Moyes kung’oka West Ham, mrithi apatikana

Muktasari:

  • David Moyes amefundisha timu sita tofauti katika maisha yake ya ukocha ambazo ni Preston North End, Everton, Manchester United, Real Sociedad, Sunderland na West Ham United.

London. Kocha aliyeondoa nuksi ya miaka 43 ya West Ham United, David Moyes ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huku nafasi yake ikitarajiwa kuchukuliwa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Hispania, Julen Lopetegui.

West Ham United imethibitisha jana kuwa imefikia makubaliano na kocha huyo kutoongeza mkataba wake baada ya ule wa sasa kufikia  tamati mwishoni mwa msimu huu.

“Kwa niaba ya kila mmoja ndani ya West Ham, napenda kutoa shukrani za kipekee kwa David kwa mchango aliotoa kwa klabu katika kipindi chake kama meneja.

“David amekuwa mweledi katika kufanya naye kazi na anaondoka akiwa na heshima yetu kubwa na heri nyingi.

“Anastahili kuwekwa katika daraja la juu kwa huduma alizoipa West Ham na tunamtakia kila la kheri kwa hapo baadaye,” alisema mwenyekiti mwenza wa West Ham, David Sullivan.

Akizungumzia uamuzi huo, Moyes alisema maisha yake ndani ya klabu hiyo yamekuwa ya kipekee.

“Nimefurahi kufanya kazi na kila mmoja ndani ya West Ham na napenda kushukuru Bodi kwa kunipa fursa ya kusimamia timu hii kubwa,” alisema Moyes.

Inaripotiwa kuwa uongozi wa West Ham United umefikia makubaliano na kocha wa zamani wa Wolves na timu ya Taifa ya Hispania, Julen Lopetegui.