Walimu waonywa mikopo ‘kausha damu’

Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka walimu kukopa kwenye taasisi rasmi za kifdha ikiwamo benki na kuachana na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama mikopo umiza na kausha damu.

Sendiga alisema hayo jana mjini Babati kwenye warsha ya Mwalimu Spesho iliyohusisha walimu 200 wa shule za msingi na sekondari.

“Eneo kubwa lililoathirika na mikopo hii ni kada ya elimu na afya kwa kuweka bondi kadi zao za benki, tunapaswa kuachana na hayo kwani yanadhalilisha na kufedhehesha taaluma," alisema Sendiga.

Aliwataka walimu hao kubadilika na kuachana na mtindo huo mbovu wa maisha wa kujibebea mizigo ya mikopo, kwani inawaathiri kipato chao na cha familia zao kwa ujumla.

Mmoja wa walimu, Abdalah Hussein alisema walimu wengi wanakimbilia mikopo ya kausha damu kutokana na masharti nafuu.

“Mkopo benki ni hadi uwe na dhamana ya nyumba, ila mikopo umiza ukiwa na mtungi wa gesi tu unajitwalia zako bila wasiwasi," alisema Hussein.

Hata hivyo, alisema elimu waliyoipata sasa itawanufaisha kwani walimu wengi wataondokana na mikopo umiza na kausha damu.

Meneja wa benki ya NMB kitengo cha wateja maalumu, Queen Kinyamagoha aliwaahidi walimu hao kuwapatia elimu ya fedha ili watumie mikopo ipasavyo na kutimiza malengo yao.