Dart yawashushia rungu watumishi sita, wamo madereva Mwendokasi

Muktasari:

  • Watumishi sita wa Dart na Udart watachukulia hatua za kinidhamu baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma bora kwa abiria wanaotumia usafiri wa mabasi ya mwendokasi.

Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) umewasimamisha kazi watumishi wawili – Shabani Kajiru na Brown Mlawa ili kupisha uchunguzi wa kina dhidi yao, baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kajiru ni msimamizi wa Kituo cha Mwendokasi cha Kiuvukoni na Mlawa ni ofisa ufuatiliaji wa kituo hicho. Watumishi hao wanadaiwa kushindwa kuchukua hatua za haraka baada ya kutokea sintofahamu kati ya abiria waliokuwepo kituoni hapo na madereva wa mabasi hayo.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Machi 28, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia imeeleza kuwa Machi 26, 2024 saa mbili usiku katika kituo cha mwendokasi cha Kivukoni, kulitokea vurugu kati ya abiria na madereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Morocco na Kivukoni.

Kihamia amesema hali hiyo ilitokana na abiria wengi waliokuwa wanasubiri basi la kwenda Kimara kwa muda, kuamua kuingia katika basi la Morocco na kumwamuru dereva wa basi aliyekuwa na mwenzake wawapeleke Kimara.

“Madereva hao waliendelea na kusimamia ratiba ya basi na kukataa kuwapeleka Kimara, hali iliyosababisha vurugu kati ya abiria na madereva hao waliopeleka basi hilo Morocco. Baada ya malumbano ya muda mrefu waliamua kuwarudisha abiria hao Kivukoni, kitu ambacho sio busara.

“Hali ya malumbano ilipozidi, waliamua kuwapeleka abiria hao Kimara, Kajiru alipata taarifa hizi mapema lakini hakuzifanyia kazi,” amesema Kihamia katika taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Dk Kihamia amemwelekeza mtoa huduma wa mpito (Udart) kuwachukulia hatua stahiki, ikiwemo kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa kina madereva Salehe Maziku na Chande Likotimu waliokuwa wakiendesha basi hilo.

Pia, ameagiza Udart kuwasimamisha kazi msimamizi wa Kituo cha Mwendokasi cha Kivukoni Lameck Kapufi pamoja na ofisa usafirishaji, Erick Mukaro huku Dart ikitoa onyo kwa watumishi, kuwa haitasita kuwachukulia hatua watakaobainika kukiuka maadili ya utoaji wa huduma kwa wananchi wanaotumia usafiri huo.

“Dart inaomba radhi kwa kilichotokea na tunaahidi kuendelea kuboresha huduma zaidi kwa wananchi, lakini pia tunawataka watumiaji wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka kufuata utaratibu uliokwekwa na wakala pamoja na mtoa huduma,” amesema Kihamia.