Nani anawajibika ulinzi wa walimu kazini?

Usalama wa mwalimu awapo kazini ni suala muhimu linalomwezesha atekeleze majukumu yake ipasavyo.

Usalama humfanya mwalimu awe na ari ya kupenda kazi yake na kuongeza ubunifu katika kuboresha ujifunzaji na ufundishaji.

 Mwalimu ni mlezi na mzazi wa wanafunzi, ambaye mara zote huhakikisha maadili na nidhamu za wanafunzi vinaakisi malengo ya mtalaa unaotekelezwa.

 Wakati kada nyingine kama jeshi, huhitaji ulinzi kwa watoa huduma, walimu wanaosimamia kundi kubwa la wanafunzi, hujikuta wakifundisha pasipo hofu ya usalama wao.

 Hali hii hutokana na imani waliyonayo kwamba wanafunzi ni watoto wao ambao wanapaswa kuwachukulia kama walezi; yaani mabadala wa wazazi.

Hofu ya usalama siku hizi imewalazimu hata wa wajiitao watumishi wa Mungu kupanda madhabahuni wakisindikizwa na mabaunsa. Wanasiasa pia wanahutubia wakiwa na walinzi pembeni.

 Hii yote ni katika kuimarisha usalama kazini. Huenda hata usalama wa mwalimu kazini unapaswa kuimarishwa kwa mtindo huu.


Hali halisi

Hali ya walimu kuhisi ni wazazi inaonekana kupoteza maana, kwani wanafunzi hawathamini dhana hii, jambo linalochangia kuhatarisha usalama wa mtoa huduma.

 Hivi karibuni imetokea sintofahamu kwa wanafunzi kuwadhuru walimu wanapotekeleza majukumu yao, jambo linatohatarisha usalama wa mwalimu kazini.

 Machi, 27, 2024, gazeti hili liliripoti habari ya mwanafunzi wa kiume wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Mwika, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, aliyempiga mwalimu kichwani kwa kutumia chepe na kumsababishia majeraha.

 Tukio hilo lilitokea usiku wa Machi 25, 2024 wakati mwalimu huyo aliyetambulika kwa jina moja la Matendo, alipokuwa akizunguka kukagua wanafunzi waliokuwa wanajisomea usiku.

 Ilidaiwa kuwa mwalimu alipokuwa akifanya ukaguzi, alivamiwa na mwanafunzi huyo aliyemjeruhi kisha kutoroka shuleni hapo.

 Septemba 4, 2020, Jeshi la Polisi mkoani Mara, lilithibitisha kumtia nguvuni mwanafunzi, Mwita Machamo (17) wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Kiagata aliyedaiwa kumkata kwa panga mwalimu wa shule hiyo, Majogoro John.Chanzo tukio hilo ni mwanafunzi huyo kushindwa kumpeleka mzazi shuleni alipotakiwa kufanya hivyo.


Uko wapi usawa?

Matukio haya yaliripotiwa pasipo kupewa uzito sawa na matukio ya ukatili ambayo walimu hudaiwa kufanya.

 Kwa mfano, tukio lililotokea jijini Mbeya Oktoba 06, 2016 ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya walimu wa shule ya Mbeya Day waliodaiwa kumshushia kipigo mwanafunzi, wa kidato cha tatu, Sebastian Chinguka.

 Hatua hiyo ilikuja baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mwanafunzi huyo akipigwa kikatili na walimu.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mwanafunzi huyo kutofanya zoezi la somo la Kiingereza. Taarifa zilieleza kuwa walimu waliofanya kitendo hicho walikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo.

 Hapa simaanishi video zinazoonesha walimu wanapowapiga wanafunzi zisambae katika mitandao ya kijamii, ila itoshe tu kusema kwamba uzito unaochukuliwa mwalimu anapodhurika si sawa na pale mtoto anapokuwa amefanyiwa ukatili na watoa huduma yaani walimu.

 Jambo la kusikitisha ni pale baadhi ya majina ya wanafunzi waliofanya vitendo hivi viovu yanapofichwa kwenye vyombo vya habari kwa kile wanachodai ni kulinda usalama wao.

 Hapa unaweza kujiuliza; usalama wa mwalimu ambaye ni mbadala wa mzazi mlezi uko wapi?


Uzoefu wangu Arusha

Miaka 10 iliyopita nikiwa mwalimu mkoani Arusha, wanafunzi walikuwa hawaambiliki.

 Utovu wa nidhamu ulikithiri na kusababisha taaluma shuleni hapo kushuka kwa kiwango kikubwa, ambapo kwa mara ya kwanza tulisikitishwa na matokeo ya wanafunzi 56 yakiwa ni daraja sifuri kati ya wahitimu 340.

 Chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa taaluma shuleni hapo, kilikuwa ni wanafunzi kuwadharau walimu. Ilikuwa ni nadra kuwakusanya mstarini ili kuwapa maelekezo.

 Kipindi hicho wanafunzi waliwapopoa mawe walimu mstarini na kutawanya wakati mkuu wa shule akitoa maelekezo.

 Sintofahamu hiyo iliweza kudhibitiwa na aliyekuwa Kamanda wa polisi Wilaya ya Karatu, Mathias Nyange, kwa kuamua kuja shuleni hapo na kikosi cha askari wapatao 40.

 Wanafunzi katika shule hiyo walikuwa wakidai wali, upatikanaji wa maji ya uhakika na kushinikiza baadhi ya walimu kuondolewa kwa sababu walikuwa wakiwanyima uhuru wa kumiliki simu, kwenda mjini kwa muda walioona unafaa na kufundisha kwa kiwango duni.

 Kufuatia misukosuko hiyo, wanafunzi zaidi ya 60 walifukuzwa shule moja kwa moja. Angalau kwa sasa nidhamu ya shule hiyo imekuwa ya kuridhisha.

 Nimetoa kisa hiki kuufahamisha umma kwamba usalama kazini kwa mwalimu ni tete kufuatia uwepo wa vijana wenye umri wa balehe, amabo mara nyingi huwa na makundi rika yanayochangia kueneza tabia mbovu shuleni.


Hali nchi nyingine

Hali si shwari pia hata kwa nchi jirani ambapo usalama wa mwalimu kazini bado upo shakani.

 Mei mwaka jana, mwanafunzi wa kiume wa darasa la sita (shule haijatajwa), kaunti ya Garissa nchini Kenya, alizua taharuki baada ya kumshambulia mwalimu wake kwa kisu mara baada ya kuulizwa sababu ya kuwa mtoro.

 Kwa mujibu wa televisheni ya Citizen ya nchini humo, inadaiwa baada ya mwalimu wake kumuuliza hivyo huku akiongea kwa msisitizo ulizuka mzozo, baadaye mwanafunzi aliondoka darasani na kurejea akiwa na kisu na kumchoma mwalimu huyo sikioni.

 Baada ya tukio hilo mwalimu huyo wa kike alijeruhiwa vibaya na kukaribia kupoteza uwezo wake wa kusikia.

 Mwaka 2018 nchini Ufaransa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Saint-Jean-de-Luz, alimchoma kisu ubavuni mwalimu wa Kihispania, hali iliyoleta taharuki na kuilazimu wizara ya elimu nchini humo, kuahidi kuchukua hatua na kuimarisha usalama wa walimu kazini.


Mzizi wa tatizo

Kiini hasa cha matatizo ya utovu wa nidhamu, ni malezi na mazingira mabovu ya ujifunzaji na ufundishaji. Wanafunzi wa kisasa hawapendi sana kufuatiliwa na walimu vijana ambao mara zote hupenda kuheshimiwa.

 Katika mkanganyiko huo wanafunzi waliofika balehe huhisi wamepevuka kiasi cha kutotakiwa kufuata maelekezo. Wakati huo huo, walimu huhisi wanadharaulika na wanafunzi wasiofuta maelekezo yao.

 Mtaalamu wa saikolojia Mmarekani Erick Erickson (1902–1994), alitambulisha nadharia ya maendeleo ya kibinafsi inayoitwa: "Ericksonian Psychosocial Development".

 Nadharia hii inalenga kuelezea jinsi watu wanavyokua na kujenga utambulisho wao kupitia hatua mbalimbali za maisha.

 Kwa mujibu wa Erickson, kuna hatua nane za maendeleo ambazo kila mtu hupitia kutoka utoto hadi uzee, kila moja ikiwa na changamoto yake ya kisaikolojia ambayo inahitaji kushughulikiwa ili kufikia ustawi wa kibinafsi.

 Ni jukumu la kila mlezi, hasa walimu kujua mbinu za kushughulika na tabia za wanafunzi pasipo kuathiri usalama wao kazini.

 Lakini baadhi ya mbinu za uongozi katika shule za binafsi, huchangia mmomonyoko wa maadili ya wanafunzi na kuhatarisha usalama wa mwalimu.

 Kwa mfano, inapotokea mwanafunzi anakiuka taratibu, mmiliki wa shule kwa kuhofia kupoteza mteja, ambaye ni mwanafunzi muovu, humtaka mwalimu eti atumie saikolojia kuendana na tabia za ‘waovu hao.’

Wanafunzi shule nyingi za binafsi, hasa zisizo na wateja wa kutosha mara zote hutishia kuhamia shule nyingine pale wanapofuatiliwa nyendo zao kinidhamu, jambo ambalo hulea tabia zinazohatarisha usalama wa mwalimu kazini.

 Walimu pia wemekuwa hawaivi ipasavyo kimaadili wawapo vyuoni. Taasisi nyingi za elimu, badala ya kumjenga mwalimu kudhibiti nidhamu ya wanafunzi, hujikita zaidi kufundisha taaluma pekee ili kumwezesha amudu mbinu za kuongeza ufaulu awapo kazini.

 Uvaaji na lugha ya mwalimu awapo darasani, huchangia wanafunzi kumdharau na kuhisi ni kama mwenzao. Si ajabu kwa baadhi ya shule kukuta mwalimu anapopaswa kupewa heshima na wanafunzi darasani wakiwa wamesimama na kuwambia kauli kama: “Kaeni tu. Mimi ni mwenzenu, mnasemaje washkaji, halafu nawaona kama mna hali za kufeli feli hivi.”

Kauli za namna hii huwafanya wanafunzi wamuone mwalimu wao ni kituko na ikitokea akalazimika kutoa adhabu kwa wanaoshindwa kutekeleza majukumu yake, ndipo huibuka suala la kutunishiana misuli na kuhatarisha usalama wa mtoa huduma huyo.

 Vijana wa kisasa pia hawapendi kufundishwa na walimu wanaofuata sana sheria kama: kusahihishwa kwa kukosolewa sarufi katika insha, kufuatiliwa uhusiano wao wa kimapenzi, kurekebishwa lugha wanayotumia kwa wakubwa zao na mengineyo.

 Juhudi hizi za mwalimu kutaka mwanafunzi akae katika mstari zimekuwa zikisababisha mlezi huyu aonekane kuwa na tabia za kizamani.

 Mara nyingi walimu wanaofuata sana sheria na taratibu wamekuwa wakipewa majina kama: mnaa, mnoko, mkoloni, mzee baba na mengine mengi. Inapotokea mwalimu huyo akashikilia uzi bila msaada wa watoa huduma wenzake, ni lazima ahatarishe usalama wake kazini.


Wazazi nao chanzo

Wazazi pia hawako nyuma katika kusababisha mazingira ya usalama wa mwalimu kuwa shakani, hasa pale wanapohisi watoto wao ni maalumu wawapo shuleni kiasi cha kukataa kila adhabu anayopaswa kuitoa mwalimu.

 Wazazi wamekuwa wakisikika mara nyingi wakisema kwa mfano: “Siwezi nikalipa ada kwa wakati halafu nisikie mwanagu kapewa adhabu eti na mwalimu fulani kwa kosa fulani. Muda huo anaompa adhabu mwanagu anasoma saa ngapi?

 Hoja kama hizi zimekuwa zikizorotesha juhudi za walimu katika kurekebisha tabia za wanafunzi.

 Wazazi wamekuwa vinara wa kuhakikisha wanafunzi hawafanyi shughuli yoyote shuleni, kwa kile wanachodai baada ya kulipa ada na michango mingine, ni sharti taasisi husika iajiri watumishi wa kufanya kazi zote.

 Misimamo ya namna hii imekuwa ikihatarisha usalama wa mwalimu ambaye haridhiki labda na usafi wa darasa, unadhifu wa mwanafunzi pamoja na mwenendo wake kitaaluma, vinavyoweza kumlazimu kutoa adhabu stahiki ili kutunza nidhamu ya mwanafunzi pasipo kujua kuwa anahatarisha usalama wake kazini.