Usilete saikolojia ya shuleni kwenye maisha

Muktasari:

  • Tatizo langu mimi niliitazama picha ile kwenye taswira ya mtoto na mtu mzima, siyo kifaranga na jogoo. Ilinikumbusha jinsi mtoto wa kiume anavyojitengenezea utawala wake kungali mapema sana. Kinachomwangusha ni uwezo wa kujitafutia misosi na mabavu ya kumdunda baba anaporudi kutoka ulevini na kumsumbua mama.

Hivi karibuni niliona klipu ya kifaranga kikipigana na jogoo. Haikuwa ya kutengenezwa kwa maana ya vikaragosi, bali ni kweli mpita njia alikutana na tukio hilo akaamua kulichukua kwa kamera ya simu yake. Nilipoiona nilicheka sana. Wenzangu waliponiuliza kilichonichekesha kiasi kile, nilicheka zaidi hadi wakadhani nimepiga “cha Arusha”. Hata hapa naandika ningali nacheka tukio hilo.

Tatizo langu mimi niliitazama picha ile kwenye taswira ya mtoto na mtu mzima, siyo kifaranga na jogoo. Ilinikumbusha jinsi mtoto wa kiume anavyojitengenezea utawala wake kungali mapema sana. Kinachomwangusha ni uwezo wa kujitafutia misosi na mabavu ya kumdunda baba anaporudi kutoka ulevini na kumsumbua mama.

Lakini jinsi anavyomtazama baba yake utajua tu kwamba anamuonya kimoyomoyo: “We ngoja tu nikue!” Kwa kawaida mtoto wa kiume huwa rafiki wa mama, wakati mtoto wa kike huwa karibu na baba yake. Sababu ni kwamba mwanamke hutegemea ulinzi wa mwanamume hata awe mdogo kiasi gani, na wanaume hupenda kuwa walinzi wa wanawake. 

Kule katika mikoa ya bara kulikuwa na utamaduni wa wanawake kumtanguliza mtoto wa kiume wanapokwenda safari. Imani zao zinawaongoza kuwa wamemtanguliza kiongozi atakayewatetea na kuwalinda safarini.

Ilikuwa sawa kwenye mfumo dume, kwani mtoto wa kiume ukimsumbua mama yake njiani atakupopoa kwa mawe. Kwa bahati nzuri wasumbufu nao walijua kwamba wakimchapa kidume huyo watakuwa wametangaza vita na baba zake. Hivyo mtoto alikwenda kifua mbele akiamini kwamba anawalinda mama na bibi zake. Aliendelea kufanya hivyo kwa kumlinda mkewe pale alipokua na kuoa.

Hivi sasa mambo yanabadilika kwa kasi kutokana na teknolojia na utandawazi. Baadhi ya tamaduni na mifumo dume imepigwa chini. Hivyo akinamama kwa kuwa wameingia kwenye mfumo wa “fifte-fifte” wamekuwa wakijilinda wenyewe (kama singo maza), au kulindwa na sungusungu ambao baadhi ya sehemu ni watu hatarishi. Watoto sasa wanakuwa chini ya Madam huko mashuleni wakati wote.

Ule utamaduni wa kijana kumlinda mamaye au binti kulindwa na babaye umekwisha. Watoto wa leo hawana cha kujifunza kutoka kwa wazazi wao. Wengine hawaonani na familia hadi nyakati za likizo. Na hata wanaporudi wengi wao huwa wameshabadilishwa lugha: “Yes Madam” na “Yes Sir” badala ya “Ndio baba” na “Ndio mama”.

Kwa upande mmoja watoto wa kike wamekuwa na maendeleo na fursa nyingi zaidi ya kaka zao. Ni kwa sababu ya hamasa zinazoendelea duniani kote katika kumuinua mtoto wa kike. Ni jambo zuri sana, lakini kwa upande wa pili watoto wa kiume wanaangukia pua kwa ukosefu wa fursa hizo. Hakuna taasisi zinazowekeza nguvu zao katika malezi ya mtoto wa kiume.

Sababu hii inawafanya vijana kuwa dhaifu sana kwenye ndoa. Mwanzoni nimesema kuwa mtoto wa kiume alikuwa akijitengenezea utawala tangu mapema, na hii inatokana na silika yake kama mvulana. Anapokemewa kufanya hivyo hudhani anaonewa, hivyo kujitafutia kautawala kake nje ya familia.

Mara nyingi tumekuwa tukiwapoteza watoto wa kiume kwani hufikia hata kutoroka shuleni ili kwenda kuendeleza mfumo dume mtaani.

Hivi sasa umefikia wakati mgumu kwani hata wasichana walio tayari kuolewa wanakosa vijana wa kuwaoa. Hata wale wanaobahatika kuolewa hawadumu kwenye ndoa, maana vijana hawataki kuendeshwa na wasichana. Tena umkute huyu aliyetoroka shuleni kwenda kuendeleza kale kamfumo ndiyo kabisaaaa... hawatachelewa kutiana mangumi na kijana kukimbia RB ya Polisi.

Hali inazidi kuwa ngumu pale watoto wanapolelewa na singo maza. Tusiongopeane, maisha ya sasa ni magumu kwa malezi ya upande mmoja. Hivyo inambidi mama kutafuta madoni wa kumsaidia baadhi ya masuala kama karo za watoto mashuleni. Watoto nao (hasa wa kike) kwa jicho la kisogoni wanajifunza kitu kipya kutoka kwa mama yao. Kuna hatari wakaharibu masomo katika kupraktizi usingo maza.

Hivi sasa waganga wa kienyeji na wachungaji wamekuwa na soko kubwa la watu wanaotatizika kwenye mahusiano. Kuna wimbi la wanaotafuta ndoa, na wengine fedha za kukidhi mahitaji kama yale. Mimi silioni hili kuwa suluhisho, maana wa kweli wangemwambia mhusika arudishe mkanda nyuma na kuanza upya. Lakini vinginevyo nao wanaweza kumfanya kuwa mtaji kwa kumchanganyia mapichapicha ili mradi aendelee kutoa hela.

Saikolojia ya shule inasema ukiwa na misongo usikae kimya bali uongee na watu (u-share) ili kuipunguza. Lakini saikolojia ya maisha inakataa jambo hilo. Ukiongea hovyo matatizo ya nyumbani kwa watu, ujue unasambaza sumu. Ni kwa sababu utaishia kusema “Jirani akanielekeza kwa mganga”, na hapo ndipo nawe unawaelekeza wenzio kwa mganga huyo. Tiba ya kweli ni kuyarekebisha hayo hapo juu.