Nyoshi ana gharama balaa!

Muktasari:

  • Wiki hii Nyoshi Elsaadat kupitia bendi yake ya Bogoss Musica  ametrendi baada ya kutoa wimbo ‘Vimba’ ukiwa na video yake ambayo inafanya vizuri.

Jina la Nyoshi lilikuwa kubwa zaidi alipokuwa akiitumikia Bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ ‘Wazee wa Pamba’ jukwaani kabla ya kumiliki bendi yake mwenyewe inayoitwa Bogoss Musica ‘Nyumba ya Baba’. Tangu amekuwa katika bendi hizo Nyoshi hajawahi kufanya vibaya kwenye muziki wa dansi.

Wiki hii Nyoshi Elsaadat kupitia bendi yake ya Bogoss Musica  ametrendi baada ya kutoa wimbo ‘Vimba’ ukiwa na video yake ambayo inafanya vizuri.

Nyoshi pia ni mmoja wa wanamuziki Wacongo wanaoishi Tanzania kwa muda mrefu ambao pia toka ameingia hapa Tanzania hajawahi kurudi Kongo.

Mwananchi lilimfata hadi nyumbani kwake Kimara Stop Over na amefunguka mambo mengi ya muziki na maisha kijuma.

Nyoshi yuko nchini tangu mwaka 1992 na ameliambia Mwananchi kukaa kwake muda mrefu ni kwa sababu ya Watanzania, ni ni wenye upendo sana, hivyo akajiona kama yupo nyumbani kwao Congo.

“Mara ya kwanza naingia Tanzania ilikuwa 1992. Nilipapenda kutokana na upendo walionionesha Watanzania nikajiona kama nipo kwetu Congo. Pia muziki wangu ni sababu nyingine ya kuwa hapa na watoto pia ndio maana nimekuwa kama ndugu yao na ndomaana naendelea kuishi hapa.”

Aidha Nyoshi anasema “Kuna baadhi ya maneno yalikuwa yananichukiza, wakisema nimekimbia kwetu kwa sababu ya vita, mimi nimetoka Congo hakukuwa na vita. Haya maneno huwa yananikwaza sana.”

                       

Vipi muziki umemlipa?

Anasema muziki haujamlipa kwa upande wa pesa lakini umemfanya atambulike Afrika na kimataifa na kumpatia marafiki wengi ambao wana msaada mkubwa kwenye maisha yake.

“Labda niseme tu  mafanikio makubwa niliyoyapata kwenye muziki ni  kupata watoto wengi ambao wanasoma naamini watakuja kuwa watu wakubwa, hayo ndio mafanikio makubwa kwangu na kufahamiana na watu,” anasema Nyoshi.


Wanamuziki  kukimbia na kurudi kwake

Anasema wamekuwa wakiondoka wakidai masilahi ni madogo lakini wanarudi wakidai wamepashindwa huko walikokwenda.

“Tatizo la wanamuziki huwa haturidhiki. Tunauficha ukweli mfukoni tunaongea uongo. Wakitaka kuhamia bendi nyingine huwa wamajieleza sana ili waondoke. Mimi si wa kukulipa pesa ndogo halafu unaondoka unarudi. Wanamuziki wangu wengi wananifanyoia hivyo. Ningekuwa soiwalipi vizuri wasingerudi. Wakisema hivyo wasikilizeni tu, ni waongo,” alisema na kuongeza; “Hata uwanunulie nyumba, uwalipie kodi huwa hawaridhiki wataondoka tu. Ni wepesi kudanganywa kama watoto wadogo.”


Hataki kumzungumzia Patcho

Kumeibuka stori mitandaoni mwanamuziki  Patcho Mwamba ameongea na vyombo vya habari na kumzungumzia vibaya Nyoshi na kusababisha watu kujiuliza kama wana bifu na inaelezwa si mara moja amefanya hivyo na hana muda wa kumjibu.

“Mimi najielewa sana. Hivi ulishawahi sikia mimi katika mahojiano yangu nimemzungumzia huyo? sababu sitaki unafiki na hata kama kuna mtu ana ugomvi na mimi aseme.”

Anasema na kuongeza; “Naweza kuwataja watu wenye ubaya na mimi, roho mba, wanafki, lakini kwa nini niwataje wakati wana familia zao, mke na watoto wakisikia ina faida gani?”

“Kukaa kimya kwangu nakuheshimu. Nina mke na watoto, hivyo siwezi kuanza kusema vibaya au kutukana vibaya kwenye mahojiano. Nina uwezo wa kuongea mambo mabaya hapa ila tutachekwa sana. Yeye aendelee tu kunitukana ila sitanyanyua mdomo wangu kumjibu.”


Ajificha darini

Nyoshi anasema wanamuziki wa Congo wa bendi ya Stono Musica ‘Wajerajera’ ya Ndanda Kosovo walikamatwa na kuwekwa ndani kwa ajii ya utata wa vibali vyao vya kufanya kazi nchini na yeye akakimbilia juu ya dari.

“Hii siku siwezi kusahahu sababu wanamuziki wa Jelajela ya Ndanda Kosovo walikuwa wanaingia nyumbani kwangu hapo hapo wakakamatwa. Mimi nilikimbilia juu ya dari nikawa nawasikia tu chini wananitafuta. Waliona picha yangu kubwa ukutani wakasema huyu ndiye tulikuwa tunamtafuta. Hapo mke wangu marehemu Rukia Bruno alikuwa amesafiri kwenda Zanzibar.”


Gharama za mavazi, viatu

“Ukitazama hapa si unaona viatu vingi sana pamoja na nguo? Sasa hapa  kila kiatu kina nguo yake na vyote natumia pesa nyingi, kiatu cha pesa ndogo nanunua Sh50,000 au laki nane, lakini inategemea na brand ya kampuni vipo hadi vya laki mbili, kuna viatu vinatoka nje ya nchi natumia pesa za Euro na kila kiatu kina ngozi ya wanyama.kuna ngozi ya punda, nyoka, chui, simba, Mamba, pundamilia na ngozi zingine

“Napenda sana kuvaa ndio maana chumba hiki chote nimeweka nguo na viatu tu na napendelea kila ninachovaa kiendane na viatu, tunaweza kuchambua hapa na tusimalize leo,” anasema Nyoshi.


Ameanza kutumia mkorogo akiwa na miaka sita

Nyoshi anasema alianza kuchubua ngozi ya uso wake kwa mkorogo tangu akiwa na miaka sita, hivyo anawashangaa wanaomuona wa ajabu huku akidai kujichubua kwake ni kujipamba kama wanamuziki wengi wa Congo wafanyavyo.

“Sioni ajabu kupaka mkorogo, nimeanza tangu nikiwa darasa la sita hadi leo ni miaka mingi, pia napaka kwa kuwa ni mwanamuziki ninayejua kujipamba nashangaa wanaonishangaa, we huoni yangu ngozi imetulia na kuwa na mvuto kwa sababu natumia vipodozi vya gharama ambavyo mtu mwingine hawezi kumudu gharama hizo.

“Gharama zake ni kubwa, naweza kutumia Mkorogo wa laki tatu hadi tano kwa kuwa nachanganya vitu vingi na naweza kukosa vvote lakini mkorogo lazima uukute kwenye kabati langu la vipodozi,” anasema Nyoshi.

Nyoshi El Saadat anasema akiamua  kuwa mweupe sana inawezekana lakini anapunguza baadhi ya vipodozi vikali ili aweze kuzuia ngozi yake na huwa anaficha aina gani ya mkorogo anaoutumia kwa kuhofia kuigwa.


Watoto 14, bado anaongeza

“Mimi nina watoto 14,  ila kuna watoto  wengine wawili nimeambiwa ni watoto wangu, hapa nafanya uchunguzi ili nijue ukweli na kama wangu nawachukua na kuwahudumia mimi napenda sana watoto na bado nataka kuongeza zaidi ya hawa.”

Aidha Nyoshi anasema, hakuna hata mtoto wake mmoja ambaye amerithi kazi yake ya muziki, ila kuna mtoto wake Blandina alianza kuingia kwenye muziki lakini baadae amekuwa kimya hajui imekuwaje kama kaacha au vipi.


Simba lialia, hajui wachezaji

Hapa Nyoshi amepigaje? Anasema akiachana na muziki anapenda kufuatilia soka na ni shabiki wa Simba kwa Tanzania, kimataifa anaifuatilia Real Madrid. Ila katika wachezaji wa Simba hawajui zaidi ya Clotaus Chama kwa sababu ana rangi nyeusi na watu wanamzungumzia kila wakati.

Pia wachezaji wa Simba wanaotoka Congo amewajua hivi majuzi sababu akitoka kwenye mechi mapema wameumia, Fabrice Ngoma, Henock Inonga na kwasababu wanazungumziwa.

“Mimi bana mbali na muziki nafuatilia sana mpira na timu yangu ni  Simba kwa hapa Tanzania, ila siwjui wachezaji wake zaidi ya Chama kwa sababu rangi yake nyeusi.

“Kuna huyu Feisal Salum ‘Feitoto’ yuko timu gani namsikia tu naye, na kwa upande wa Yanga ninaowajua ni Joyce Lomalisa na Fiston Mayele (sasa hayuko Yanga) kwa kuwa wanazungumziwa sana.”