Wadau usafirishaji wachambua uteuzi bosi mpya Dart

Muktasari:

  • Awali, Dart ilikuwa ikiongozwa na Dk Edwin Mhede, aliyedumu kwa siku 971 kabla ya uteuzi wake kutenguliwa.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Dk Athumani Kihamia kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka(Dart), wadau wa usafirishaji wamechambua uteuzi wake.

Taarifa ya uteuzi wa Dk Kihamia imetolewa usiku wa Alhamisi, Januari 11, 2024 kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus.

Wakiuchumbua uteuzi wa Dk  Kihamia kwa nyakati tofauti, wadau wa usafirishaji nchini, akiwamo  Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori  wa Kati na Wadogo(Tamstoa), Chuki Shabani wamesema shida sio kubadilisha viongozi, bali ni namna ya watu walioteuliwa kusimamia mradi huo.

Shabani amesema ifike mahali wanaoteulia kusimamia mradi huo wawe na uzoefu katika sekta ya usafirishaji.

“Kama mnakumbuka zamani tulikuwa na mtu anaitwa Mwaibula, huyu jamaa alileta mabadiliko makubwa sana katika sekta ya usafirishaji kwa kutujia na ubunifu wa mistari ya rangi katika ruti mbalimbali za daladala,”amesema Shabani.

Ameongeza kuwa mradi huo watu wanapaswa kuelewa kuwa ni biashara na biashara haihitaji digrii.

“Biashara ni kile kipaji kutoka kwa Mungu, na sio digrii za darasani, hivyo kwa mradi huu wa mwendokasi walau wangemuingiza mtu mmoja aliye na uzoefu katika usafirishaji awe hata mwenyekiti na kusaidia kuongoza wasomi waliopo,”amesema.

Mwenyekiti huyo amesema kwa miaka minane ambayo mradi huo umeanza, waendeshaji walianza na mabasi 200, na baadaye wakaongezewa na Serikali 70, lakini leo mabasi mazima yaliyopo hayazidi hata 40.

“Wakati  kuna mfanyabiashara wa usafiri wa mabasi ya kwenda mikoani kwa miaka hiyo  minane alianza na basi moja lakini sasa anayo 30, ni wazi kwamba hapo kuna tatizo.

“Pia, tujiulize wakati ule tuna viwanda vya nguo ikiwamo Urafiki, Ufi, vilikuwa vinafanya kazi vizuri  bila ya kuwa na wasomi, lakini sasa hivi kipindi ambacho tuna wasomi wengi, tuulizane hivyo viwanda vipo wapi,?”amesema Shabani.

Hata hivyo, amesema kama  italazimu wasomi wawepo basi  sio wa makaratasi tu, bali wenye uzoefu kwenye biashara ya usafirishaji.

Msemaji wa Chama cha  Wamiliki wa Mabasi Tanzania(Taboa), Mustapha Mwalongo amesema mtendaji wa kusimamia mradi huo anapaswa kuwa mtu wa kuingia mtaani mara kwa mara kujionea huduma na sio kusubiri taarifa kutoka kwa watendji wake wa chini.

“Wengi wanaoajiriwa mwendokasi naona ni watu wanaojihusisha sana  na ofisi kuliko kuingia kunapotolewa huduma mtaani, hii ni kazi isiyohitaji makaratasi mengi.

“Huko mtaani akiingia  ndipo atakutana na changamoto za magari, abiria, vituo na kisha kwenda kuishauri bodi hiki tufanye hiki, kile tufanye hivi kwa kuwa kazi ya gari ndio inataka hivyo na sio maandishi kwenye makaratasi,” amesema  Mwalongo.

“Sisi wamiliki wa mabasi, kuna muda tunashtukiza kuingia kwenye mabasi, huko tunakutana na abiria wamewekewa vigoda, ndoo za kukalia katikati na mambo mengine, hapo tunachukua hatua haraka, lakini sio kusubiri kuletewa taarifa ofisini au kupata malalamiko kutoka kwa abiria ni wazi kuna muda utaletewa za uongo,”amesema Mwalongo.

Mmoja wa wamiliki wa daladala na mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Wilaya ya Kinondoni(Uwadar),Ghalib Mohammed amesema kazi ya Dart ni kumsimamia mwendeshaji ambaye ni Udart (Kampuni ya Usafirishaji wa Mabasi yaendayo Haraka ) kuleta huduma nzuri kwa wananchi.

 Lakini Mohamed anaonyesha wasiwasi wake kuwa hili haliwezi kusimamiwa vizuri kwa kuwa mamlaka zote hizo watendaji wake kwa sasa wameteuliwa na serikali hivyo hakuna wa kumsimaia mwenzie.

Badala yake alishauri kuwa ni vema mwendeshaji akabaki kuwa mtu binafsi, na kama wa kwanza ameonekana kushindwa atafutwe mwingine na wawe wawili hadi watatu ili kuleta ushindani.

“Kwa miaka yote hiyo tangu usafiri huu wa mwendokasi uanze, kumebadilisha wakurugenzi mbalimbali, hatuoni mabadiliko yoyote zaidi ya sura mpya za watu lakini hali ya usafiri inazidi kuwa mbaya kila kukicha.

“Hebu ifike mahali waachiwe watu bianafsi, kwa kuwa hawa wanaendesha shughuli hiyo kwa faida, wakiona mabasi yameharibika wanaagiza mapya, lakini kwa Serikali mtendaji ataona kama wafanyakazi wanalipwa, mabasi yakiharibika akiandikia anapewa hela anayatengeneza, hawezi kuumiza kichwa huyu,”amesema Mohammed.

Pia, amekumbushia kipindi ambacho Serikali ilikuwa ikitoa huduma ya usafiri wa daladala ukilinganisha na sasa, akisema hali imekuwa tofauti na kuitaka ijaribu kuwapa hata wamiliki wa daladala kuifanya hiyo kazi waone kama hakutakuwa na mabadiliko.

Pia, amesema ni vema wakaondoa masharti ya kuwataka kujiunga kama kampuni ndio waukamate mradi huo, kwa kuwa hivi sasa biashara imebadilika mtu mmoja anaweza kuwa kampuni kubwa na mambo yakaenda.

“Uzuri bei za mabasi tunazijua na yanapopatikana, benki zipo tayari kutukopesha, watengenezaji wa mabasi pia wapo tayari kutukopesha, tunachosubiri ni Serikali tu ituruhusu kwa kuwa uwezo huo tunao, watuamini tu,”amesema mmiliki huyo.