Hofu yatanda kuibuka wizi wa majumbani

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linaendelea kusimamia mifumo ya kiusalama kwa kushirikisha wananchi katika kuzuia uhalifu

Dar es Salaam. Hofu imetanda kwa wananchi wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na Pwani kutokana na ‘upepo’ wa wizi wa vitu vya majumbani, hasa runinga na redio.

Wizi huo unafanyika zaidi usiku, huku wanaokumbwa na matukio hayo wakieleza namna wanavyohisi wezi kuwapuliza dawa za usingizi.

“Nafikiri walinipulizia dawa, sababu sio kawaida yangu kulala fofofo, hakuna aliyesikia mpaka asubuhi tulipoamka na kukuta mlango wa sebuleni uko wazi, hatujui walifungua saa ngapi wala wameingiaje,” alisema Mariam Rashid, mkazi wa Kibaha kwa Mfipa, mkoani Pwani.

Kauli kama hiyo inatolewa na Samwel Tindwa, mkazi wa Tuangoma, Temeke jijini Dar es Salaam, akidai walitumia mlango wa jikoni kuingia ndani.

“Huwa na kawaida ya kuamka saa tisa alfajiri siku zote kwenda msalani, lakini siku ya tukio, sikuamka hadi saa 11 alfajiri niliposhtushwa na mabishano ya mke wangu akimwambia mtoto hakufunga mlango wa jikoni,” alisema Tindwa.

“Ule mlango mimi ndiye niliufunga, nilipoamka kwenda sebuleni nikakuta wamechukua TV ya inchi 50 na redio, nahisi walitupulizia dawa, maana huwa nina kawaida ya kuacha madirisha wazi ili nipate upepo wa nje, tangu mwaka 2013 nilipohamia hapa sijawahi kuibiwa, hii ndiyo mara ya kwanza.”

Sehemu ya dirisha la nyumba ikiwa imekatwa na wezi.

Sophia John, anayeishi Pugu Kajiungeni Dar es Salaam, pia amekutana na dhahama hiyo kama ilivyotokea kwa Adirian Adriano wa Kibaha kwa Mathias ambao wote wameibiwa runinga.

Hata hivyo, Mwanaheri Juma wa Mbagala Rangitatu alisema zaidi ya miaka mitano, hakuwahi kusikia vibaka nyumbani kwake, hadi wiki iliyopita ambako waliingia na kuiba taa zote za nje.

“Kuna mawili, huenda ndiyo wameanza kujitengenezea njia ya kurudi tena na kuamua kuanza na taa, lakini si kwangu tu, hata jirani yangu pia amekutana na masahibu haya,” alisema Kalunde.

Tindwa anazungumzia aina ya vitu vinavyoibiwa sana hivi sasa kuwa ni redio na runinga, huku akisema; “huenda wanaona rahisi kubebeka. Kwangu walichukua TV kubwa ya inchi 50 na redio, katika kupeleleza nimesikia wateja wakubwa wa vitu hivi wengi ni wenye baa na wale wenye mabanda yanayoonyesha mpira au sinema.”

Mariam, mkazi wa Kibaha alisema kwake walichukua TV ya inchi 42, begi la shule la mtoto, suruali na Sh30,000.

“Hawakuwa na nia ya kumdhuru yeyote, waiingia chumba cha watoto na sebuleni, hakuna aliyesikia hadi asubuhi tulipoamka tukakuta tumeibiwa, siku hiyo pia jirani zetu kama wanne nao waliibiwa TV,” alisema.


Kupuliziwa dawa

Dk Abdul Mkeyenge wa Temeke alisema kuna aina nyingi za dawa za usingizi zinazoweza kutumiwa na wezi kufanya uhalifu.

“Ukipuliziwa zinakusababishia usingizi kwa muda fulani, lakini zipo nyingine kama ukiweka maji jirani na dirisha, ikipulizwa nguvu yake inapotea, nyingine zinauzwa kiujanja unjanja tu huko mitaani,” alisema Dk Mkeyenge.

Meza ya kuwekea TV ikiwa tupu baada ya wezi kuiba TV na king'amuzi.

Hali ya ulinzi mitaani

Licha ya baadhi ya Serikali za mitaa kuwa na utaratibu wa ulinzi shiriki, inaelezwa bado mwamko wa wananchi kujitoa ni hafifu.

Baadhi ya viongozi wa Serikali za mitaa, Kibaha na Temeke walioomba hifadhi ya majina yao walisema muitikio wa wananchi kushiriki kwenye ulinzi shirikishi bado mdogo.

“Hapa kwetu tulikuwa na utaratibu wa kila familia kuchangia Sh500 kwa mwezi kwa ajili ya kuwapa motisha mgambo wa kijiji, lakini ikawa ngumu watu wengi kuchangia, hivyo tukaacha jukumu la ulinzi kuwa la kila mmoja wetu,” alisema mmoja wa wenyeviti wa Serikali ya mtaa mjini Kibaha.

Huko Temeke, mwenyekiti mwingine wa mtaa alisema awali walikubaliana Sh5,000 kwa mwezi kwa kila familia.

“Tulienda vizuri, ilisaidia kusahau wizi mtaani, baadaye kuna watu walikataa kutoa, tukasitisha zoezi, hivi sasa hadi mchana kama nyumbani hakuna mtu si salama,” alisema.


Jeshi la Polisi lafunguka

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesisitiza kuendelea kusimamia mifumo ya kiusalama kwa kushirikisha wananchi katika kuzuia, kubaini na kupambana na vitendo vya kihalifu kuanzia ngazi ya mtaa.

“Niwaombe wananchi waendelee kutoa ushirikiano katika operesheni mbalimbali tunazofanya,” alisema Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alipozungumza na Mwananchi.

Alisema wamekuwa wakifanya operesheni zinazosaidia kuwakamata watuhumiwa.

Kamanda Muliro alisema hivi karibuni walifanya doria maeneo mbalimbali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 13 wakiwa na vifaa vya kielektroniki vyenye thamani ya Sh30 milioni, zikiwamo TV.

“Niwaombe wananchi, waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kulinda mitaa yao sambamba na kutoa taarifa mapema kama wamebaini viashiria vya uhalifu katika maeneo yao,” alisema Kamanda Muliro.