Xavi aweka rekodi ya kadi Ulaya

Hispania. Kocha wa Barcelona Xavi Hernandez, ameweka rekodi ya kadi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya juzi kutolewa uwanjani.

Xavi aliishuhudia timu yake ya Barcelona ikiondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na PSG baada ya kuchapwa mabao 4-1, ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Camp Nou na kutupwa nje kwenye hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 6-1, huku kocha huyo akipewa kadi nyekundu ya tatu.

Xavi sasa ameweka rekodi ya makocha wa La Liga waliopewa kadi nyingi, akiwa ameshapewa nyekundu tatu na za njano 22, kuanzia alipoanza kuifundiaha Barcelona miaka miwili iliyopita.

Huu ulikuwa mchezo ambao unaonekana kuwa upande wa Barcelona baada ya kushinda ule wa kwanza kwa mabao 3-2 nchini Ufaransa wiki moja iliyopo, hivyo kupewa nafasi kubwa ya kuvuka kwenye hatua hii.

Mwamuzi Istvan Kovacs, alitoa kadi nyekundu upande wa Barcelona kwenye mchezo huo uliokuwa na kasi ya hali ya juu.

Pigo kubwa la Barcelona ilikuwa kadi ya dakika ya 30 ya mchezo aliyopewa  Ronald Araujo, ambaye alidaiwa kumwangusha Bradley Barcola hali ambayo ilianza kuzua malalamiko kutoka kwa Xavi.

"Maamuzi yalikuwa mabaya sana, nilimwambia mwamuzi kuwa alichezesha mchezo huu vibaya kuliko. lilikuwa siyo jambo sahihi yeye kutoa kadi ile nyekundu.

"Nilimweleza kuwa yeye ndiye kaumaliza mchezo ule, alikasirika lakini ulikuwa ukweli mtupu. Kumweleza vile alikasirika na kunitoa nje, hakukuwa na jinsi nyingine zaidi ya kusema ukweli.

"Tulikuwa kwenye wakati mgumu baada ya kadi ile, tulipokuwa 11 kwa 11 kila kitu kilionekana kuwa kinaweza kwenda vizuri na timu ilikuwa kwenye muunganiko mzuri.

"Ni aibu kuona msimu unamalizika bila kombe kwa ajili ya mwamuzi, napenda kuona tunacheza 11 kwa 11 kila mchezo, hili suala la kutolewa nje ni baya sana alisema Xavi ambaye ataondoka Barcelona mwishoni mwa msimu huu.

Mchezo mwingine wa usiku wa kuamkia jana, ulishuhudia timu nyingine ya Hispania, Atletico Madrid ikitupwa nje na Borrusia Dortmund baada ya kuchapwa mabao 4-2 na kutupwa nje kwa jumla ya mabao 5-2.