Jezi mpya Arsenal? Zaibua gumzo

London. Kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu juzi iliyodaiwa kuvuja kwamba ndiyo mpya ya Arsenal kwa msimu ujao, baadhi wakisema imefanana na chupa huku wengine wakisema ni jezi kali zaidi kupata kutokea kwa The Gunners.

Baadhi ya mashabiki Arsenal wameungana na wa Tottenham kuiponda jezi hiyo, ambayo hata hivyo haijathibitishwa kama ni jezi rasmi ya nyumbani ya Arsenal ya msimu ujao.

Ukurasa wa X (Twitter), uitwao Football Headlines uliweka picha ya jezi hiyo mpya ya Arsenal ambayo kwa mujibu wao ndio itatumika katika msimu ujao wa Ligi Kuu England na mashabiki baada ya kuiona walisema inaonekana kama chupa tu.

Mashabiki hao waliiponda jezi hiyo kutokana na rangi yake nyekundu inaonekana kama ni umbo la chupa.

Shabiki mmoja wa Arsenal aliandika: "Hata Adidas wanatufanyia utani wa kutengeneza jezi zenye nembo ya chupa kwetu sisi machupa."

Neno chupa limekuwa ni jina la utani la Arsenal katika kipindi cha hivi karibuni kutokana na kushindwa kumaliza kimafanikio misimu ambayo inaonekana kama wangekuwa mabingwa.

Iliwahi kuwa hivyo kwa msimu uliopita ambapo iliongoza ligi hadi dakika za mwisho ilipoanza kufanya vibaya na kuipa Manchester City nafasi.

Hivi karibuni washika mitutu hawa wamepoteza mechi ya ligi dhidi ya Aston Villa pia wakatolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich.

Kocha wao Mikel Arteta alisisitiza kwamba hawajafanya vizuri wiki iliyopita lakini bado wapo katika mbio za ubingwa na wanaamini watafanya vizuri.

Jana washika mitutu hawa waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolves na kufikisha pointi 74 zilizowawesha kupanda kileleni wakifuatiwa na Man City yenye pointi 73 na Liverpool yenye 71, ambazo zina mechi moja mkononi ukilinganisha na Arsenal.


Hata hivyo, sio wote wanaoziponda jezi hizo. Mitandao mbalimbali iliyoripoti madi ya kuvuja kwa jezi hizo, imesema ni kati ya jezi kali zaidi kupata kushuhudiwa kwa Arsenal.

Mtandao mmoja uliandika: "Jezi za kuvutia kupita maelezo (ambazo hakika mashabiki watazisubiri kwa hamu."

Huku shabiki mmoja wa Arsenal akiandika: "Hizi huenda ndio jezi zetu bora zaidi za nyumbani kuwahi kutokea."

Wewe una maoni gani?