfipo Gidion, alithibitisha kumpoteza mwanafunzi huyo.

Dk Gidion alibainisha kuwa Maria alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili akichukua stashahada ya uandishi wa habari.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Wiliam Mkonda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Septemba 14, mwaka huu saa nane usiku eneo la Kawe Mzimuni ambapo kikundi cha wahalifu zaidi ya10 wakiwa na silaha za jadi, walivamia nyumba ya Paschal Basu (56).

Alisema baada ya kuvamia nyumba hiyo yenye vyumba 15, walivunja milango na kupora fedha, simu za mkononi, kujeruhi watu watatu na kumuua Maria Paschal (24).

“Tukio walilofanya wahalifu hawa ni jambo baya na linalotakiwa kulaaniwa na kukemewa na Mtanzania yoyote anayechukia uhalifu kwa watu kama hawa ambao hawataki kutumia njia halali za kujitafutia kipato,”alisema Kamanda Mkonda

Kamanda Mkonda, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kukabiliana na uhalifu wa aina tofauti unaofanyika katika maeneo yao.