Kane aanza tizi Bayern Munich

Muktasari:

  • Kane aliumia wakati klabu yake ikivaana na Darmstadt kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani, lakini jana alionekana akifanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya Borussia Dortmund utakaopigwa Jumamosi ijayo.


Munich, Ujerumani. Staa wa Bayern Munich, Harry Kane juzi aliondolewa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya England baada ya kuumia kifundo cha mguu, lakini jana alionekana akifanya mazoezi.

Kane aliumia wakati klabu yake ikivaana na Darmstadt kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani, lakini jana alionekana akifanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya Borussia Dortmund utakaopigwa Jumamosi ijayo.

Bayern Munich juzi iliweka taarifa ikisema kuwa mshambuliaji huyo anafanya mazoezi mwenyewe kwenye uwanja wao wa mazoezi.

Kane alifanyiwa mabadiliko kwenye mchezo ambao timu yake hiyo ilishinda mabao 5-2 dhidi ya Darmstadt na alikosa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya England na  Brazili juzi.

Alikwenda England lakini akarejea Ujerumani haraka baada ya madaktari wa timu yake ya Taifa kujiridhisha kuwa hayupo fiti.

Nahodha huyo wa England, amekuwa na matatizo ya kifundo cha mguu kwa muda mrefu kuanzia alipokuwa akiitumikia Tottenham Hotspur, lakini hajakosa mchezo wowote wa Ligi Kuu ya Ujerumani, msimu huu akiwa ameshapachika mabao 31 katika michezo 26.

Hata hivyo, Bayern ambayo imetwaa ubingwa wa Bundesliga mara 11 haijasema kama mchezaji huyo atakosekana kwenye mchezo huo muhimu wa Jumamosi. Ikiwa imebakiza michezo nane lakini ipo nyuma ya vinara Bayer Leverkusen kwa tofauti ya pointi nane.