Viatu vyamponza akinusurika kifo kwa kipigo kisa wizi wa kuku

Ismail Hassan aliyenusurika kifo kwa kipigo kwa kosa la wizi wa kuku. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

Kijana aliyeiba kuku 11 na kuwachinja kisha kukimbia, viatu vyamkamatisha baada ya kuvisahau bandani wakati akichinja kuku hao.





Mtwara. Taharuki imezika baada ya kijana aliyefahamika kwa jina la Isamail Hassan mkazi wa Magomeni Manispaa ya Mtwara Mikindani kunusurika kifo kwa kipigo baada ya kukamatwa kwa kosa la kutaka kuiba kuku 11 ambao tayari alishawachinja majira ya usiku.


Akizungumza na Mwananchi ilipotembelea katika mtaa wa Magomeni Manispaa ya Mtwara Mikindani Fadhili Chala  mkazi wa mtaa huo alisema kuwa kumekuwa na wizi unaoendelea katika mtaa huo lakini walikuwa hawajapata uhakika nani anafanya vitendo hivyo.


Alisema kuwa kijana huyo alivamia nyumba na kuvunja banda na kuchinja kuku 10 akiwa anamalizia wa 11 alikutwa na wenyewe hivyo akakimbia.

“Huyu dogo tunaishi naye hapa mtaani tulikuwa tunamuhisi kuwa ni mwizi lakini tulikuwa hatuna uhakika ni mgeni anaishi na kaka yake amekuja hivi karibuni lakini tulipoamua kumfatilia tulibaini kuwa mtaa aliotoka alikufukuzwa kwa wizi hivyo tukaanza kuwa makini nae.”


“Baada ya kujua kuwa ameonwa na mwenye kuku alikimbia lakini alisahau kiatu kibaya zaidi mguu wake tunaujua hivyo ikatulahisishia kumfata na tulipomuuliza alikiri kuiba na kwenda kuwauza”


Naye Getruda Nyagari makazi wa magomeni kwa mtawike (aliyeibiwa) alisema kuwa nikiwa nimelala nilisikia kuku wanalia bandani nikaona sio kawaida ikabidi nitoke nje ambapo nilimuona mwizi akiwa kashika kuku na kisu mkononi.


“Nilipoona ameshika kisu nilirudi ndani haraka kwakujihami nikajifungia na kuanza kuita mwizi nikiwa ndani majirani waliposikia walitoka nje na mimi nikatoka nje na kuanza kumsaka mwizi huyo ambaye tayari alikuwa ameshaaondoka eneo lile na alikuwa amewachinja kuku 11 tayari kwenye karo” alisema Nyagari 


Nae Sylivia Mbogo Mkazi wa Magomeni alisema kuwa yeye ameshawahi kuibiwa zaidi ya mara mbili ambapo awamu kwanza aliibiwa kuku wanne na awamu ya pili kuku 12 wote walichinjwa hivyo kumfanya awe na hofu.


“Huyu mwizi amekuwa na tabia ya kuiba majumbani mimi pia niliwahi kuibiwa zaidi ya mara mbili na mara ya pili alichinja kuku 12 bandani yaani naamka nakuta damu ndani ya banda ilinisikitisha sana” alisema Mbogo


Kwa upande wake mwizi mwenyewe kabla hajapelekwa Polisi, Issmail Hassan alikiri kufanya wizi huo kisha kwenda kuuza kuku hao ili apate riziki.


“Ni kweli nimechinja kuku ambao sio wangu kwa hiyo mimi ni mwizi sirudii tena yaani nimepigwa sana naomba mnisamehe nikirudia mnifanye chochote ila wizi nimeacha kuanzia leo usiku nilikuwa na pita tu nikakuta kuku nikachukua na kuchinja kuku saba tu” alisema Hassan


Kwa upande wake mjumbe wa mtaa wa Chipuputa Dadi Likammalila alisema kuwa tukio hilo sio zuri kwakuwa limekuwa likisikika bila kujua nani anafanya hivyo kukamatwa kwake kutaleta amani katika mtaa huo.


Vilevile Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara Nicodemus Katembo amesema kuwa anafatilia tukio hilo kisha atatoa taarifa kamili.