Kuokota chupa si laana tena, kwa sasa ni fursa ya kipato

Kijana Maulidi Athumani akipima chupa za plastiki anazozikusanya  mtaani na kuziuza jijini Dar es Salaamu. Picha na Maktaba

Muktasari:

Kwa utamaduni wa siku nyingi ambao ulizoeleka kabla ya teknolojia kuruhusu ufungaji wa bidhaa kwa namna tofauti zikiwamo chupa za plastiki, watu wenye upungufu wa akili pekee ndiyo walionekana majalalani wakiokota chupa na makopo.
Ilikuwa ni nadra mtu timamu kuonekana maeneo hayo isipokuwa kama anaenda kumwaga taka alizonazo.

Zamani ilikuwa ni laana kuambiwa utaokota makopo. Siku hizi ni fursa ya biashara inayokuza kipato cha wote wanaoweza kufanya hivyo.
Kwa utamaduni wa siku nyingi ambao ulizoeleka kabla ya teknolojia kuruhusu ufungaji wa bidhaa kwa namna tofauti zikiwamo chupa za plastiki, watu wenye upungufu wa akili pekee ndiyo walionekana majalalani wakiokota chupa na makopo.
Ilikuwa ni nadra mtu timamu kuonekana maeneo hayo isipokuwa kama anaenda kumwaga taka alizonazo.

Madampo mengi yalikuwa mbali na mji ambako magari ya taka na wafanyakazi wa halmashauri walikuwa wanasogea huko wakitekeleza majukumu yao. Hawa wangeweza kukutana na wagonjwa wa akili ambao wamekosa huduma hivyo kuyaacha makazi yao na kurandaranda majaani. Ingawa bado wapo mpaka sasa, wanasikitisha wakionekana.
Uchafu walionao; kuanzia mavazi, miili yao hata chakula wanachookota hakiwezi kutumiwa na mtu wa kawaida ambaye kuambiwa awe kwenye hali hiyo ilikuwa ni adhabu kubwa.
Kutokana na maendeleo ya kiuchumi na ongezeko la uhaba wa ajira rasmi, hivi sasa kuna wanawake, vijana hata wazee, wanaookota chupa hizi kujipatia kipato. Licha ya changamoto zilizopo, wanakabiliana nazo na kusonga mbele.
Bila kutambua ni lini mzigo wao utakuwa mkubwa na wenye kilo nyingi ili waweze kupata pesa itakayotosha kukidhi mahitaji yao muhimu mara baada ya kuuza.
Abdallah Njechele anasema amekuwa akitumia zaidi ya wiki moja kuzunguka mitaani, kwenye daladala, baa, shule hata hospitali kuokota chupa hizo.
“Jua, mvua, vumbi, njaa, kudharauliwa na watu vyote vinanisonga wakati natafuta chupa hizi kila mtaa ninaopita,” anasema.

Anasema baada ya kukusanya chupa huziuza kwa Sh250 kwa kilo bei ambayo ni ndogo ikilinganishwa na, nguvu na muda anaoutumia.

“Licha ya bei kuwa ndogo, huwa tunakatwa kati ya kilo mbili au tatu kwenye kila mzigo wa kilo 10 tunaouza. Huenda ikawa kilo tano katika kilo 20 kwa madai ya kufidia hasara,” anasema Njechele.

Mwanahawa Yusto hukusanya chupa hizi kwa kuwatumia wajukuu zake wanaozunguka mitaa mbalimbali kuzitafuta kisha yeye kwenda kuziuza. Anasema bei hiyo inayopangwa na watu wanaoenda kuuza kiwandani inawaumiza.

“Hatuna fedha ya kujikimu na wajukuu zangu wanaelewa hilo hivyo hawana budi kuingia mtaani kuzitafuta tuweze kununua chochote,” anasema bibi huyo.

Chupa wanazookota wajukuu wake, anasema huwa ni safi zisizo na madhara na ikitokea wakakuta kinywaji kilichobaki, hukimwaga kabla ya kuzipeleka kwa mnunuzi.

Wanunuzi

Mnunuzi wa jumla wa chupa hizo aliyepo Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam, Jackson Godfrey anasema kila mkusanyaji hukatwa baadhi ya kilo kulingana na mzigo alioleta ili kuweza kufidia hasara inayoweza kupatikana.

Anasema wengine wanaweka maji, mchanga hata haja ndogo ili kuongeza uzito. Inakuwa ngumu kukagua chupa moja baada ya nyingine endapo mzigo ni mkubwa. Anafanya hivyo kwa sababu hata yeye anapozipeleka kiwandani hukatwa kilo kadhaa kuondoa uwezekano wa kuwapo vitu vinavyoweza kusababisha hasara itokanayo na upungufu wa uzito.

Kuhusu bei anasema si wanunuzi wanaopanga. “Ni kiwandani, wakishusha bei nasi tunashusha. Zamani tulikuwa tunauza kilo moja kwa Sh550 hivyo sisi tulikuwa tunanunua kwa Sh400. Sasa hivi bei imeshuka, tunauza kwa Sh400 na tunanunua kwa Sh250.”

Viwanda

Msimamizi wa mitambo ya kusaga chupa katika Kampuni ya Bottles Investiment iliyopo Kurasini, Suleiman Msumi anasema chupa zinapofikishwa katika eneo hilo hukakuguliwa, kusafishwa na kuondolewa nembo ya biashara iliyobandikwa katika chupa hiyo. Nembo zinazoondolewa ni zile ambazo ni ngumu kuchakatwa.

Anatolea mfano chupa za maji ya dasani anazosema nembo yake ni ngumu na haisagiki kirahisi hivyo wanalazimika kuiondoa. “Nyingine zinawekwa hivyo hivyo kwani baada ya kusangwa huingia kwenye kinu chenye maji ambako chupa huzama chini na nembo zinaelea,” anasema Msumi.

Soko la chupa hizi lipo China. Msumi anasema baada ya hatua hiyo, chupa hukaushwa na kuwekwa katika viroba kwa ajili ya kusafirishwa na kuhitimisha mchakato unaofanywa Tanzania katika mnyororo wa biashara hiyo.

Msimamizi wa kampuni hiyo, Peng Hou anasema zikifika China, chupa hizo ni malighafi muhimu kwenye viwanda vya nguo na vitambaa vya aina mbalimbali. Kutokana na Serikali nchini humo kuweka sheria ya kudhibiti uingizaji wa malighafi kutoka nje, biashara imeshuka.

“Si kila nguo inatengenezwa kwa pamba kwa asilimia 100, ikiwa hivyo bei yake inakuwa kubwa na watu wanaweza wakashindwa kununua. Kinachofanyika, wanachanganya asilimia 80 ya malighafi iliyotokana na chupa hizi (polyster fibre) asilimia 80 na inayobaki huwa pamba. Hapa bei ya nguo inakuwa rahisi,” anasema Hou.

Anasema mabadiliko ya Sheria yamekusudia kuwalinda wafanyabiashara wa nchini humo na kuzipa heshima bidhaa za ndani.

Si kampuni za nje pekee zinazosafirisha chupa za plastiki kwenda nje ya nchi. Kampuni za Mohammed Enterprises (Metl) na Bakhresa (SSB) pia hufanya biashara hiyo na kuuza China ingawa viwanda vingi duniani vinatumia chupa hizo kama malighafi ya uzalishaji.

Kwa mujibu wa Kiwanda cha Oak Hall cha Marekani kinachozitumia kuzalisha nguo za aina mbalimbali, chupa 27 zinatosha kutengeneza joho moja.

Afya

Kama ilivyo kwa biashara nyingine, changamoto hazikosekani. Wataalamu wa afya wanasema umakini unahitajika kwa wote wanaojihusisha na biashara hii hasa waokotaji.

Dk Zeinabbas Ladha wa Hospitali ya Ibrahim Haji Dar es Salaam anasema kutokana na uwezekano wa chupa zinazotupwa maeneo mbalimbali kuwa katika hali tofauti ya kuunguzwa, kujazwa mkojo au vitu vingine vya ajabu, zinaweza kumsababishia muokotaji maambukizi mikononi au minyoo.

“Zikiwa zimeungua na mtu akala bila kunawa baada ya kuzishika anaweza kupata saratani ya mikono au tumbo kwa sababu plastiki zinazobanduka anaweza kuzimeza pasipo yeye kujua,” anasema.

Anasema kwa chupa zilizotoka hospitali zilizotumiwa na mgonjwa mwenye bakteria au virusi waokotaji wanaweza kupata maambukizi wasipokuwa makini.

Mtaalam wa masuala ya Jinsia na Maendeleo, Sultan Mhina anasema kuna tofauti kati ya kumfanyisha mtoto kazi kwenye ajira rasmi na kujiajiri kuanzia ngazi ya familia.

“Kuna tozo, kanuni na sheria zimewekwa sehemu rasmi ambazo zinatakiwa kufuatwa tofauti na kazi anayoagizwa na mzazi kama kuokota makopo au kitu kingine,” anasema Mhina.

Anasema changamoto iliyopo ni watoto kuishi katika mazingira magumu hivyo suala hilo kutoepukiki ingawa kuna mipaka ya kufanyishwa kazi.

Serikali

Biashara ya chupa imesaidia kuimarisha usafi wa maeneo mengi nchini. Ofisa Afya na Mazingira wa Jiji la Dar es Salaam, Enezael Ayo anasema zaidi ya watu 21,000 wanajishughulisha na uokotaji taka hivyo kupunguza kuzagaa kwake mtaani.

“Taka zimepungua kwa sababu zaidi ya tani 240 zimekuwa zikikusanywa kwa siku na kupelekwa viwandani. Usafirishaji wa chupa hizo pia unaliingizia taifa fedha za kigeni,” anasema Ayo.

Ofisa huyo anasema watu wanapaswa kubadili mtazamo juu ya taka za aina mbalimbali ili waanze kuziona fursa zilizopo. Anasema kuna mpango wa kuhamasisha kuzigeuza kuwa chanzo cha kipato kwa kuzielekeza kwenye utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama vile mikeka, mabomba ya maji au kamba za nailoni.

Tayari kuna vikundi vimeanzishwa jijini Dar es Salaam vinavyotumia taka ngumu kutengeneza mkaa mbadala na bidhaa nyinginezo.

Ofisa Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Christopher Nassari anasema vipo viwanda vilivyosajiliwa kwa ajili ya kufanya urejeleshaji wa chupa za plastiki maeneo tofauti nchini.