Al Ahly watua Dar kwa tahadhari

Muktasari:

  • Katika mechi sita zilizopita baina ya Simba na Al Ahly, kila timu imepata ushindi mara mbili na zimetoka sare mbili

Msafara wa Al Ahly umewasili mchana huu Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya Simba, Ijumaa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa lakini imekiri kuwa italazimika kufanya kazi ya ziada kupata matokeo mazuri kutokana na ubora wa wapinzani wao.

Mkuu wa msafara wa Al Ahly, Hossam Ghaly, amesema kinachowapa wasiwasi mkubwa dhidi ya Simba ni uwepo wa kocha, Abdelhack Benchikha.
 

                       

Akizungumza na Mwananchi Ghaly ambaye ni kiungo wa zamani wa Ahly, amesema Simba ni timu bora kwa kuwa wamekutana nayo mara kadhaa, lakini sasa wana wasiwasi zaidi kwa kuwa ipo chini ya kocha mzoefu.

Ghaly aliyetwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika akiwa na Misri mwaka 2010 ni kati ya wachezaji wa heshima wa timu hiyo inaelezwa kuwa yupo hapa nchini ili kuhakikisha timu hiyo inafikia sehemu nzuri.

Alisema mechi yao ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa itakuwa ngumu kutokana na rekodi ya Benchikha ambaye kila walipokutana naye amekuwa akiwapa ugumu.

"Simba tunaweza kuifunga, Lakini nadhani kitu kinachotufanya tuwe na wasiwasi ni uwepo wa kocha Benchikha (Abdelhak), nadhani mnafahamu ubora wake kwa sasa na namna anavyojua kusimama na mbinu zake," alisema Ghaly.

"Nipo hapa kuhakikisha timu inapata wakati mzuri wa mechi hii ya Ijumaa (Machi 29), tunaamini makocha wetu watakuja na mpango mzuri wa kupata ushindi, hatujawahi kupata ushindi hapa kwa Mkapa tukicheza na Simba, hili ni eneo lingine ambalo linatufanya tuwe makini na mechi hii.

"Sina wasiwasi na kikosi chetu tutacheza kwa ubora wetu kupata matokeo mazuri ambayo yatatupa wepesi kabla ya mechi ya marudiano kule Cairo, tunataka kutetea ubingwa wetu msimu huu," alisema Ghaly aliyewahi kuitumikia Tottenham Hotspur ya England.

Benchikha anasifika kwa kusimamia ajenda moja mpaka mpaka mwisho wa msimu akiwa amewahi kufanya hivyo akiwa na RB Berkane ya Morocco na USM Alger, kisha zote akazipa makombe ya shirikisho.

Simba na Ahly zimeshacheza michezo nane, kila moja imeshinda nyumbani kwake michezo mitatu zikitoka sare kwenye mechi mbili, mmoja Dar es Salaam na mmoja Cairo Misri, kwenye mechi hizo Ahly imefunga mabao 12, huku Simba ikifunga saba.
Hata hivyo, kwenye Ligi ya Mabingwa hivi karibuni, mchezo huu ndiyo unatazamwa kwa umakini wa hali ya juu kwa kuwa ni mara ya kwanza timu hizo zinakutana kwenye mtoano.