Othman akosoa mfumo wa utendaji nchini

Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa  Zanzibar, Othman Massoud Othman (kushoto),   akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano na mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Jesse Mikofu,  yaliyofanyika nyumbani kwake Chukwani, Zanzibar leo. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

Othman ametoa mfano wa kasoro zinazotokea kwenye uchaguzi, akisema ifike mahali waachiwe watu wafanye uamuzi

 Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud, amesema licha ya Tanzania kuwa na fursa nyingi na wananchi kusikilizana, inaathiriwa na mfumo wa uendeshaji nchi ambao unahitaji kurekebishwa.

Amesema mfumo uliopo kwa sasa unaruhusu baadhi ya taasisi kuendeshwa kiitikadi na dhuluma, jambo ambalo halisaidii nchi, hivyo kuhitaji marekebisho.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alizungumza hayo leo Aprili 22, 2024 katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Unguja.

“Kama Mungu kutupenda basi katupenda sana, bado tuna fursa ya kukaa chini kwa madhehebu ya dini, vyama vya siasa na tukazungumza mambo yetu bila uhasama, Mungu katujaalia, tuitumie fursa hiyo kusimamia mabadiliko na mageuzi kuifanya nchi hii kuhakikisha mfumo wetu wa uendeshaji wa nchi ubadilike,” amesema.

Amesema katika mfumo wa uwajibikaji kila mtu analalamika hata mamlaka zenyewe.

“CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali analalamika, Rais kila siku anapanga na kutumbua, kuna vitu ambavyo tunahitaji kufanya marekebisho, shida yetu bado kuna maeneo mfumo wa kitaasisi tunaenda kwa itikadi na dhuluma hii nadhani haitusaidii,” alisema.

“Lazima kwa pamoja tushirikiane tujenge na tuseme ni Tanzania ipi tunayoitaka na tuje na mpango unaosema lazima tufanye marekebisho,” amesema.

Ametoa mfano wa kasoro zinazotokea kwenye uchaguzi, akisema ifike mahali waachiwe watu wafanye uamuzi.

“Hii ndiyo itakayotujenga lakini kila mmoja anachukua faida kwa sababu refarii anaye mkononi, haya ni mambo ya kizamani. Sote kwa pamoja tufike mahali tujenge mustakabali wa nchi yetu. Bado tunayo fursa kubwa na si kwamba itadumu kila siku ikija ikaparaganyika kidogo hatutaweza kuipata tena,” ameeleza.


Mafanikio ya ACT-Wazalendo

Akizungumzia mafanikio ya ACT-Wazalendo ikifikisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, na mipango ya baadaye,  alisema licha ya uchanga wa chama hicho kimepiga hatua kuvizidi vyama vilivyoanzishwa miaka mingi.

Amesema chama hicho kimeshiriki uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza mwaka 2015, wa pili mwaka 2020, na kinatarajia kushiriki wa tatu mwaka 2025.

“Kwanza chama ni wanachama, ukitazama idadi ya wanachama kimekuwa zaidi ya mara 20 ikilinganishwa na kilivyoanza, kubwa zaidi mtandao wa chama kuwa taasisi umekua kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Amesema kwa mara ya kwanza katika mkutano wa ACT-Wazalendo uliofanyika hivi karibuni,  ulihudhuriwa na wajumbe kutoka majimbo yote 226 ya uchaguzi, na kimefanya uchaguzi ngazi ya mikoa 39 ya kichama.

Alisema hiyo ni hatua kubwa kitaasisi kwani uongozi wa chama hicho umekamilika.

“Ni chama ambacho naweza kusema kimekamilika na hii ni kuonyesha kiasi gani tumekua. Kuna vyama vimeanzishwa miaka mingi lakini naamini kitaasisi haviwezi kufikia hata robo ya ACT-Wazalendo tulipofikia hivi sasa,” amesema.

Amesema pia chama hicho kimekuwa na nyenzo, ikiwemo mpango mkakati na wameandaa ahadi kwa Watanzania ambayo ilizinduliwa na kuanza kufundishwa kwa wanachama na wafuasi wao.

Amesema wana maono na kuwa na mafunzo ya viongozi kwa kushirikiana na taasisi, vyama na jumuiya za vyama vya siasa.

“Kwa hiyo, unaona ACT tulipotoka na tulipo inaonyesha ni chama makini, chama ambacho kinakua. Kwetu sisi ni jambo muhimu sana,” amesema.


Miaka 10 ijayo

Katika maono yake kwa miaka 10 ijayo, Othman alisema Watanzania hawatawapima walipo sasa, watawapima kwa watakayokuwa wamefanya kupitia mpango mkakati maalumu.

Hata hivyo, ameisema mpango huo unafanyiwa tathmini na wataalamu kisha kutengeneza uwezo kitaasisi.

Amesema kupitia mpango wa Ahadi kwa Watanzania wa mwaka 2020/25 na 2025/30, utawaongoza kuelekea wanapotaka kwenda.

Othman amesema wamekusudia kufanya kazi, kukua kitaasisi na kushirikiana na watu.


Kushika dola

Kama ilivyo lengo la chama cha siasa kushika dola, Othman alisema wamejipanga kuishika hivi karibuni na kwa jinsi mipango ilivyo wanaamini watafanikiwa kwani wanaenda hatua kwa hatua.

“Kwa mfano, kwa upande huu wa Zanzibar hili ni suala la wakati tu, ni jambo ambalo tukiwa na uchaguzi wa kweli hautakuwa kama wa mwaka 2020, hilo kwa Zanzibar tuna hakika. Kwa upande wa Tanzania Bara, tunayo kazi ya kufanya na tunaamini tutafika si muda mrefu,” amesema Othman.

Amesema kuna mambo mengi ya kujifunza kwa Zanzibar ambayo wanaamini yatawasaidia Tanzania Bara.

Amesema mbinu waliyotumia kupata wananchi Zanzibar ndiyo wanayoenda kuitumia Tanzania Bara.

“Tunaamni Watanzania wa leo ukiwafikia, ukawajulisha, ukawaeleza na kuwafanya na wao wajiulize maswali kama ninavyojiuliza, kwamba nchi yetu ina rasilimali lakini kwa nini tuwe kama tulivyo ndiyo kimewasaidia Zanzibar watu watamani mabadiliko na mageuzi,” amesema.

Alisema kilichobakia sasa ni namna gani ya kuwafikia wananchi na  kuwaeleza.

“Sisi tunaamini maeneo ambayo ulikuwa huyategemei lakini ndiyo yamefanikiwa maana tumekuwa na mtandao wa kichama katika ngazi ya majimbo na mikoa,” amesema.

Othman amesema wananchi kwa sasa kuna mambo wanayatamani na wana uelewa tofauti na ilivyokuwa nyuma kwa hiyo ni jambo la kujipanga kufikisha ujumbe kwa Watanzania.

“Mikakati tunayo, kusema kweli yaliyopo Zanzibar yametufunza na yatatusaidia katika kujenga chama hiki katika upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.


Uchaguzi Serikali za Mitaa

Amesema ACT-Wazalendo wamejipanga kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Amesema wamejipanga kuwa na wagombea wengi kadri inavyowezekana.

Amesema hivi sasa wana timu inayofanyia kazi jambo hilo, kuangalia maeneo gani ya kimkakati na ya kushiriki, ili wasipoteze nguvu nyingi kwa mambo mengine.

Hata hivyo, amesema kuna mambo wanahisi ni vyema yakarekebishwa katika mfumo wa uchaguzi, kwani wamepata uzoefu baada ya kushiriki katika uchaguzi mdogo na wameona changamoto zilizopo.

Amesema wanaelekea kwenye Tume Huru ya Uchaguzi, lakini ngazi ya chini kwenye halmashauri mambo ni bado.

Othman amesema hivyo watafanya mawasiliano na Serikali na vyama vya siasa kupitia Baraza la Vyama vya Siasa.


Haki katika uchaguzi

Amesema si kwamba haki itakuja yenyewe bali inatakiwa kutafutwa kwani kuna watu wamejengwa kwa muda mrefu (akimaanisha wamejengwa kutotenda haki).

“Kwa hiyo haya ni mambo lazima tuyafanyie kazi, kama uchaguzi huu utafanyika kesho hatuamini kama kutakuwa na haki, hatujafika huko, lakini tunayo fursa ya kufika huko,” amesema.

Anataja mipango ya kuwafikisha huko ni kuhakikisha wanatumia mbinu kadhaa ikiwa ni pamoja na kupeleka hoja zao katika Serikali, viongozi wa vyama na kuna baadhi ya maeneo yamezaa tija.

“Wakati mwingine mnaweza kuwa na mfumo lakini unahitaji wasimamizi wazuri. Kwa hiyo sisi hatufanyi maandamano lakini tunatumia njia tunazohisia zitasaidia ndiyo hizo za kupeleka hoja kukutana na viongozi,” amesema.