Hatutadhibiti tindikali kwa kukurupuka

Muktasari:

  • Tamko hilo pia linawataka wanaouza kemikali hatarishi, mbali na kujisajili pia kuhakikisha wanafuata taratibu zote za usalama wa kemikali hizo, ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu za kila kemikali husika kama inavyoelezwa katika vifungu 16(f) na 28 vya sheria hiyo pamoja na maelekezo yatakayotolewa na Mkemia Mkuu.

Gazeti hili juzi lilichapisha habari za uchunguzi katika ukurasa wa kwanza kuhusu jinsi tindikali inavyouzwa kama njugu jijini Dar es Salaam. Pamoja na kushuhudia watu wakiuziwa kemikali hizo kiholela pasipo kuzingatia sheria husika, waandishi wetu pia waliweza kununua kiasi kikubwa cha kemikali hizo kirahisi pasipo kutakiwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.

Uchunguzi huo ulitegua kitendawili cha muda mrefu kuhusu sababu za kuongezeka kwa vitendo vya kumwagia watu tindikali, vitendo ambavyo vimeacha maswali mengi pasipo majibu, hasa kwa kutilia maanani kwamba matumizi ya kemikali hizo kwa wingi hayawezi kuwapo kama mamlaka husika zingekuwa zinaweka udhibiti wa kutosha wa kemikali hizo.

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu licha ya kuongezeka kwa vitendo hivyo vya kinyama, Mkemia Mkuu wa Serikali jana alikurupuka na kutoa tamko kali kuhusu udhibiti wa tindikali na kusisitiza utekelezaji wa Sheria Namba 3 ya mwaka 2003 (Sura ya 182) kuhusu Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani.

Tunasema alikurupuka kwa sababu tamko lake halionyeshi kutolewa kwa umakini kulingana na wakati tuliopo, kwa maana ya kutilia maanani mazingira halisi ya nchi yetu hivi sasa, bali lilitolewa kwa msukumo wa jamii na pengine mamlaka za juu katika kutaka majibu ya haraka kuhusu matukio hayo.

Tamko lake limetolewa eti kuwakumbusha wadau wote wa kemikali kujisajili na mwisho wa kufanya hivyo ni Novemba 30 mwaka huu.

Tamko hilo pia linawataka wanaouza kemikali hatarishi, mbali na kujisajili pia kuhakikisha wanafuata taratibu zote za usalama wa kemikali hizo, ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu za kila kemikali husika kama inavyoelezwa katika vifungu 16(f) na 28 vya sheria hiyo pamoja na maelekezo yatakayotolewa na Mkemia Mkuu.

Hakufafanua maudhui yaliyomo katika vifungu hivyo, wala kusema ni wakati gani Mkemia Mkuu atatoa maelekezo kuhusu kemikali hizo.

Tatizo tunaloliona hapa ni kuzembea au kushindwa kwa Ofisi ya Mkemia Mkuu kutoa elimu na uhamasishaji kwa umma ili waielewe sheria hiyo ya matumizi ya kemikali.

Kumbe sheria ipo na kwa kiasi fulani inajitosheleza, kwamba waagizaji, wauzaji na wasafirishaji wa kemikali wanatakiwa kwa mujibu wa sheria hiyo kujisajili kwa Mkemia Mkuu.

Huu ni uthibitisho kuwa, baada ya Bunge kupitisha sheria hiyo mwaka 2003, Mkemia Mkuu alifungia nakala zake kabatini badala ya kuhakikisha wadau wote wa kemikali wanaifahamu sheria hiyo vizuri na zinawekwa taratibu stahiki za kutoa elimu ya sheria hiyo mara kwa mara.

Ni kichekesho kwamba wadau wote wa kemikali wawe wamesajiliwa ifikapo Novemba 30. Hii inaonyesha kwamba Mkemia Mkuu hatambui kwamba wadau wote hawaishi katika miji mikubwa ambayo ina mawasiliano mazuri.

Kwa kuwataka wadau hao wajisajili kwa kujiandikisha kupitia mtandao wa chemis.gcla.go.tz anadhihirisha kwamba hajui hali halisi na mazingira ya wadau wanaoishi mikoani au katika miji midogo na vijiji ambako hakuna mitandao na mawasiliano ya aina hiyo.

Ni vyema Serikali ikatambua kwamba udhibiti wa matumizi mabaya ya kemikali unahitaji umakini na ubunifu wa hali ya juu.

Tunapendekeza sheria husika ifanyiwe marekebisho ili iweze kwenda na wakati, hivyo elimu ya umma ni muhimu ili uwepo udhibiti shirikishi wa matumizi ya kemikali hizo.