‘Kariakoo dabi’ yakosa mwenyewe

Muktasari:

  • Kwa takribani wiki mbili, mashabiki wa klabu hizo walikuwa wakitambiana kila mmoja akivutia upande wake kuhusu ‘derby’ hiyo iliyozikutanisha timu hizo za mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam.

Siyo Emmanuel Okwi wa Simba au Ibrahim Ajib wa Yanga, aliyetoka uwanjani kifua mbele kwa kufunga bao katika mchezo wa jana.

Kwa takribani wiki mbili, mashabiki wa klabu hizo walikuwa wakitambiana kila mmoja akivutia upande wake kuhusu ‘derby’ hiyo iliyozikutanisha timu hizo za mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam.

Wakati Yanga ina makao makuu yake makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Simba ina maskani Mtaa wa Msimbazi.

Yanga na Simba zilivaana jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na miamba hiyo ilitoka sare ya bao 1-1, ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Matokeo hayo yanaiweka Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 16 sawa na Yanga, lakini ina uwiano mzuri wa idadi ya mabao.

Kabla ya mchezo huo, kelele za mashabiki kila mahali ni Okwi na Ajib, kila kona na mashabiki wa klabu hizo kila mmoja alikuwa akimtambia mwenzake kupitia wachezaji hao.

Mashabiki wa Simba walitabiri Okwi angekuwa mwiba kwa Yanga na wapinzani wao walijibu Ajib angewalaza mapema ‘Wekundu wa Msimbazi’, lakini hali imekuwa tofauti. Okwi aliyekuwa amevaa fulana nyekundu ndani iliyokuwa na maandishi ‘I love Jesus’, aliondoka uwanjani mikono mitupu kama ilivyokuwa kwa Ajib.

Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 57 kupitia kwa Shiza Kichuya kabla ya Yanga kusawazisha dakika ya 60 kwa bao la Obrey Chirwa.

Kichuya alifunga bao hilo baada ya kipa wa Yanga, Youth Rostand, kupangua kizembe mpira wa krosi uliopigwa na Okwi kutoka upande wa kushoto.

Rostand alipangua mpira ukamkuta Erasto Nyoni aliyetoa pasi ya mwisho kwa Kichuya aliyefunga bao hilo kwa shuti la karibu. Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, ameifunga Yanga mabao matatu tangu alipotua Simba.

Chirwa, alifunga bao hilo baada ya kupata pasi ya kiungo wa pembeni, Geofrey Mwashiuya, aliyepenyeza mpira uliowapita mabeki wawili wa Simba akiwemo kipa Aishi Manula.

Yanga na Simba zimekuwa na mchuano mkali wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu tangu ilipoanza kutimua vumbi Agosti 26.

Straika huyo wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ amerejea katika ubora wake na amekuwa na bahati na uwanja huo.

Mabeki wa Yanga Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ waliocheza pacha jana, walichuana vikali kumpa ulinzi Okwi, lakini aliwatoka na kufunga bao.

Okwi amefunga mabao manane, Ajib amepachika matano na kila mmoja anawania kutwaa kiatu cha dhahabu msimu huu.

Nahodha wa Simba, Method Mwanjali na Juuko Murshid walimpa ulinzi mkali Ajib aliyejiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu kutoka Mtaa wa Msimbazi.

Kivutio kingine katika mchezo wa jana walikuwa wachezaji wa nafasi ya kiungo Haruna Niyonzima wa Simba na Papy Tshishimbi wa Yanga waliotoa burudani ya pekee.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza Simba ilitawala mchezo kulinganisha na Yanga, lakini iliongoza kufanya madhambi. Simba ilicheza faulo 15 na Yanga 14.

Yanga ilifumua mashuti matatu langoni mwa wapinzani wao na Simba haikupiga shuti. Timu zote zilipata kona mbili kila moja.

Pia Obrey Chirwa, Dante, Ajib na Tshishimbi walicheza kwa ustadi na upande wa Simba walikuwa James Kotei, Haruna Niyonzima, Juuko na Mwanjali. Chirwa, mchezaji wa kimataifa wa Zambia, amefikisha mabao matatu katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Kichuya amefikisha mabao manne.

Timu hiyo iliwatoa Laudit Mavugo na James Kotei na kuingia John Bocco, Jonas Mkude. Yanga iliwatoa Geofrey Mwashiuya, Raphael Daudi na kuingia Emmanuel Martin na Pato Ngonyani.

Mchambuzi soka Ally Mayay alisema kipindi cha kwanza Simba ilicheza vizuri kwa kufika mara nyingi langoni kwa Yanga.

Nahodha huyo wa zamani wa Yanga, alidai Simba ilikuwa butu katika umaliziaji licha ya kutengeneza nafasi nyingi.

Beki wa Yanga, Gadiel Michael alisema wanashukuru kupata pointi moja kuliko kupoteza mchezo na wanajipanga kwa mechi zijazo.

“Tumecheza vizuri na matokeo ndio hayo tunashukuru kupata sare kuliko tungepoteza,” alisema Gadiel.

Naye Kichuya alisema kuwa makosa katika timu zote mbili yalizigharimu timu hizo na mchezo kumalizika kwa kutoka sare.

“Yanga walifanya makosa tukatumia kufunga na sisi tulifanya makosa na wenzetu wakasawazisha,” alisema Kichuya.

Yanga: Youth Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Pius Buswita, Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi, Ibrahim Ajib, Raphael Daudi na Geofrey Mwashiuya.

Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Method Mwanjali, James Kotei, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, Emmanuel Okwi, Laudit Mavugo na Shiza Kichuya.