Ken Gold yapanda Ligi Kuu Bara 

Muktasari:

  • Ken Gold ambayo awali ilijulikana kama Gipco FC ya mkoani Geita, imeshiriki Championship kwa misimu mitatu nyuma bila kupanda na sasa imekamilisha ndoto zake kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Baada ya kusota kwa misimu mitatu mfululizo bila mafanikio,  hatimaye Ken Gold imepanda Ligi Kuu baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya FGA Talents, leo.

Mabao pekee na ya kihistoria yaliyoipandisha timu hiyo yamefungwa na Mishamo Michael na Robert Mackidala na kuifanya Ken Gold ya wilayani Chunya Mkoani Mbeya kufikisha pointi 67 na kujihakikishia nafasi ya Ligi Kuu msimu ujao.

Mchezo huo ambao umepigwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa, Ken Gold ilihitaji ushindi tu ili kujihakikishia nafasi hiyo na haikufanya makosa na kufikia malengo yake.

Pointi 67 za timu hiyo zinaweza kufikiwa na Pamba Jiji tu iwapo atashinda mechi ya mwisho dhidi ya Mbuni baada ya leo kutakata kwa mabao 2-1 dhidi ya TMA na hivyo timu hizo zitapanda zote moja kwa moja.

Hata hivyo, kitendo cha Biashara United kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Pan African, yanaipa nafasi kubwa Pamba Jiji kutafuta japo sare katika mchezo ujao ili kujihakikishia ndoto yake ya zaidi ya miaka 20, bila Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Ken Gold,  Jumanne Challe amesema haikuwa kazi rahisi lakini kujituma kwa wachezaji na ushirikiano wa wadau ndio siri ya mafanikio. 

"Kazi haikuwa rahisi niwapongeze vijana walipambana, lakini sapoti ya uongozi, mashabiki na wadau ambao walitupa sapoti kwa muda wote na sasa tunataka kumaliza vinara wa Ligi tukiwa tumeshakwea Ligi Kuu," amesema Challe.