Watalii watano wafariki ndani nyambizi ya Titan - OceanGate yasema

Waliofariki katika Nyambizi ya Titan

Muktasari:

  • Kampuni ya OceanGate ambao ni watengenezaji na waendeshaji wa Manowari ndogo ya kitalii ya Titan, imesema watu watano waliokuwa kwenye safari ya kutalii eneo la ajali ya meli ya Titanic, kwa kutumia chombo hicho chini ya maji, wamefariki dunia.

Marekani. Kampuni ya OceanGate ambao ni watengenezaji na waendeshaji wa Manowari ndogo ya kitalii ya Titan, imesema watu watano waliokuwa kwenye safari ya kutalii eneo la ajali ya meli ya Titanic, kwa kutumia chombo hicho chini ya maji, wamefariki dunia.

Wanaume hao watano walikufa katika kile walinzi wa Pwani wanaamini kuwa ni janga kubwa.

Watalii waliokuwa kwenye nyambizi hiyo ndogo ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa OceanGate Stockton Rush (61), wafanyabiashara Hamish Harding (58) pamoja Shahzada Dawood (48) ambaye aliambatana na mtoto wake Suleman (19).

Katika mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi, Admirali John Mauger wa Walinzi wa Pwani ya Marekani alisema kuwa mabaki hayo yanaaminika kuwa sawa na nyambizi ya Titan.

Haijulikani ni nini kilisababisha uharibifu wa Titan.

Kutoweka kwa nyambizi hiyo kulisababisha juhudi kubwa ya utafutaji wa kimataifa iliyohusisha vikosi vya Marekani, Kanada, Uingereza na Ufaransa.

Kwa mujibu wa mtandao wa BBC, katika taarifa yao, OceanGate imesema inathamini "kujitolea kwao kutafuta watalii hawa watano, mchana na usiku, kufanya kazi bila kuchoka kusaidia wafanyakazi wetu na familia zao".

Mabaki hayo yalipatikana na gari la utafutaji la chini ya maji linalodhibitiwa kwa mbali (ROV) takriban futi 1,600 (480m) kutoka kwenye mabaki ya Titanic.

Vipande vitano tofauti viligunduliwa ambavyo viliruhusu mamlaka kuthibitisha kuwa vilitoka kwa Titan, ikiwa ni pamoja na sehemu ya mkia.

Haijulikani ni lini hitilafu hiyo ilitokea au ni nini huenda kilisababisha.

Adm Mauger alisema hakuwa na jibu la iwapo miili ya watu hao watano waliokuwemo kwenye nyambizi inaweza kupatikana.

"Haya ni mazingira ya ajabu yasiyosameheka huko chini kwenye sakafu ya bahari," alisema.

ROV's zitasalia katika eneo hilo huku uchunguzi wa kilichotokea ukiendelea, Mauger aliongeza.

Wafanyakazi wengine - ikiwa ni pamoja na wataalam wa matibabu na mafundi - wataanza kuondoka.

Mapema wiki hii, mamlaka ilisema kwamba ndege za Canada ziligundua sauti za chini ya maji, ambazo baadhi ya wataalam walikisia kuwa huenda zilikuwa ishara kwamba abiria nyambizi hiyo walikuwa bado hai.

Walinzi wa Pwani sasa wanaamini kuwa hakukuwa na uhusiano kati ya kelele na eneo ambalo mabaki ya Titan yalipatikana kwenye sakafu ya bahari.

Walinzi wa Pwani wa Marekani wanasema mawazo yao yapo na familia na kuhakikisha wanaelewa vizuri kadiri wanavyoweza kuhusu kile kilichotokea na kuanza kukubali kilichotokea kwa wapendwa wao.

Kwa upande wa mchakato huo mkubwa, wataendelea kuchunguza eneo la bahari ambako mabaki yamepatikana.

Kuna maswali mengi kuhusu jinsi, kwa nini na wakati hii ilitokea.

Hayo ni maswali ambayo tutayakusanya sasa wakati serikali zikikutana na kujadili jinsi ya kufanya uchunguzi.

Ajali hiyo ilitokea umbali gani na mabaki ya meli Titanic?

Eneo la ajali hiyo mbaya linaaminika kuwa futi 1600 (487m) kutoka upinde wa ajali ya Titanic.

Iko katika eneo ambalo hakuna mabaki yoyote ya meli ya Titanic.

Maafisa walisema vipande vitano vikuu viligunduliwa katikati ya vifusi karibu na eneo la mkasa wa Titanic.

Miongoni mwao, sehemu ya 'pua' la nyambizi hiyo sehemu ya nje ya 'chemba ya presha' ya chombo na mabaki mengine

Titan, ambayo ilijengwa na kuendeshwa na OceanGate, ilitoweka Jumapili asubuhi muda mfupi baada ya kuanza safari ya kuelekea kwenye eneo la ajali ya meli ya Titanic takriban maili 435 kusini mwa St John's, Newfoundland.

Wanaume wote watano waliokuwa ndani ya meli hiyo wanaaminika kufariki dunia papo hapo baada ya meli hiyo kukabiliwa na shinikizo kubwa la maji na 'kulipuka'.

Waliouawa ni Mkurugenzi Mtendaji wa OceanGate, Stockton Rush, mkongwe wa Jeshi la Wanamaji wa Ufaransa Paul-Henri (PH) Nargeolet, bilionea wa Uingereza Hamish Harding, mfanyabiashara wa Pakistani Shahzada Dawood na mtoto wake Suleman, ambaye alikuwa na umri wa miaka 19 pekee.

Jana, timu ya Walinzi wa Pwani nchini Marekani ililipoti kuisha kwa akiba ya hewa ya oksijeni iliyomo kwenye chombo cha chini cha maji ‘monawari’ ambacho kilipotea siku ya Jumapili katika eneo ilipotokea ajali ya Titanic.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘Daily Mail’ walieleza kwamba taarifa kutoka kwa opereta wa chombo hicho, OceanGate Expeditions amesema monawari hiyo ilikuwa na uwezo wa kusambaza hewa ya oxygen kwa saa 96 pindi inapokutana na hali ya dharura na Tayari hizo zilikuwa zimeisha na kuzua hofu na wasiwasi kuhusu uhai wa watu watano ndani ya chombo hicho.

Hata hivyo, meli ya utafiti ya Ufaransa ya Atalante, iliyokuwa na chombo cha kuzamia cha roboti chenye uwezo wa kufikia kina kilipo ajali ya Titanic, takriban futi 12,500 (mita 3,810) chini ya uso, ilikuwa imewasili katika eneo la utafutaji.

Chombo hicho cha utafiti cha Atalante mara ya kwanza kilikuwa kikitumia sauti ya mwangwi kuweka ramani kwa usahihi sehemu ya chini ya bahari ili iweze kuwa rahisi kufikiwa kwa chombo hicho, taasisi ya utafiti ya baharini ya Ufaransa Ifremer imesema.