Wafahamu watano waliofariki katika nyambizi ya kitalii Titan

Nyambizi ndogo ya kitalii iliyojulikana kama Titani, ikiwa katika matayarisho kabla ya kuzama na kupotea

Muktasari:

  • Kikosi cha Marekani na kile cha Canada, wamejaribu kuitafuta manowari hiyo bila mafanikio, hata hivyo jana wamefanikiwa kupata sehemu ya mabaki ya nje ya chombo jicho kilichokuwa kimebeba watu watano ambao ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa OceanGate Stockton Rush (61), wafanyabiashara Hamish Harding (58) pamoja Shahzada Dawood (48) ambaye aliambatana na mtoto wake Suleman (19).

Marekani. Waokoaji wamekuwa wakimbizana na muda kuitafuta nyambizi ndogo ya kitalii Titan, iliyopotea siku ya Jumapili karibu na kisiwa cha Newfoundland, Canada katika bahari ya Atlantiki.

Chombo hicho kilizama ili kuyafikia mabaki ya meli ya Titanic, iliyo umbali wa mita 3,800 katika sakafu ya bahari.

Kuzamia hadi katika mabaki hayo kwenda na kurudi inachukua jumla la masaa nane. Lakini timu nyambizi ya Titan inayomilikiwa na kampuni ya OceanGate, ilipoteza mawasiliano na meli ya MV Polar Prince, saa moja na dakika 45 baada ya kuzamia baharini, kwa mujibu wa vikosi vya ulinzi wa baharini vya Marekani.

Kikosi cha Marekani na kile cha Canada, wamejaribu kuitafuta manowari hiyo bila mafanikio, hata hivyo jana wamefanikiwa kupata sehemu ya mabaki ya nje ya chombo jicho kilichokuwa kimebeba watu watano ambao ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa OceanGate Stockton Rush (61), wafanyabiashara Hamish Harding (58) pamoja Shahzada Dawood (48) ambaye aliambatana na mtoto wake Suleman (19).

OceanGate hutoza dola za kimarekani 250,000 kwa mtu mmoja kwa safari ya siku nane kuondokea Canada kwenda kutalii mabaki ya Titanic.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Mwananchi Digital inakuletea utambulisho wa watano hao.

Hamish Harding

Kwenda kuyaona mabaki ya Titanic kunahitaji mambo mawili, pesa nyingi na moyo wa kusafiri. Bilionea wa Uingereza, Hamish Harding 58 ana yote mawili hayo.

Harding alikuwa katika nyambizi hiyo siku ya Jumapili, kampuni yake ya Action Aviation na mtoto wake wa kambo, Brian Szasz alisema kupitia mtandao wa kijamii katika ujumbe ambao baadaye ulifutwa.

Msafiri wa angani na mtalii, ambaye anaishi Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwanzilishi wa Action Group na Mwenyekiti wa Action Aviation, kampuni ya uuzaji na utoaji wa huduma za usafiri wa angani yenye makao yake Dubai.

Ni mhitimu wa fani ya Natural Sciences and Chemical Engineering kutoka chuo kikuu cha Cambridge. Harding ana shauku na mambo ya anga tangu akiwa kijana, ndio maana akawa rubani na mwanamichezo ya kuruka kutoka angani.

Mwaka 2022 alitajwa miongoni mwa mashujaa wa safari za angani, na mwanachama wa bodi ya kilabu ya wasafiri. Klabu maarufu ya kimataifa ya wavumbuzi na wanasayansi.

Harding ameshasafiri mara kadhaa kwenda bara la Antaktika, ambako alimsindikiza mwana anga wa zamani Buzz Aldrin mwaka 2016. Akiwa na miaka 86 Aldrin alikuwa mtu wa kwanza wa umri wake kufika ncha ya Kusini ya Dunia.

Mwaka Harding akishirikiana na kampuni ya kitalii ya White Dissert walizindua ndege ya kwanza binafsi itayokwenda katika bara hilo. Mapenzi yake kwa safari pia yalimpeleka anga za juu. Juni 2022 alikuwa katika msafara wa misheni ya Blue Origin ya kampuni ya Jeff Bezos.

Harding ana rekodi tatu za Guinness: Mwaka 2019 alisafiri kuzizunguka ncha za dunia kwa kasi kubwa zaidi. Mwaka 2021, pamoja na Mmarekani, Victor Vescovo, alivunja rekodi mbili ya masafa na ya muda, kwa kuzama umbali wa kina cha mita 11, 0000 katika shimo la baharini la Mariana katika bahari ya Pacific.

Prince Shahzada Dawood

Prince Dawood ni mwanaume kutoka familia ya kibiashara ya Kipakistani ambaye ni raia wa Uingereza, pia, ni mwanachama wa bodi ya Prince Trust - mfuko wa hisani wa Uingereza. Mtoto wake wa kiume, Suleiman pia alikuwa pamoja naye kwenye msafara huo.

Taarifa iliyotolewa na familia ya Dawood, “mtoto wetu Prince Dawood na mtoto wake, Suleiman walikwenda safari ya kuona mabaki ya Titanic katika bahari ya Atlantiki. Wakati huu, nyambizi yao ndogo imepoteza mawasiliano na hatuna taarifa za kutosha kwa sasa. Juhudi zinaendelea zikiongozwa na serikali kadha na mashirika ya uvumbuzi wa chini ya bahari, ili kupata mawasiliano na nyambizi yao na kuwarudisha nyumbani.”

Familia ya Dawood, ni moja ya familia tajiri nchini Pakistan. Pia shughuli zao zimejikita Uingereza. Prince Dawood, ni makamu mwenyekiti wa Engro Corporation. Kampuni ya mbolea, chakula na nishati.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Prince Dawood alizaliwa Pakistan kisha akahamia Uingereza. Huko alisoma sheria katika chuo kikuu cha Backingham. Baadaye alisoma shahada ya pili kuhusu soko la nguo ulimwenguni, katika chuo kikuu cha Philadelphia.

Prince Dawood, ni mdhamini wa taasisi ya SETI, kampuni ya tafiti za anga za juu. Prince Dawood anaishi Uingereza na mke wake, Christine na watoto wao Suleiman na Alina. Ni mpenzi wa picha na wanyama.

Ni makamu mwenyekiti wa Dawood Heracles Corporation, ambayo ni sehemu ya kampuni ya Dawood Group. Familia hii imedumu katika biashara kwa zaidi ya karne moja.

Prince Dawood alianza kuwa sehemu ya biashara ya familia kuanzia 1996. Dawood Heracles Corporation inaendesha na kusimamia viwanda mbali mbali.

Prince Dawood amekuwa kiungo muhimu katika maendeleo na ubunifu katika eneo la nishati, kilimo, chakula, nguo na usafishaji wa mafuta.

Suleman Dawood

Suleman Dawood, 19, mtoto wa bilionea Dawood mkazi wa Surbiton kusini mashariki mwa London. Ni mwanfunzi wa wa Chuo Kikuu cha Strathclyde na miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo.

Mapema wiki hii taarifa ya familia imemtaja Suleman kama "shabiki mkubwa wa fasihi ya hadithi za kisayansi na kujifunza mambo mapya", na kuwa na shauku katika michezo ya kufikirisha akili (Pazzle games) na aliyependa kucheza mpira wa wavu (volleyball).

Kijana Suleman ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Kimataifa ya ACS Cobham huko Surrey, alikuwa amemaliza mwaka wake wa kwanza katika Shule ya Biashara ya Strathclyde.

Mkuu wa chuo Kikuu na Naibu Chansela, Prof Sir Jim McDonald, aliwaandikia wanafunzi kuwafahamisha kuwa Suleman alikuwa kwenye nyambizi hiyo ndogo ya kitalii.

Katika ujumbe huo, alisema: "Ninawaandikia kwa moyo mzito kushiriki habari kwamba mmoja wa wanafunzi wetu, Suleman Dawood, ni abiria kwenye meli ya chini ya maji ambayo haipo katika Atlantiki ya Kaskazini.

"Najua utaungana nami katika kutuma salamu sala zetu kwa familia zao na wapendwa wao."

Stockton Rush

Stockton Rush ndiye mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa OceanGate Expeditions.

Wengine wawili ni Stockton Rush ana asili ya Marekani, ni Rais wa OceanGate, kampuni ya kukodisha na tafiti za kisayansi, na uvumbuzi katika vina virefu vya bahari.

Tangu kuundwa kwake 2009, kampuni hiyo imeweza kutengeneza vifaa vya kufika umbali wa mita 4,000 na 6,000 chini ya bahari.

Rush alianza kazi yake angani, akawa rubani mdogo zaidi duniani akiwa na miaka 19 mwaka 1981. Miaka mitatu baadaye, alijiunga na McDonnell Douglas Corporation kama injinia katika majaribio ya programu ya usafiri wa anga ya F.15. Uzoefu wake wa anga, na shauku ya bahari vilimfanya kuanzisha kampuni ya OceanGate 2019.

Mwaka 2012 alishiriki uanzishaji wa OceanGate Foundation, shirika lisilo la kibiashara linaloshughulika na kukuza maendeleo ya teknolojia za baharini, sayansi, historia na kiakiolojia. 1989 alitengeneza ndege ya majaribio ya Glasair III ambayo inafanya kazi hadi leo.

Paul-Henry Nargeolet

Nargeolet, mwenye umri wa miaka 77, anajulikana kama mtaalam wa Titanic, alikuwa mmoja wa abilia katika chombo cha Titan kutizama mabaki ya meli ya Titanic iliyozama 1912.

Mchoraji wa bahari na mpiga mbizi wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Ufaransa, aliyejipatia jina la ‘Bwana Titanic’ kwa sababu alishiriki katika msafara wa kwanza miaka miwili baada ya kugunduliwa kwa mabaki ya meli hiyo 1987, na ni mtu pekee duniani aliyetembelea eneo hilo la mabaki ya Titanic zaidi ya mtu mwingine yeyote.

Pia alikuwa wa kwanza kurudisha kifaa kwenye uso wa bahari - sahani ya fedha - na aliwahi kuwa mkurugenzi wa utafiti wa chini ya maji wa kampuni ya RMS Titanic ambayo inamiliki haki za ajali hiyo.

Katika mahojiano na mchapishaji Harper Collins, aliwahi kusema wakati alipoona kwa mara ya kwanza "sehemu nzuri zaidi ya ajali", upinde, uliojulikana na filamu ya James Cameron, "tuliweza kuona minyororo ya nanga, winchi zilizong'olewa na mashapo ndani ya maji. Kwa dakika 10 hakuna aliyepumua”.

Alimuoa mwandishi wa habari wa runinga wa Amerika Michele Marsh, ambaye alifariki 2017, ambaye walijuana kupitia matukio ya Titanic, wakati alipoitwa kwa mawasiliano ya mtu aliyenusurika katika janga hilo.

Alizaliwa Machi 2, 1946 huko Chamonixin katika Haute-Savoie ya Ufaransa, Nargeolet aliishi kwa miaka 13 huko Casablanca, Morocco kabla ya kuhamia Paris akiwa na umri wa miaka 16 kukamilisha masomo yake.

Mnamo 1964 alianza kazi yake katika Jeshi la Wanamaji la Ufaransa, ambapo alihudumu kama afisa aliyebobea katika uondoaji wa mgodi, kupiga mbizi na mzamiaji wa kina chini ya maji, hadi 1986. Alihamishwa katika miaka ya 80 hadi Kikundi cha Uzamiaji wa Chini ya Maji (GISMER), ambapo pia aliendesha baadhi ya nyambizi.

Alisafiri dunia nzima akipata ndege na helikopta za Ufaransa zilizozama na kugundua pia gari la Kirumi lililoanguka kwa kina cha mita 70.

Mnamo 1986 alichaguliwa na taasisi ya utafiti ya Ufaransa IFREMER kutazama utafiti wa chini ya maji juu ya Titanic. Wakati huo, alikuwa kamanda wa kikundi cha wapiga mbizi cha Jeshi la Wanamaji la Ufaransa, ambao dhamira yao ilikuwa kusafisha Mfereji wa Suez.

"Sikuwa na hamu tena na Titanic" alikuwa alieleza katika mahojiano na Le Parisien -. Nilikuwa nimeona au kusoma ripoti juu ya mada hiyo, lakini sikuwa na wazo kwamba ingechukua nafasi muhimu sana katika maisha yangu ".

Mnamo 1987, aliendesha msafara wa kwanza kwenye eneo la ajali pia akiendesha majaribio ya 1993, 1994 na 1996.

Kuanzia mwaka wa 1994, Nargeolet aliwahi kuwa mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Rasilimali za Majini na Chini ya Maji cha Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan (CMURM) na, kutoka 1996 hadi 2003, alifanya kazi na Aqua+, kampuni tanzu ya Canal+, ambayo alielekeza misheni ya chini ya maji ya manowari mbili.

Tangu 2007, Nargeolet amekuwa akifanya kazi kwa mkurugenzi wa RMS Titanicas wa mpango wa utafiti wa chini ya maji. Kazi yake imejumuisha kuendesha Magari Yanayoendeshwa kwa Mbali (ROVs) pamoja na majaribio ya kupiga mbizi kwenye maeneo ya ajali.

Kama sehemu ya utafiti, kazi yake imesababisha urejeshaji wa takriban vitu 5,500 katika kipindi cha mbizi 35. Kama mtaalamu wa Titanic, ameshiriki katika utayarishaji wa filamu mbili za Titanic: The Legend Lives On (1994) na Deep Inside the Titanic (1999), na kuchapisha kitabu, In the deeps of the Titanic (“In the Kina cha Titanic").

Wakati wa msafara wa OceanGate mnamo 2022, pia uligundua uwepo wa "mfumo wa mazingira wa kuzimu" kwenye muundo wa basalt ambao haukujulikana hapo awali karibu na Titanic.