Simba, Yanga usiku freshi tu

Muktasari:

  • Hiyo ni kutokana na matokeo mazuri ambayo Simba na Yanga zimekuwa zikiyapata kwa emchi za kimataifa ambazo huwa zinacheza usiku kwenye uwanja huo huku mara chache sana zikipoteza.

Dar es Salaam. Muda wa mechi haupaswi kuwa sababu ya kujitetea kwa Simba na Yanga wakati zitakapokabiliana na Al Ahly na Mamelodi Sundowns katika mechi za nyumbani za hatua ya robo fainali ya  Ligi ya Mabingwa Afrika, Ijumaa na Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hiyo ni kutokana na matokeo mazuri ambayo Simba na Yanga zimekuwa zikiyapata kwa mechi za kimataifa ambazo huwa zinacheza usiku kwenye uwanja huo huku mara chache sana zikipoteza.

Ijumaa, Simba itacheza na Al Ahly na Jumamosi, Yanga itaikaribisha Mamelodi Sundowns katika uwanja huo, mechi zote zikipangwa kuchezwa kuanzia saa 3:00 usiku.

Katika mechi tano zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo Simba imecheza usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Mechi za usiku ambazo Simba ilipata ushindi kati ya hizo tano zilizopita ambazo ilicheza usiku, ni dhidi ya Jwaneng Galaxy ambayo ilikuwa ya mwisho ya hatua ya makundi msimu huu ambapo ilipata ushindi wa mabao 6-0, yaliyopachikwa na Clatous Chama, Omar Jobe, Ladack Chasambi, Kibu Denis, Saido Ntibazonkiza na Fabrice Ngoma.

Kabla ya hapo, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya robo fainali ya mashindano ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly, kwa mabao ya Sadio Kanoute na Kibu Denis.

Mechi nyingine mbili ambazo ilipata ushindi usiku zilikuwa ni hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita dhidi ya Horoya ambao iliibuka na mabao 7-0 na dhidi ya Vipers iliyoshinda bao 1-0 lakini ilichapwa mabao 3-0 na Raja Casablanca.

Mechi dhidi ya Horoya, mabao saba ya Simba yalifungwa na Clatous Chama aliyepachika matatu na Sadio Kanoute na Jean Baleke ambao kila mmoja alifunga mawili huku bao m oja la mechi dhidi ya Vipers likifungwa na Chama.

Kwa upande wa Yanga, katika mechi tano zilizopita ambazo ilicheza usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ilipata ushindi mara tatu na kutoka sare mbili.

Mchezo ambao iliibuka na ushindi mkubwa ni ule ambao iliichapa CR Belouizdad kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo ilishinda mabao 4-0 yakipachikwa na Mudathir Yahya, Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki na Joseph Guede na kabla ya hapo ilitoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly, bao lake lilipachikwa na Pacome Zouzoua.

Katika mechi nyingine ya usiku, ilitoka sare ya bila kufungana na Rivers United katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na iliichapa Monastir kwa mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa usiku ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, ikipata mabao yake kupitia kwa Kennedy Musonda na Fiston Mayele.

Winga wa zamani wa Simba, Uhuru Selemani alisema kuwa ushindi wa Simba na Yanga nyumbani utachangiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji.

"Kama wachezaji wasipocheza kwa kujitolea na kufuata vyema kile wanachoelekezwa, makocha watakuwa wanafanya kazi bure hata kama ni wazuri. Wachezaji wa Simba na Yanga wanapaswa kufahamu kwamba hii ni nafasi nzuri kwao kujiweka katika ramani ya soka Afrika kwa kuzitoa Mamelodi na Al Ahly," alisema Uhuru.

chezaji wa zamani wa Yanga, Kenny Mkapa alisema kuwa inawezekana Yanga na Simba kuzifunga Mamelodi Sundowns na Al Ahly.

"Hakuna kinachoshindikana kama wachezaji watajituma. Hizo timu mbili wanazocheza nazo zinafungika lakini ni lazima wachezaji wetu wajitume kwa dakika zote 180 ambazo watakabiliana nazo," alisema Mkapa.