Mwanamke ni mwarobaini wa changamoto za huduma za maji safi na usafi wa mazingira

Dar es Salaam. Maji ni rasilimali muhimu kwa ajili ya ustawi wa
jamii na maendeleo kwa ujumla. Amani haitawali, pahali pasipo
na maji.

Ndiyo maana Umoja wa Mataifa (UN), kuelekea katika
maadhimisho ya Siku ya Maji duniani, Machi 20, imeamua kuja
na: “Uhakika wa maji kwa amani na utulivu,” kama kauli mbiu ya
kuhamasisha usimamizi mzuri wa rasilimali maji kwa ajili ya kuleta
amani na utulivu miongoni mwa jamii.

Hatua kubwa za maendeleo zimepigwa hadi sasa, hata hivyo, ni
theluthi mbili tu (sawa na asilimia 67) ya shule zinazopata maji ya
kunywa na kwa wasichana, upatikanaji wa huduma za maji safi,
na usafi wa mazingira ni jambo muhimu linaloathiri mahudhurio ya
shule, hususan wakati wa hedhi, na ni moja ya sababu kuu za
wasichana kuacha shule.

Inaelezwa kuwa asilimia 43 ya zahanati na 13 ya vituo vya afya
vyenye vyoo havifikiwi na wagonjwa. Kuondoa maambukizi katika
vituo vya afya ni muhimu katika kupunguza vifo vya akina mama
wajawazito wanaojifungua katika vituo hivyo ambapo takriban
asilimia 93 ya akina hao wameripotiwa kupoteza maisha.

Serikali inatambua kuwa bado wanawake ndiyo wahanga
wakubwa pindi maji safi, huduma za usafi wa mazingira na vyoo
bora vinapokosekana, na hiyo inaongeza uhitaji wa mbinu mpya
na bunifu za kukabiliana na changamoto za sekta hiyo.

Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan alijitokeza
hadharani na kuahidi kuwa atafanya kazi ya kuwaondolea
wanawake mzigo wa kubebea ndoo kichwani (yaani “Kumtua
Mama Ndoo Kichwani”).

Kampeni hiyo maarufu ya Rais inalenga kuinua uwekezaji katika
usambazaji wa maji majumbani kwa kufanya maji safi na salama
yapatikane kwa wote kwa umbali unaokubalika ili wanawake
wasisafiri tena umbali mrefu kuchota maji.

Kujumuishwa kwa masuala ya kijinsia katika usimamizi wa
rasilimali za maji, inawafanya wanawake kukaa katika meza ya
kufanya maamuzi yanayohusu masuala ya maji safi na usafi wa
mazingira, kwa kuwa tayari wana ufahamu wa changamoto
zinazowakabili.

Serikali kupitia mpango wa WSDP (III) imedhamiria
kuwajumuisha wanawake moja kwa moja katika ngazi za
maamuzi yanayohusisha upatikanaji wa huduma za maji na usafi
wa mazingira kufikia asilimia 30 na kuhakikisha usawa wa kijinsia
katika sekta ya maji unafikiwa ifikapo mwaka 2025.

Utekelezaji wa malengo hayo utahusisha kuendesha semina
elekezi kuhusu umuhimu wa usawa katika usambazaji wa
huduma za maji, mafunzo ya jinsi ya kuzingatia usawa wa kijinsia
katika huduma za maji na kuwashirikisha wanawake katika
maamuzi yanayohusu huduma ya maji.

Uwezeshaji wa wanawake katika huduma za maji na usafi wa
mazingira unahusu kupanua uwezo wa kufanya uchaguzi na
udhibiti katika maeneo mengi yanayohusiana na WASH.

Hivyo, upatikanaji wa rasilimali za maji safi kwa wanawake,
ufanyaji maamuzi, na kuimarisha sera na michakato mipana zaidi
ya kitaasisi inayojibu changamoto zao (wanawake na wasichana),
inasaidia kutimiza mahtaji ya kila siku na ya muda mrefu ya
huduma za maji na usafi wa mazingira.

Kwa upande wa sekta binafsi, WaterAid, kwa nafasi yake kama
mdau muhimu wa masuala ya huduma za maji na usafi wa
mazingira nchini, ajenda ya ujumuishi na ushirikishaji wanawake
imekuwa sehemu ya uzoefu wao kwa muda sasa kupitia Mpango
Mkakati wa Tanzania wa Miaka Mitano (2023-2028), ambao

umeeleza nafasi ya mwanamke katika kutafuta masuluhisho ya
kudumu katika sekta ya maji.
Taasisi hiyo inasukumwa na maono ya kuhakikisha kuwa hakuna
mwanafunzi wa kike anayeshindwa kufikia malengo yake kwa
kuwa shuleni kwao hakuna miundombinu ya maji au usafi wa
mazingira inayomfanya ashindwe kusoma anapokuwa katika
hedhi.

WaterAid, kupitia, wadau mbalimbali imesaidia ujenzi wa
miundombinu ya huduma za maji tangu mwaka 1983, ikisaidia
wanawake wenye uhitaji kukabili changamoto za utembeaji
umbali mrefu kutafuta maji.

Kiujumla, kwa miaka zaidi ya 40 ya uzoefu wa kufanya kazi
nchini, taasisi hiyo imesaidia watu milioni 1.8 kupata huduma ya
maji safi, watu 800,000 kupata vyoo bora na watu milioni 26
kupatiwa msaada wa huduma za usafi wa mwili na mazingira.

Kama hiyo haitoshi, taasisi hiyo imetekeleza miradi
inayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu na kuwa viongozi
wanaoweza kufanya maamuzi na kupanga mikakati inayohusu
huduma za maji na usafi wa mazingira na kufanya kazi na
wanaume na viongozi kuwahamasisha kuhusu nafasi ya
wanawake katika majukumu ya kufanya maamuzi huku
ikihakikisha wanawake wananufaika nayo na kuweza kushiriki
katika shughuli za kiuchumi zinazohusiana na huduma hizo.
Mkurugenzi Mkaazi wa WaterAid nchini, Anna Mzinga anasema:

“Maendeleo yanayojumuisha usawa yanajikita zaidi katika
kutambua vikwazo vya huduma za maji na usafi wa mazingira na
kuja na afua zitakazosaidia kuziondoa moja kwa moja.

Afua hizo zitaangalia jinsi ya kuwawezesha wanawake walio
katika mazingira magumu kudai haki zao na kuziendea fursa za
usimamizi wa rasilimali mali za maji kwa wao ndiyo waangalizi wa
kwanza wa familia huku zikiwapa elimu mamlaka zinazohusiana
na huduma hizo au wanaofanya maamuzi kujua kile

wanachopaswa kufanya ili kuhakikisha wanawake hawachwi
nyuma.

Kupitia uandaaji, mapitio na uwekezaji wazi mikakati kwa wadau
wa sekta ya maji wanaweza kuendesha mafunzo kwa mabalozi
wa usawa wa kijinsia katika sekta ya maji, kufanya tafiti
mbalimbali za tathmini ya athari na kuchapisha matokeo na
kuendelea mapambano katika kufikia usawa wa kijinsia kwenye
sekta ya maji.

Nyakati zimebadilika, na dunia ina mtazamo mpya wa jinsi ya
kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za maji na usafi
wa mazingira, wanawake wakiwa ndiyo kiini cha utafutaji majibu
ya changamotoo zilizopo za upatikanaji na usambazaji wa
huduma za maji na usafi wa mazingira.