Zwena nje Mamelodi ikiivaa Yanga

Muktasari:

  • Mamelodi itatua nchini na zaidi ya watu 70 kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 usiku.

Kikosi cha Mamelodi Sundowns ambacho kinatarajiwa kutua nchini kesho kitakuwa bila nahodha wake Themba Zwane, ambaye hatacheza mchezo wa Jumamosi ijayo.

Mamelodi itatua nchini na zaidi ya watu 70 kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 usiku.

Zwana ambaye ni mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho hatakuwepo kwenye mchezo huo baada ya kuwa na kadi tatu za njano alizopewa kwenye michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Huyu ni kati ya mastaa wa Mamelodi ambao wamekuwa na heshima kubwa kwenye kikosi hicho alichoanza kukitumikia mwaka 2011, lakini akiwa na historia nzuri ya kupewa kadi kwenye michezo ya ligi pamoja na ile ya kimataifa.

Kiungo huyo mshambuliaji, alipewa kadi kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe katika dakika ya 47, Pyramids dakika ya 65 na kurudia tena kwenye mechi dhidi ya Mazembe dakika ya 90.
Rekodi zinaonyesha kuwa kiungo huyo anayeichezea timu ya Taifa ya Afrika Kusini  alijiunga na Mamelodi mwaka 2011.

Kwenye michezo sita ya makundi amefanikiwa kucheza dakika 328, lakini akitajwa kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho, mara nyingi amekuwa akikosekana kwenye kikosi cha Mamelodi anaingia winga Lesiba Nku.

Staa huyo anayevaa jezi namba 18, ameitumikia timu ya Taifa ya Afrika Kusini  michezo 39 na kufunga mabao tisa, akiwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu amepiga pasi 222, amegusa mpira mara 322 kwa jumla, hajafanikiwa kufunga bao lolote akiwa amepiga mashuti manne na mawili ndiyo yamelenga lango.

Katika Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2023), alifanikiwa kufunga mabao mawili mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya Namibia.