Ai... wai bitwini mai intavyuu yua pasing uraundi?

Khalid Mohammed. Top In Dar mwenye mamlaka na makuzi ya Kinondoni Studio. Ulimi wake una mkataba na lugha ya Malkia. Mcheshi mpaka ucheshi wenyewe unaushangaa ucheshi wake. ‘Komediani’ tumbo joto huko waliko.

Top In Dar anachekesha zaidi kuliko kuimba kwa sasa. Ameteka utawala wa Chid Benz kwenye himaya ya vipaza sauti vya online tv. Maiki zinamfuata kila kona alipo. Zinamhitaji zaidi yeye kuliko anavyozihitaji.

Zeze ndo ngoma yake iliyompa hukumu ya kuishi kimuziki zaidi. Akawa mkubwa kuanzia Mtaa wa Mkwepu mpaka Kibera Nairobere. Ni mnyama kweli anapopewa haki ya kucheza na jukwaa. Filamu ya Girl Friend ikaongezea uzito wa jina lake.

Unakumbuka vyema wakati huo Mnyama akitoka kisanii? Alikuwa juu kuliko mnara wa meli pale feri. Sikia kwa watu tu, pisi za mjini zilimtetemekea. Hii haikuwa kwenye

‘faivu stazi hoteli’ za Dar tu. Hii ilikuwa funika bovu Afrika Mashariki yote.
Kina Naziz walitamani sauti ya Mnyama isikike kwenye nyimbo zao. Na kina Jalong’o walitamani kufanya mahojiano naye. Hakuwa Top In Dar tu, bali alikuwa top top top. Waulize wale watu ambao walibahatika kuwepo nyakati za Bongo Fleva siyo Amapiano.

Siku moja nipo na wana mitaa ya kule Mikocheni. Njia ya Sayansi inayotokea Msasani kwa Mwalimu. Kushoto baada ya ‘Rozi Gadeni’, kulikuwa na baa inaitwa Lafiesta. Watu tulikula biere na kucheza pool pale kila siku ya Mungu.

Tulienda kwa mengi sana pale. Kwanza mademu wakali wakali sana walikuwa wananywea’ga’ pale. Pili mademu wakali walikuwa wanapita sana njia ile. Tatu mademu wakali walikuwa na ‘saluni’ karibu na ile baa. Nne kulikuwa na demu nyuma ya ile baa mkali balaa.

Hizi sababu nne zilitosha mabishoo wa kizazi kile, kutelekeza pesa za enzi za ‘Big Ben’ Mkapa. Pool na pombe kilikuwa kitu cha ziada, kwanza hata msosi wao haukuwa mkali kiviiile. Kifupi mademu ndio ulikuwa uchawi wa ile baa na sisi kama mazuzu tulihudhuria ‘dei tu dei’.

Siku moja ‘tumechili’ na raba zetu za Kwa Mkorea na Kwa Makoba Kariakoo. Mara paap, inapaki ‘Maki tuu baluni’. Enzi hizo ‘baluni’ sijui ni kama gari gani kwa sasa. Kila msela aliyepiga pesa ndefu alitaka ‘kupushi baluni’. Noma mzee baba enzi hizo wanahesabika wenye mikoko.

Mara anashuka bishoo wa Kinondoni. Top In Dar Mnyama yuko peku peku. Anafungua buti ya gari na kutoa raba na kuivaa. Akiwa bado kainama akifunga kamba. Anatokea mtoto Shamsa kutoka nyuma ya nyumba ile ile yenye baa na kumfuata TID. Majuto!

Anazama kwenye ndinga wanasepa. Siku hiyo ndipo nikajua kwamba wote tulikuwa tunaenda pale baa kumvizia Shemsa. Lile tukio lilikuwa la kikatili sana kwetu sote pale. Tulipigwa ganzi. Na ndo ukawa mwisho wetu kufika pale.
Wote tuliingia wivu kwa tukio lile. Hiyo ni miaka ya 2002, 2003 mpaka 2004 hapo.

Bongo Fleva iko juu kinomanoma. Na Top In Dar alikuwa mmoja wa wasanii supa kweli kweli. ‘Kupush’ ndinga nyakati zile haikuwa kitu kidogo aiseee. Ogopa!
Mtafute TID kwa sasa. Jamaa bado ana nguvu kubwa sana. Sijajua bado kama anajitafuta ama utajiri ndo unamtafuta? Kuna kitu kipo ndani yake Mnyama. Kitu ambacho kinahitaji akili kubwa zaidi ya hizi zilizopo ili kujua ni kitu gani. Top In Dar ana kitu kikubwa sana.

Maneno yake ‘yanatrendi’ sana kuliko ngoma za Diamond. Misemo yake ina nguvu kuliko ‘singo’ kibao za Alikiba. Kwanini? Mimi na wewe hatujui. Bila shaka tunahitaji akili iliyo juu ya uwezo wetu wa kufiriki kujua kilichopo ndani ya TID. Jamaa ni pesa ambayo bado ipo nyuma ya pazia.

‘Ni Yeye...’ huu ni msemo wake maarufu sana. Sijui aliwaza nini. Lakini huu ni msemo ambao ulitumiwa mpaka kwenye kampeni na watu wa Chadema. 2020 kwenye kampeni zao na Tundu Lissu, Chadema walipita na huu msemo kila kona ya nchi. Na kuna wakati alileta zogo la kutaka kulipwa.

‘Mtoto Mdogo...’ msemo huu pia ni zaidi ya singo ya msanii yeyote Bongo hii. Hii misemo ipo siku itageuka pesa kwake Mnyama. Hizi ni tungo tata zinazoweza kutumika kwa namna kama ‘kauli mbiu’. Kwa kampuni za biashara ama taasisi binafsi na za serikali.

Lakini hivi sasa hii misemo ya mtoto wa Kino. Inaishia kuwapa faraja tu watu bila kumpa pesa. Kitu chochote ambacho ‘kinatrendi’ kwa dunia ya sasa ni pesa. ‘Wai... Wai’ misemo ya TID asipate pesa? Kuna sehemu watajaa. Hizi ni faranga za wazi wazi kwa Mnyama.

Mzee Kigogo, halikuwa jina lake ni msemo wake. Ambao baadaye sasa ukageuka kuwa jina lake. ‘Levo’ zake za ‘trendingi’ za misemo yake siyo za nchi hii. Haiwezekani akitoa msemo flan hivi unatambaa sana, lazima ana kitu. Kitu gani? Ndo tunapokwama.

Hivi sasa anakimbiza na ‘Wai bitwini mai intavyuu yua pasingi araundi’. Kila kona watu wanautumia, kuanzia mitandaoni mpaka mitaani. Siyo masela, ‘masista duu’ na ‘majentromani’. Kama ni kitu cha kawaida mwambie kaka yako afanye kama yeye. Tuone!

Maisha na kipaji cha ovyo ni kulwa na doto.  Kipawa kikubwa sana lakini hakitumiki. Kwa sababu hakuna akili hiyo ya kutumia vipawa vya watu kuwa pesa. Mnyama ana kitu atafika mbali.