Rais Samia anaongozwa na falsafa gani katika uongozi wake?-5

Dhana ya mageuzi imezoeleka sana kwenye medani za siasa na uchumi. Si wakati wote mageuzi yanaanza kwenye fikra kwanza; kuna wakati mageuzi huanza  kutekelezwa kwenye vitendo ndipo yakatafsiriwa kifikra. Sisi wanadamu tunajifunza mengi kutokana na maisha ya wanyama wa aina mbalimbali wa nchi kavu, majini na angani.

Kuna filamu moja sikumbuki jina ila ilikuwa inaonesha mbinu za kujihami ambazo paka anatumia akikutana na nyoka ana kwa ana. Kwanza anajinyoosha tambarare, kisha anaunyanyua mkia juu na kuukunja kidogo kule kwenye ncha unapata umbo la nyoka aliyeinuka.

Halafu anautikisa mkia wake na kuupeleka kulia na kushoto. Hapo vyoka ndipo anainuka amgonge na paka anamng’ata shingoni na kumaliza kazi.

Mfano mzuri wa mageuzi ni pale Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina alipo watangazia Watanzania wenye sifa na uwezo waombe nafasi za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma kwa ushindani. Japo mja ni mzito na kwamba suluhu huibua changamoto zingine, lakini haijambo watajitokeza wenye uwezo.

Hapo tunapata elimu kubwa kwamba kabla hujachukua hatua kwanza, tulia usiwe na kiherehere, fanya subira na utafakari ni kwa namna gani utafanikiwa katika hilo kusudio lako hata kama umelizoea.

Hali ya hewa hubadilika na mazingira pia. Mazingira ya miaka ya 80 kwenye kisomo cha watu wazima cha akinamama Asia Mfaume Kawawa na wataalam wenzie, kiliwezesha kufikia asilimia 85 ya wahitimu. Miaka 40 baadaye mazingira yamebadilika na kiwango kimeshuka.

Mwaka 2023 vijana wengi walimaliza darasa la saba na mahitaji yao sio kama ya wazazi wao. Fursa wanazotaka ni tafauti na zinakinzana na desturi, imani au sheria za nchi. Utatumia mizani gani ili vijana wawe na haiba ya Kiafrika na wazalendo, wakati huo huo wabebe mazuri ya utandawazi? Huo ni mfano wa mtanziko ukitaka mageuzi karne ya 21.

Rais SSH kama kiongozi mkuu, tena mwanamke amelipa uzito suala la mageuzi kwenye falsafa yake kwa kuelewa kwamba, muwa umefika kwenye kifundo. 2024 ni mwaka wa Uchaguzi  Serikali za Mitaa ukifuatiwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ni muhimu Taifa liwe na fikra zilizokomaa lijielewe, lijiamini na lijitathamini ili vyama vya siasa vinavyotaka kuweka wagombea nafasi mbalimbali na wananchi tujadili na kufikia muafaka.

Yako wapi maridhiano ya mustakabali wa Tanzania tuitakayo, ambayo yataimarisha uvumilivu wenye tija  na mshikamano wa Taifa katika kujenga upya pale palipo bomoka. Hili ni jukumu la kila Mtanzania ili baadaye tusije tafuta mchawi.

Kawaida ya mageuzi ni kuacha mazoea na kuelewa kwamba kuna machungu yatageuka matamu na matamu yatakuwa machungu.

Mazoea huwa magumu kutoka akilini na katika vitendo kwa hiyo ni suala la mchakato, hatua kwa hatua kwani maridhiano na uvumilivu ndio chachu ya kuleta mageuzi.

Tuchukue mfano wa ndoa, mnapoanza uchumba lugha yake huwa tamu na hasa mkiwa mbalimbali basi hamu yakuwa karibu ina panda. Mkijaliwa kuwa na wapambe na ndugu wema mshukuru Mungu, kwa kawaida lazima kutakuwa na wapambe nuksi ndumila kuwili.

Ndio maana ndoa ina wageni wanne wa kwanza ni heshima yeye ni mtulivu, lugha na vitendo vyake ni vya kuleta furaha na amani. Wakati huu hata msipoongea jicho pekee linatosha. Mnapodhani kuwa sasa mnaelewana ndipo mgeni wa pili anaingia anaitwa mazoea.

Huyu ni tofauti na heshima, yeye anajiona ni mwenyeji anakujua wewe mwanzo mwisho na anakuona wa kawaida tu. Kama ni mume alikuwa hali chakula nje, basi atakula anakokujua akirudi usimuulize.

Kama ni mke alizoea kukupokea waaaooo unapotoka kazini ndio kwanza atakwambia maji ya kuoga chota bombani kama una njaa angalia kwenye hotipoti. Hizo ni dalili kuwa mgeni wa tatu dharau kafika. Dharau anamkaribisha sijali kirahisi kwani, anawakumbatia wabaya wenu akidhani ndio wema wake. Na mchakato wa mageuzi ndio hivyo.

Tatizo sio watu bali ni namna tunavyorithi na kuiga mifumo na tunavyoitumia bila kutafakari faida na hasara zake. Tunapenda kusema hii ni mila na desturi ya kiafrika. Afrika gani na ni upi utamaduni wa Mwafrika? Utamaduni wa mwafrika ni ule wenye manufaa na wenye maslahi kwa mwafrika anzia hapo.

Tunaambiwa hatujachangia chochote kwenye ustawi na maendeleo duniani iwe kwenye sanaa, sayansi au teknolojia, je ni kweli? Eti sisi ni maskini, kama ni maskini kwa nini wanakuja kwetu kujitajirisha?

Kabla hatujawalaumu inabidi tujiulize; kama bara la Afrika ni tajiri kwa nini watu wake ni maskini! Chanzo cha umasikini na ufukara ni nini? Je umasikini na ufukara wetu ni wa kifikra yaani bongo lala! Lazima tutafakari.!

 Itaendelea kesho