NIKWAMBIE MAMA: Tiba ya awamu huunusuru mwili

Kwanza nichukue nafasi hii kukupongeza kwa dhati katika mchakato wa kuboresha Tume ya Uchaguzi. Hili limekuwa tatizo la muda mrefu kiasi cha kuwafanya wanaoathirika nalo kuona kama tatizo lililowekwa makusudi ili kuendelea kuwanyima haki. Baadhi ya viongozi waliotangulia katika awamu zilizotangulia waliliona, lakini ulikuwa ni mfupa uliomshinda fisi, hivyo mbwa hakuthubutu kuugegeda.

Kwa bahati nzuri katika sera yako ya maridhiano umeweza kuketi na waathirika wa jambo hili. Ukafikia kuanzisha mchakato unaoendeshwa na Tume ya kurekebisha sheria iliyoko chini Wizara ya Sheria na Katiba, ambayo inazunguka nchi nzima kukutana na wadau, ikiwamo vyama vya siasa kwa ajili ya kupokea maoni juu ya marekebisho ya sheria za uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.

Mchakato mzima unaendelea, huku kukiwa na mvutano mkali unaoendelea kutamalaki miongoni mwa watu binafsi, wanaharakati, wadau wa siasa, wanasiasa na serikali kwa jumla kuhusu uwezekano wa kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi. Madai ya Tume hii yanahanikizwa na hoja kwamba hakuna usawa katika siasa za Tanzania, bali wasimamizi wanasimamishwa kama vinyamkera wa chama tawala.

Bila shaka hili linakaziwa na malalamiko ya baadhi ya vyama vya siasa, na tathmini ya uchaguzi wa 2020 ambapo inaelezwa kuwa wengi wa Watanzania waliojiandikisha kupiga kura waligoma kutumia haki yao ya msingi kikatiba, na baadhi ya wagombea wa upinzani kudai kukumbana na matukio ya kutekwa, kuvamiwa na wengine kuenguliwa na wasimamizi wa uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali. Karibu vyama vyote vya upinzani vilitoa matamko ya kulaani na kukemea hali hiyo.

Lawama nyingi zilielekezwa kwa Tume ya Uchaguzi, ikilaumiwa kupendelea upande mmoja ambao ni wa chama tawala. Sababu hii ilizusha tatizo kubwa la ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya nchi yao baada ya uchaguzi. Watu wanapokosa imani katika uchaguzi, wataendelea kukosa imani kwa yeyote atakayeibuka kuwa mshindi hata kama mshindi atakuwa ni yule waliyempigia kura.

Tatizo la Tume ya Uchaguzi ni mtambuka na halina tofauti na ugonjwa. Mimi nilikuwa miongoni mwa watu waliogombezwa na madaktari baada ya kuwaambia “naumwa malaria”. Kila daktari niliyemweleza hivyo alinisahihisha: “Sema kinachokusumbua, vipimo ndio vitaonesha iwapo ni malaria au ugonjwa mwingine”. Ni kweli wagonjwa wa malaria hulalamikia homa, lakini homa inaweza kuwa dalili ya ugonjwa mwingine tofauti na malaria.

Inawezekana tatizo kuu ni jingine, au kuna matatizo ya ziada kwenye mifumo. Lakini kinachoonekana kwanza ndicho kinachodhaniwa kuwa tatizo la msingi. Inawezekana tatizo hili likaondolewa na kila mmoja akakubaliana na mabadiliko, lakini mabadiliko hayo yasikidhi mahitaji ya wananchi katika ushiriki wa uchaguzi huru.

Kwa mfumo uliopo, haiwezekani Tume iwajibike kwenye mhimili tofauti na mteuzi wake. Kamwe haijatokea mtoto wa mamba akamfuata kiboko mara baada ya kutotolewa; huu ndio utaratibu wa maumbile ulivyo. Hili ndilo tatizo kubwa linalovisibu vyama vya siasa na wadau wengine walio nje ya chama tawala. Pengine mwenyekiti na wasimamizi wa uchaguzi wasingetokana na uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano mambo yangekuwa tofauti na ilivyo sasa.

Kuna mawazo ya kwamba Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi awe ni mtu asiyetokana na mifumo ya uongozi, bali awe anajitegemea kwa shughuli zake na vyanzo vya mapato binafsi. Ni wazo zuri katika kumuepusha na utegemezi wa Serikali na vyama, lakini tukikurupuka kufikia hapo tunaweza kulipata “zungu la unga” katika nafasi hiyo. Tutakuja kuzinduka wakati nchi yetu imeshakuwa hatarishi zaidi ya Colombia.

Hivyo kwa vile umeliona tatizo hilo hapo juu, bila shaka kikosi kazi ulichokituma kuratibu mchakato wa marekebisho ya sheria ya uchaguzi kitafanya kazi yake kwa weledi na uadilifu na kukuletea mapendekezo muhimu. Ujasiri wako wa kuyaanzisha haya unanipa picha ya kutohofia lolote kwenye maamuzi utakayoyafanya kwa maslahi ya Taifa na ustawi mpana kwa vizazi vijavyo.

Pamoja na baadhi ya wanasiasa kudai yaanze kutatuliwa masuala makubwa kama mabadiliko ya Katiba, lakini kwa maoni yangu mtu anayeumwa tumbo, kichwa, miguu, kifua na viungo vingine hutibiwa kwa awamu. Vilevile kwa kuwa malalamiko kwenye mfumo ni mengi sana, tusijiongopee iwapo tukiibadili Katiba tuliyonayo ndio tutakuwa tumemaliza matatizo. Mataifa mengi, yakiwemo ya jirani walibadili katiba, lakini yapo kwenye mizozo hata hivi sasa.

Binafsi nadhani hatua uliyoichukua ya kuketi pamoja na vyama vya upinzani ilikuwa ni mwanzo mzuri na hatua muhimu ya kupelekea mabadiliko ya mifumo inayolalamikiwa. Naamini pia utatuzi wa kero za sheria ya uchaguzi huenda ukatoa nafasi kwa mengine yaliyosalia. Huku uswahilini huwa tunaukata mti mrefu kwa awamu kuanzia matawi, ili usije kuangukia nyumba na kuharibu makazi.

Niwaombe tena wanasiasa na wadau wasiwe na haraka kwenye mambo ya msingi kama haya. Hatua moja huzalisha nyingine, na hatimaye safari huisha. Waswahili walisema “ukitaka kuruka mtaro patana na nyonga,” kwa maana usije ukajilaumu na matokeo yake. Kama pale mwanzo hawakusikilizwa hata kwenye moja ya maoni yao, kuna ubaya gani yakianza kutekelezwa kwa awamu?