Simba yaijazia KVZ mastaa Kombe la Muungano

Muktasari:

  • Simba ndio bingwa wa mwisho wa Kombe la Muungano ikilitwaa mwaka 2002 na baada ya hapo mashindano hayo hayakufanyika tena.

Simba imeweka hadharani kikosi chake kitakachoanza dhidi ya KVZ kwenye Kombe la Muungano muda mfupi ujao katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar huku ikiwa na kundi kubwa la nyota wake.

Katika mechi ya leo, Benchi la ufundi la timu hiyo limefanya mabadiliko manne tu katika kikosi chake kilichocheza dhidi ya Yanga na kupoteza kwa mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Jumamosi iliyopita.

Badala ya Hussein Kazi ambaye alicheza kwa dakika nyingi dhidi ya Yanga akichukua nafasi ya Henock Inonga, kocha Abdelhak Benchikha leo amemuanzisha Kennedy Juma kucheza nafasi ya beki wa kati.

Babacar Sarr ambaye alianza katika nafasi ya kiungo mkabaji, leo hatokuwepo uwanjani na nafasi yake amepangwa Mzamiru Yassin wakati nafasi ya Saido Ntibazonkiza ameanzishwa Ladack Chasambi.

Sadio Kanoute hatokuwepo pia leo na nafasi yake amepangwa Freddy Michael na ukiondoa hao, hakuna mabadiliko mengine katika kikosi kilichoivaa Yanga na kupoteza.

Kikosi cha Simba kinachoanza dhidi ya KVZ usiku huu  kinaundwa na Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, Che Malone, Fabrice Ngoma, Ladack Chasambi, Mzamiru Yassin, Freddy Michael, Clatous Chama na Kibu Denis.