Sanamu ya Karume ilivyotelekezwa porini bila matunzo

Sanamu la Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume likiwa katikati ya pori baada ya kutelekezwa eneo la Bwawani Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Jumbe aliiongoza Zanzibar kuanzia Aprili 1972 akimrithi hayati Karume hadi mwaka 1984 alipolazimika kujiuzulu kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa visiwani humo.

Unguja. Katika hali ya kushangaza, wakati Zanzibar imetoka kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi, mamlaka zinaonekana kujisahau kuhusu matunzo ya alama zake kuu za Taifa.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini moja kati ya sanamu tatu za mwasisi wa Mapinduzi hayo, Hayati Abeid Amani Karume, imetelekezwa katikati ya pori bila ya uangalizi wowote.

Sanamu hiyo ni iliyopo nyuma ya jengo la iliyokuwa hoteli ya Bwawani katika Mtaa wa Funguni mjini Zanzibar ambayo sasa imebaki kuwa gofu.

Katika azma ya kumuenzi Rais huyo wa kwanza wa Zanzibar aliyeuawa Aprili 7, 1972 ndani ya ofisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Unguja, wakati huo zikiwa ofisi za Chama cha Afro Shirazi (ASP), Serikali ilitengeneza sanamu tatu kutoka India kwenye miaka ya 1970 chini ya wataalamu kutoka Urusi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amekiri kutofahamu iwapo kuna mazingira ya aina hiyo ya sanamu ya muasisi huyo.

Ameahidi kuchukua hatua za haraka kufuatilia ili apate maelezo mazuri kutoka kwa wasaidizi wake.

Ofisa mmoja mwandamizi mstaafu aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kwa sharti la kutokutajwa jina, ameliambia Mwananchi kuwa hiyo ilikuwa fikra ya Rais wa Zanzibar wa awamu ya pili, Hayati Aboud Jumbe Mwinyi.

Jumbe ameiongoza Zanzibar kuanzia Aprili 1972 akimrithi hayati Karume hadi mwaka 1984 alipolazimika kujiuzulu kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa visiwani humo.

“Tatizo letu hatuna utamaduni mzuri wa kutunza kumbukumbu. Sanamu hizi zilipokuja nchini zilikuwa na rangi nzuri ya dhahabu,” amesema mstaafu huyo na kuongeza:

“Lakini kwa utashi wa baadhi ya watu tu zikapakwa rangi nyeusi na kupoteza haiba yake.”

Hata hivyo, licha ya kupakwa rangi na kuharibiwa, hilo linaweza lisiwe tatizo kubwa, changamoto ni sanamu hizo ambazo zimekosa matunzo na kutelekezwa.

Sanamu moja kati ya hizo imewekwa mbele ya ofisi za CCM Kisiwandui na nyingine katika Uwanja wa Ndege Chake Chake, Pemba, zote zikitunzwa vizuri zakionekana safi wakati wote.

Wiki kadhaa zilizopita, mwandishi wetu alitembelea eneo la nyuma ya hoteli ya Bwawani ambako kwa sasa imebaki gofu baada ya Serikali kutangaza kuitoa kwa mwekezaji binafsi, mchakato uliokwama kwa muda mrefu sasa.

Wakati huo kilikuwa kipindi cha wiki ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo mwaka huu yalitimiza miaka 60 kwa sherehe za aina yake.

Kinyume cha matarajio ya wengi kukuta sanamu hiyo iko katika hali ya usafi na matunzo mazuri, kilichopo imekutwa katikati ya msitu. Kwa sasa eneo la gofu la hoteli hiyo iliyong’olewa kila kitu kama vile madirisha, milango na vifaa vyake vyote vya hoteli kupotea halitamaniki kwa lolote.

Baadhi ya watu wanahoji ni kwa namna gani wana Mapinduzi wenye mapenzi kwa kiongozi aliyeongoza ukombozi, kuiacha sanamu hiyo bila matunzo.

“Ni kweli hoteli haifanyi kazi na sasa inatafutiwa mwekezaji, lakini si busara kuiacha ikifunikwa na pori kubwa pamoja na kuificha alama ya mwasisi wa Taifa,” amesema mmoja wa waliokuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo na kuongeza:

“Lazima Serikali ione aibu kwa hili na ifanye kitu kuweka mambo sawa.”

Mjasiriamali anayefanya shughuli za mamalishe jirani na eneo hilo, Mwanahawa Mfamau, amehoji sababu ya Serikali kuweka askari wa vikosi vya SMZ kulinda magofu hayo, akiuliza wanalinda kitu gani?

Ameshauri pamoja na kulinda, ni vyema askari hao wapewe kazi ya kufyeka pori linaloificha sanamu ya Mzee Karume ili eneo hilo liwe safi na salama.

Amesema kuliacha pori hilo pia kunahatarisha usalama wa wananchi na hata wageni wanaotembelea Zanzibar, kwani wahalifu wanaweza kulitumia kwa maficho baada ya kufanya matukio ya wizi, ukabaji na ubakaji.

Kauli ya Mwanahawa haitofautiani sana na hoja ya Khatib Ali, ambaye amesema viongozi wanaendeleza na kulinda alama zinazoonekana kwa wepesi machoni kwa wengi.

Amesema sanamu hiyo kwa kuwa ipo katika eneo ambalo halina mwingiliano wa watu wengi ndiyo maana limesahaulika, akidai hawamtendei haki si tu mwenye sanamu hiyo, bali hata aliyeamua itengenezwe kwa ajili ya kumbukumbu na alama za Taifa.

“Hata Wazanzibari wenyewe hawatendewi haki, kwani yule ni kiongozi mkuu na mwasisi wa Taifa hili, kwa hiyo alama zake hata picha ni haki kutunzwa katika heshima yake,” amesema.

Mmoja wa wataalamu wa sanaa ya uchoraji kisiwani hapa, Abdulraziz Abdul amesema kuliko sanamu hiyo itelekezwe ni vyema ikabomolewa, maana katika mazingira hayo haileti heshima na taswira nzuri kwa kiongozi mkuu kama huyo.

Amesema kitaalamu, sanamu ni alama muhimu ambayo hubeba na kuzingatia heshima zote za mtu husika, hivyo haina budi kulindwa na kuheshimiwa.

Mbali na kupewa heshima, lakini inatumika kama ukumbusho na inaweza kuwa kivutio kwa wageni wanapotembelea nchi husika wanaposoma historia huhusianisha na picha au sanamu ya muhusika mwenyewe.

Kabla ya kukumbwa na masaibu hayo, Hoteli ya Bwawani ilikuwa ya kwanza ya aina yake kwa ukubwa na uzuri, kumilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ujenzi wake ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1970 kabla ya kifo cha Mzee Karume, na ilipoanza kazi ya kupokea watalii na wageni wengine, ilisifika kwa kiwango kizuri cha huduma hali iliyochangia kukua kwa utalii wa Zanzibar.